Mojawapo
ya wajibu wa kisheria wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kukagua
taarifa za wafanyabiashara ili kuhakiki usahihi wa kumbukumbu za
biashara.
Katika
kutekeleza zoezi hili, TRA imechukua hatua mbalimbali ikiwemo
kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kutunza kumbukumbu za
biashara na kusisitiza utumiaji wa mashine za kielektroniki za kodi
(EFDs).
Wakati
wa kutekeleza jukumu hilo TRA ilibaini wafanyabiashara wengi wanakiuka
sheria za kodi kwa kutokutoa risiti, hivyo wamekuwa wanachukuliwa hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria.
Vilevile
Mamlaka ya Mapato Tanzania imebaini kuwa kuna njama ya baadhi ya
wafanyabiashara kuhamasisha wenzao nchi nzima kufunga biashara kwa
makusudi endapo tutaendelea na ufuatiliaji na uhakiki wa bidhaa
zilizouzwa bila kutolewa risiti na kutekeleza agizo la serikali la
kusitisha matumizi ya kodi elekezi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini.
Njama hizi ni ukiukwaji wa sheria na hazipaswi kuvumiliwa.
Wafanyabiashara
na wananchi wote kwa ujumla wanafahamishwa kwamba kutokutoa risiti
baada ya kufanya mauzo au kutoa huduma ya kibiashara ni kosa la jinai
linalostahili adhabu.
Hivyo
wafanyabiashara wanatahadharishwa kutofunga maduka kutokana na sababu
zinazotolewa na wafanyabiashara wanaofanya njama hizo.
Endapo
TRA itawabaini wafanyabishara wanaokula njama hizi itachukua hatua kali
za kisheria dhidi yao ambazo zitapelekea kuzuiwa kufanya biashara moja
kwa moja hapa nchini.
TRA
inatoa wito kwa wananchi wote kudai risiti kila wanapofanya manunuzi na
kutoa taarifa za wafanyabiashara ambao hawatoi risiti. Vilevile
wanaombwa kutoa taarifa katika ofisi yoyote ya TRA za kuwafichua
wafanyabiashara wanaokula njama za kuhamasisha wenzao nchi nzima kufunga
biashara kwa makusudi.
Taarifa hizi zinaweza kutolewa pia kupitia namba za simu zifuatazo: 0800780078 au 0800750075.
Barua pepe
Huduma@tra.go.tz
au services@tra.go.tz
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Alphayo J. Kidata
KAMISHNA MKUU
0 comments:
Post a Comment