Thursday, March 17, 2016


Ikiwa ni siku tatu tangu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad, atangaze kuwa baadhi ya wananchi wa Zanzibar wanakimbilia porini kuhofia usalama wao, ametiwa mbaroni.

Kukamatwa kwa Masoud sasa kunafanya idadi ya viongozi wa chama hicho waliotiwa mbaroni na kuhojiwa polisi kufikia wanne tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka jana.

Viongozi wengine waliohojiwa na Polisi na kuachiwa kwa dhamana ni Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Alin Shehe na mshauri wa mikakati wa chama hicho, Eddy Riyami.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam, jana alithibitisha kukamatwa kwa Masoud, ambaye ni Waziri wa zamani wa Miundombinu na Mawasiliano katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alisema kiongozi huyo alikamatwa na kitengo cha upelelezi nyumbani kwake mtaa wa Mbweni mjini Zanzibar jana.

Alisema kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mwembe Madema ili kusadia uchunguzi juu ya taarifa alizotoa katika mkutano wake na waandishi wa habari na kuzungumzia hali ya amani ya Zanzibar na wananchi wake.

“Tunamshikilia kwa uchunguzi, kuna mambo ya msingi tunaona yanahitaji kufanyiwa uchunguzi na yeye kusadia polisi uchunguzi wake,” alisema Mkadam.

Kufuatia kukamatwa huko kwa Masoud, CUF imelaani kitendo hicho na kusema kuwa kamata kamata hiyo inawalenga viongozi wa chama hicho na wanachama wake pekee.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mazrui alisema matukio yote ya uvunjifu wa amani yaliyotokea visiwani hapa, yamekuwa yakihusishwa  na CUF na Jeshi la Polisi huwakamata viongozi wa chama hicho pekee.

“Tunasema huu ni uonevu wa hali ya juu, maana viongozi na wafuasi wa CUF pekee ndio wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi, hii yote inatokana na uchaguzi wa marudio, hivyo  kutoshiriki kwetu kwa uchaguzi isiwe sababu ya kuadhibiwa,” alisema.

Aidha, alisema suala la kushiriki au kutoshiriki katika uchaguzi ni hiari ya mtu, hivyo kwa wale ambao hawatashiriki uchaguzi huo, wasiadhibiwe wala wasidhalilishwe na wale ambao wametangaza kushiriki waende wakapige kura.

Kwa upande wa mke wa Masoud, Rahma Issa, alisema askari kazu wasiopungua sita wakiwa na silaha za moto mbili walifika nyumbani jana saa moja asubuhi na kudai wanamhitaji mumewe.

Alisema baada ya kubisha hodi, kijana wake mmoja alifungua mlango na kisha askari watatu waliingia ndani mmoja akiwa na silaha ya moto kifuani.

“Baada ya kuamshwa na kutoka chumbani walimwambia yupo chini ya ulinzi anahitajika kituo cha polisi,” alisema Rahma.

Hata hivyo, alisema baada ya kumkamata, hawakumwambia sababu ya kukamatwa kwake, lakini baada ya kuwauliza wanampekeka kituo gani walimwabia Kituo cha Polisi Mwembe Madema, Zanzibar.

Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema vitendo vya kukamatwa viongozi wa CUF ni mwendeleo wa Serikali ya CCM kuwanyanyasa viongozi na wanachama wake chama hivyo visiwani hapa.

Alisema vitendo vnavyoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi vinakwenda kinyume cha misingi ya demokrasia na haki za binadamu.

Shehe alisema matunda ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya kujenga amani na umoja wa kitaifa yameanza kuvurugwa tangu kuingia mgogoro wa uchaguzi mkuu.

0 comments:

Post a Comment