Saturday, July 25, 2015

UCHAMBUZI WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO, 2015

UTANGULIZI

Sheria hii ya Makosa ya Jinai kupitia Mtandao, 2015 ina mapungufu mengi. Mapungufu hayo yamebainika kuwa, kama sheria ikipita yanaweza kuifanya nchi ikawa ni kati nchi adui za matumizi ya mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano duniani.

Watanzania wote wanatakiwa kufahamu kuwa muswada ukipita utatumika nchini kote yani Tanzania Bara na Visiwani.

Watanzania walio wengi hawafahamu Sheria hii inawahusu kwa namna gani; lakini kwa lugha rahisi ni kuwa itamuathiri mtu yeyote anayeweza tumia Mtandao wa Intaneti kwa kutimia kifaa chochote iwe kompyuta kubwa au vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi kama kompyuta kama Simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyoendana na hivyo.

Malengo ya Sheria hii ni kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.

Matumizi ya mitandao yote mikubwa kama Twitter, Instagram, JamiiForums, Facebook, Barua pepe, WhatsApp, blogu na data zote zilizo katika kifaa chochote cha kielektroniki yanaathiriwa kwa kiwango kikubwa na Muswada huu.

UCHAMBUZI

Kifungu cha 7 
(1-3): Haibainisha ni aina gani za data ambazo haziruhusiwi kuguswa/kufutwa au zikiguswa/futwa ni kosa la jinai.

7(1g): Kipengele hiki katika kifungu hiki kinarudiwa mara kadhaa katika (Vifungu vya 32-35). Badala ya vifungu vya mbele kurejea kifungu hiki, watunga sheria wameiacha kifungu hiki kikiwa hakieleweki hadi mtu asome vifungu vya mbele.

Je mtu aliyeidhinishwa katika ibara na kipengele hiki ni nani?

Kifungu cha 8:
Muswada huu haujaweka bayana iwapo nyaraka za siri zinaweza kuwekwa wazi katika mtandao kama zina maslahi ya nchi au wananchi mf. Matumizi mabovu ya pesa za umma

Kifungu cha 14: 
Neno pornografia halijapewa maana na hivyo jambo lolote lenye mwonekano wa kiasherati (sexually vulgar) linaweza kutafsiriwa kama pornografia na kumuingiza muhusika matatizoni.

Ponografia ya mtandao isikatazwe kabisa ila inatakiwa kuweka ulinzi thabiti wa kuhakikisha watoto hawawezi kufungua mitandao ya aina hiyo.

Ponografia zote ni chafu lakini sio chafu zote ni ponorafia. Hivyo kutokana na kuwa sheria hii inasema ponografia zote ni chafu hii itasababisha kila mtu ahukumiwe chini ya kifungu B.

Uchafu na Ponografia viwe vipengele viwili tofauti.

Kifungu cha 15:
Suala la kujifanya mtu mwingine kwenye mtandao, linaweza kuleta utata kwani kuna baadhi ya mitandao ambapo watumiaji hutumia majina ambayo sio ya kwao. Itakuwaje watu kwa madhumuni mabaya wakitafuta mtu mwenye jina kama hilo na kumshtaki mtumiaji wa mtandao?

Je, mtu kujifanya mtu mwingine inahusisha mtu kutumia jina lisilo lake hata kama hajajifanya mtu mwingine? Ni vema suala hili likafafanuliwa kisheria kwakuwa ni suala muhimu lakini wachache wataelewa manaa yake.

Kifungu cha 16: 
Ni nani ana mamlaka ya kubainisha kuwa jambo lililowekwa kwenye mtandao ni la UKWELI, UONGO au UPOTOSHAJI? Ni wazi kuwa mamlaka husika inaweza tumia hili kama mtego kwa manufaa yao.

Kipengele hiki kama vingine kimeambatanisha muda usiopungua bila kusema muda usiozidi. Hivyo mtuhumiwa anaweza kufungwa hata kifungo cha maisha kutokana na mamlaka ya mahakama.

Watu binafsi wanaweza kutumia vibaya kifungu hiki kuzuia uhuru wa maoni kwa kuwaburuza watumiaji wa mtandao mahakamani kila kukicha na kuwapotezea muda wahusika ambao wanaweza kubainika mwishoni kuwa walionewa.

Kifungu cha 20: 
Katika mawasililano ya mtandao kama ilivyo mawasiliano mengine kuna ujumbe ambao mtu hawezi kuacha kuupata

Mfano kutembea barabarani na kuona bango la matangazo, au kuwa ndani ya daladala iliyowasha redio.

Vivyo hivyo katika mtandao sio kila ujumbe anaopokea mpokeaji ameuomba na hivyo kifungu hiki kinafanya kila mtu atakayepokea ujumbe bila ridhaa yake kuwa amefanya kosa la jinai. 

Kifungu cha 21(1): 
Tafsiri za Kiswahili na kiingereza zipo tofauti kabisa.

Ya Kiswahili inamlenga Mtoa Huduma na huku ya kingereza inamlenga mtu yeyote anayetumia mtandao.

Ya Kiswahili inamlazimu mtoa huduma kumtaja mhusika aliyeweka ujumbe na pia kumuadhibu mtoa huduma huku ya kiingereza inazungumzia kuhusu tafiti kwa ujumla.

Ya kiingereza ni nzuri lakini ya Kiswahili imepotoshwa na inavunja uhuru wa mawasiliano.

MUHIMU:
Hakuna kinga yoyote kwa mtoa taarifa (source) kwa mujibu wa ibara hii.

Kifungu cha 22:
Je, nani ana mamlaka ya kuamua kuwa ujumbe kwenye mtandao unatolewa au kuboreshwa kwa kusudi au bila kusudi.

Itambulike kuwa ujumbe wa kwenye mtandao huboreshwa (edit) au kufutwa wakati wowote muhusika anapoona inafaa mf. WhatsApp status, Facebook status nk.

Kifungu cha 23: 
Unyayasaji wa kupitia mtandao (cyber bullying) haujapewa maana.

Sheria inatakiwa kuweka bayana maudhi ya kihisia ni nini.

Kwani mtu yeyote atakayeudhiwa ‘kihisia’ au kudai kuwa hisia zake zimeudhiwa anaweza kushtaki. Sio kila linalosababisha maudhi ya kihisia ni unyanyasaji

Kifungu cha 27: 
Ni nani anaamua kitendo fulani ni kula njama? Mazungumzo ya kawaida na maamuzi ya kukubalika na upande mmoja yanaweza kutafsiriwa kama kula njama na watu wa upande mwingine.

Kifungu cha 31 (3a):
Sheria ya kiingereza inasema ‘as soon as practicable’ lakini ya Kiswahili inasema wakati wa upekuzi na ukamataji wa mali. Hizi zina maana tofauti.

Ibara hii inawapa mamlaka Wakuu wa Vituo vya Polisi kufanya upekuzi na kuchukua mali(za kielektroniki) na taarifa binafsi za raia bila amri ya Mahakama.

Kifungu cha 32-35
Ibara hizi zinamlazimisha mtoa huduma kutoa data za wateja wake kwa Mkuu wa kituo cha Polisi bila kibali cha Mahakama. Wakuu wa Vituo vya Polisi wamepewa nguvu sana katika sheria hii! Mahakama ipewe mamlaka haya na si Polisi, na ifanyike hivi baada ya kujiridhisha kuwa mwananchi anatakiwa kufanyiwa upekuzi, kuchukuliwa data zake au za wateja wake n.k

Kifungu cha 39-45
Watoa huduma na wahifadhi tovuti wanalindwa na ibara hizi lakini kwa masharti.

Katika ibara ya 39, Waziri anapewa mamlaka ya kuamua kipi ni kosa na kipi si kosa. Anapewa mamlaka ya kusimamisha na kusitisha huduma, kuondoa taarifa juu ya kitendo husika (mfano kulazimisha kuondoa mijadala yote ya ufisadi flani kama yeye ataona kwa mamlaka yake kuwa haufai kujadiliwa).

Muswada huu vifungu vya 31-38 na vifungu vya 39-46 zinakinzana kwani kwa wakati mmoja mtoa huduma anaweza akawa ameona jambo ameshalitoa na anajiandaa kuitaarifu mamlaka husika huku mamlaka husika (Askari Polisi) ikiwa na uwezo wa kwenda kuchukua vifaa na data za mtoa huduma.

Mamlaka ya Polisi imepewa kinga kubwa ambayo haiingiliani na sheria yoyote ile.

0 comments:

Post a Comment