Thursday, March 17, 2016


Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Amani Mwenegoha ameingilia kati kwa kuwasuluhisha maofisa wa Takukuru na polisi waliokunjana mashati wakimgombea shahidi katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi wilayani hapa.
“Nimelazimika kuita kikao cha dharura cha kamati ya ulinzi na usalama kujadili suala hili linalotishia kuvuruga uhusiano mwema kati ya taasisi hizi mbili zinazopaswa kushirikiana,” alisema Mwenegoha.
Alisema kabla ya tukio hilo, Machi 8 mwaka huu, ofisi yake ilipokea malalamiko kutoka Takukuru kuwa baadhi ya maofisa wa polisi walivuruga upelelezi na ushahidi wa kesi ya tuhuma za rushwa inayomkabili mmoja wa walimu wa shule za msingi.

 “Baada ya kikao cha zaidi ya saa nne kuanzia saa 11 jioni hadi saa mbili usiku, pande zote zimezika tofauti na nimewapa onyo mkuu wa polisi wa wilaya na mwenzake wa Takukuru nikiwataka kuwasimamia vyema maofisa waliopo chini yao kuepusha tukio kama lile,” alisema mkuu huyo wa wilaya. 
Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho ni polisi na Takukuru kuheshimiana na kushirikiana kutekeleza majukumu yao. 
“Nimeagiza OCD na mkuu wa PCCB waitishe vikao vya haraka vya ndani kujadili suala hili na kuwekana sawa,” alisema. 
Mwenegoha alisema amewapa wakuu wa taasisi hizo muda wa siku tano kuanzia Jumanne iliyopita kukamilisha vikao vyao vya ndani na kutoa mrejesho kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama jinsi walivyoshughulikia suala hilo lililoitia aibu Serikali baada ya watumishi wake kukunjana mashati hadharani. 
Alisema kitendo cha askari polisi kumkamata na kumfunga pingu shahidi wa Takukuru, Paulo Stephano kabla ya kutoa ushahidi hakikuwa cha kiungwana wala kuheshimu mamlaka nyingine ya Serikali na kimetoa taswira kuwa jeshi hilo lililenga kudhoofisha ushahidi wa taasisi hiyo.
 “Haikubaliki polisi kumvamia shahidi wa Takukuru, kumweka chini ya ulinzi, kumfunga pingu na kumtupia kwenye gari lao hata kabla hajatoa ushahidi,” alifafanua. 
Kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kitakachopokea taarifa ya vikao vya ndani vya Takukuru na polisi namna walivyoshughu-likia suala hilo kitafanyikaMarch 18,mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment