Saturday, August 17, 2013

  Ayoub Mangi ndani ya uwanja wa nyumbani
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Elimu) ulizinduliwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo jana na kutaja mikakati 9 ifuatayo: Hebu pitia mikakati hii-kisha utoe maoni yako kama inajitosheleza.

1. Upangaji wa shule kwa ubora wa matokeo ya mtihani kitaifa kuanzia shule iliyoongoza hadi ya mwisho. Lengo la mkakati huu ni kuongeza uwajibikaji na ushiriki wa jamii katika usimamizi wa utoaji wa elimu bora....

2. Utoaji wa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri. Utaratibu wa kutoa tuzo kwa shule utatoa motisha kwa shule kuongeza bidii na kutoa matokeo bora zaidi.

3. Kuwa na kiongozi cha usimamizi wa shule. Mkakati huu utasaidia kuimarisha utendaji wa shule kwa kuwawezesha viongozi wa shule kutekeleza majukumu yao kikamilifu

4. Upimaji wa kitaifa wa stadi za kusoma, kuandika, kuhesabu. Lengo la mkakati huu ni kuhakikisha wanafunzi wanamudu stadi msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu katika madarasa ya chini ya elimu ya msingi kabla ya kujiunga na madarasa yanayofuata

5. Utoaji mafunzo kwa walimu kuhusu ufundishaji mahiri wa stadi za KKK. Lengo la mkakati huu ni kuwawezesha walimu kumudu ufundishaji wa stadi za KKK katika darasa la kwanza na la pili. Mafunzo yatatolewa kwa walimu kutoka shule 6,167 za halmashauri 40.

6. Programu ya kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi katika ufundishaji na kujifunza-Students Teachers Enrichment Program (STEP). Mkakati huu utajenga utamaduni wa kuwabaini wanafunzi wenye kuhitaji msaada katika kujifunza. Aidha, utoaji mafunzo ya walimu kwa ajili ya utekelezaji yanalenga kumpa mwalimu nyenzo na uwezo zaidi wa kufundisha na kubaini na kuzingatia maeneo yenye changamoto kwa wanafunzi.

7. Ujenzi wa miundombinu muhimu ya shule. Lengo la mkakati huu ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na upatikanaji wa vifaa muhimu shuleni.

8. Utoaji ruzuku ya uendeshaji wa shule. Utekelezaji wa mkakati huu utawezesha uboreshaji wa upatikanaji vitabu vya kiada na vifaa vya kufundishia na kujifunzia shuleni.

9. Utoaji wa motisha kwa walimu. Mkakati huu utawezesha kuwatambua walimu, kutatua changamoto zinazowakabili na kuwapa motisha za kifedha na zisizo za kifedha kwa kujali maslahi na madai yao ya kimsingi.

0 comments:

Post a Comment