Monday, April 8, 2013

Makala imewasilishwa na Iddi Allute kupitia ukurasa wa Contact, nawe pia unaweza kuwasilisha taarifa unayotaka ichapishwe hapa kwa ajili ya kusomwa na wote.
---

Miaka 20 iliyopita, mwaka 1993 Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi aliandika mfululizo wa makala katika gazeti la kila wiki la Mwananchi wakati huo. Aliziita makala zake, Tuishi bila kubaguana kidini.

Mzee Jumbe akieleza katika makala zake kuwa, aliamua kuchukua uamuzi wa kuandika makala hizo ili wananchi pamoja na viongozi waweze kuchukua hatua juu ya suala la udini ambalo lilikuwa likitishia uhai na umoja wa Taifa letu.

Aliyoyaongelea Mzee Jumbe sasa yameanza kuonekena katika jamii yetu. Tatizo la udini linazidi kukua badala ya kupungua. Wanasiasa wanaongelea udini, viongozi wa dini wanaongelea udini, wanaharakati nao pia wanaongelea uwepo wa udini. Kila mahali utakapopita siku hizi, katika mada zitakazojadiliwa, moja wapo ni mada inayohusu udini.

Kabla sijaendelea na makala yangu haya, ni vema nikanukuu beti za shairi lililotungwa na Kiongozi wetu huyo alilolipa jina la Tanzania ni ya Watanzania wote
Wito huu nautoa, kwa wote watanzania
Naona hatari yaotea, twendako yangojea
Wajibu wote kuijua, tuchange kuiondoa
Enyi watanzania jueni, Tanzania yetu sote.

Huu si usaliti, pia si uchochezi
Ni onyo tena la dhati, Nilitoalo kwa wakati
Wazeni enyi wananchi, Msije kukosa bahati.
Enyi Watanzania jueni, Tanzania yetu sote.

Umoja na amani, usawa kwa wote nchini.
Akataaye ni nani, mkorofi, adui kisirani.
Aseme wazi hadharani, ya nini chini chini
Enyi Watanzania jueni, Tanzania yetu sote.

Kweli na haki kote, uwe mwendo wa wote
Hadaa au dhuluma yoyote, iwe karaha kwa sote
Hii nchi yetu sote, tufaidike nayo wote.
Enyi Watanzania jueni, Tanzania yetu sote.

Namaliza sikudhulumu, wenyewe mhukumu,
Uhuru na umoja kudumu, bila ya usawa vigumu
Hilo wazi mfahamu, je haki au dhuluma?
Enyi watanzania jueni, Tanzania yetu sote
Watu wengi wamekuwa wakiongelea uwepo wa udini hapa nchini lakini pindi unapowauliza nini hasa maana ya udini wamekuwa wakishindwa kutoa jibu lililo sahihi. Si ajabu ukaambiwa kuwa “jamaa Fulani ni mdini kwa kuwa tu anasali sala tano na muda wote anavaa kanzu na tas’bihi mkononi haimuondoki. Au pia, fulani ni mdini kwa kuwa muda wote amevaa rozali na kuwa hana starehe yoyote zaidi ya kusikiliza kwaya na kusoma Biblia.

Wakati nafikiria kuandika makala haya, niliamua kwanza kutafuta maana ya neno udini. Kitabu cha kwanza kabisa kukikimbilia ilikuwa ni kamusi ya Kiswahili sanifu, toleo la pili ya mwaka 2004. Kwa bahati mbaya, nadhani inaweza kuwa imetokana na kusahaulika au kutokana na makosa ya mchapaji neno udini halipo katika orodha ya maneno katika kamusi hiyo.

Jitihada za pili katika kutafuta maana ya maneno haya niliipeleka katika kazi za wanazuoni mbalimbali ambapo niliamini kuwa lazima watakuwa wamezungumzia neno hilo katika kazi zao. Bahati nzuri maana ya neno udini nililipata kutoka kwa viongozi wawili wa kidini hapa Tanzania. Hawa ni Mwinjilisti Kamara Kasupa na Sheikh Mohamed Issa.

Katika pitia pitia zangu katika maandiko ya Mwinjilisti Kamara Kasupa, yeye aliutafsiri udini kuwa ni Ubaguzi unaoendeshwa katika misingi ya kidini, na aliendelea kufafanua kuwa udini una kawaida nyingine mbaya, nayo ni 
ubinafsi wa kubinafsishwa katika misingi ya kidini, una kawaida nyingine mbaya nayo ni ubinafsi wa kubinafsisha kila kitu.

Tafsiri ya pili ya dhana ya udini niliipata kwa mwanazuoni maarufu wa kiislamu Sheikh Mohamed Issa. Katika mada yake iliyoitoa katika msikiti wa Haq mkoani Morogoro, aliutafsiri udini kuwa ni kupendelea dini yako kiasi cha kuwadhulumu watu wa dini nyingine, na bila kujali taratibu. Akaelezea zaidi kuwa ni kupendelea dini yako na kuwadhibiti watu wa dini nyingine wasije wakapata mafao, mafanikio na maendeleo kama ya dini yako.

Baada ya kupata tafsiri hizo, niliamua kumfuata kiongozi wangu wa dini na kukaa nae huku tukijadili masuala mbalimbali yanayoendelea katika nchi yetu. Katika mazungumzo yetu nilimuuliza, uislamu unatutaka tuishi vipi na wasiokuwa waislamu?

Alinijibu kuwa, katika Quran Tukufu Surat AN-Nisaa aya ya 36
mwenyezi Mungu anasema “Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na
chochote. Na wafanyieni ihsani wazazi wawili, na jamaa na mayatima na masikini na jirani walio karibu na jirani walio mbali, na rafiki wa ubavuni (mwenu) na msafiri aliye haribikiwa, na wale iliyowamiliki mikono yenu ya kulia (kuume). Bila shaka Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wajivunao”.


Funzo kubwa nililolipata katika aya hii ni kuwa muislamu wa kweli hatakiwi kubagua. Anatakiwa kutenda wema kwa wote bila kujali dini, kabila au utajiri wa mtu. Migogoro ya kidini, nini hasa chanzo chake na kwa nini hasa waislamu ndo wanaonekana kama wapenda fujo na vurugu? Hili ndio hasa nataka kulijadili na pia kutoa mbinu za kuiepuka migogoro hii ili isije kuliangamiza taifa hili.

Mwalimu wangu wa chuo Kikuu, Profesa Mwesiga Baregu alipokuwa akitufundisha somo lililohusu Utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani (Peace making and conflicts resolution) alikuwa akisisitiza suala la kusikiliza, kutafakari na hatimaye kuchukua hatua stahiki katika kutatua matatizo. Na baada ya hatua kuchukuliwa ni vema kuwarudishia majibu walalamikaji na walalamikiwa.

Tatizo kubwa tulilonalo sisi ni kwamba tumekuwa wagumu sana kusikiliza malalamiko hasa yanayotolewa na waislamu, na hata ikitokea malalamiko yao yamesikilizwa basi yamekuwa yakitolewa majibu mepesi sana.

Nimekuwa nikijiuliza, kwa nini hasa malalamiko ya waislamu huwa hayapewi uzito sana, huwa nakosa jibu. Labda huwa tunawaangalia watoa malalamiko, kwa kuwa labda wengi wao wanavaa kanzu zilizo chakaa na makubadhi au hata yeboyebo zilizo chakaa, hivyo tunadhani hata akili zao zimechakaa kama kanzu na yeboyebo wanazovaa.

Hili ni tatizo, maana siku hizi mtu mwenye akili anapimwa kwa vitu alivyovaa au anavyomiliki au usafiri anaotumia na hata wapi anaishi. Anayetumia VX huonekana ana akili sana kuliko anayeendesha baiskeli au mtembea kwa miguu. Anayeishi Masaki au Mikocheni na Oysterbay jijini Dar es salaam au Uzunguni, Area C na Area D mkoani Dodoma huonekana kuwa ana akili sana na amestaarabika kuliko mtu anayeishi Mbagala, Manzese hapo hapo Dar au pia anayeishi Chang’ombe mjini Dodoma.

Tumejenga tabia ya kuthamini hata mavazi na lugha. Anayevaa suti na kuongea kiingereza huonekana ana akili sana na amestaarabika kuliko anayevaa kaniki na kuongea Kiswahili.

Kuna suala moja ambalo mimi binafsi limekuwa likinikera sana na ninahisi kwa kila mpenda amani na usawa huwa anakereka. Suala hili ni kuwaita viongozi wa dini kuwa ni wahuni. Hili ni tusi kubwa hasa unapomuita kiongozi wa dini ambaye anaongoza mioyo na imani za watu. Tumeshuhudia watu kama akina Sheikh Ponda, Sheikh Farid na wengine wengi wakiitwa majina ambayo yanaonesha dharau kubwa si kwao pekee bali pia kwa dini yao na taasisi wanazoziongoza.

Lakini sababu ya pili inayowafanya waislamu waonekane kama wapenda fujo na wapenda machafuko kwamba wamekuwa katika harakati za kuitetea dini yao ambayo wanadhani kuwa imekuwa ikdharauliwa na pengine kutothaminiwa kabisa.

Hili nitalielezea. Kwa sasa kumekuwa na wanaharakati wengi na wanasiasa ambao wamekuwa katika harakati za kuhamasisha na kufanya mabadiliko mbalimbali katika mifumo yetu hasa sheria, mabadiliko ambayo kwa njia moja ama nyingine yataathiri imani na ibada za waislamu.

Mathalani, unapoanzisha vuguvugu la kuwepo kwa sheria moja ya mirathi, kitu ambacho kitaleta upinzani mkubwa kutoka katika jamii za waislamu kwa kuwa tayari wana mfumo wao wa mirathi, ambao umeelekeza namna gani mirathi igawanywe na nani apate nini na kwa nini apate hivyo.

Udini umekuwepo siku nyingi sana hapa nchini kwa sura tofauti. Vichwani mwa watu wamekuwa na dhana za ubaguzi wa kidini bila wenyewe kujijiua. Watu wanaoamini katika dini ya kiislamu wamekuwa wakidharauliwa na kukejeliwa sana. Mfano, ukitazama vyombo vya habari hasa magazeti. Mfano, ili kufikisha ujumbe kwa wasomaji, wachora wa picha za magazetini huwatumia sana wazee wenye muonekano wa kiislamu katika kuonesha watu wasiostaarabika.

Utakuta unapotaka kumchora mchawi, mganga wa kienyeji ama mtu anayependa sana kula katika sherehe au misiba, atamchora mzee aliyevaa kanzu, makubadhi, amevaa baraghashia na ameshika bakora vitu ambavyo hutumiwa sana na waislamu ingawa pia katika baadhi ya jamii kama za wahaya mavazi hayo ni mavazi ya heshima kwa wazee bila kujali dini.

Utendaji wa baadhi ya taasisi nao umekuwa ukiibua hisia za kidini. Hii ilidhihirika miaka michache iliyopita wakati hakimu mmoja jijini Dar es salaam ilipoamua kumfunga kifungo cha miezi sita, muislam mmoja aliyehudhuria mahakamani kwa kuwa tu alikataa kuvua kofia aina ya baraghashia. Aliadhibiwa kwa kosa la kudharau mahakama.

Pia upo ubaguzi katika makazi na maeneo. Maeneo mengi ambayo kiasili yamekuwa yakikaliwa na waislamu yamekuwa yakipewa majina yasiyo na nidhamu kama vile uswahilini, uswazi nakadhalika na yamekuwa yakisifika sana kwa sifa ya uchawi, kitu ambacho kimejengwa ndani ya vichwa vya watu na hutokea mpaka wageni kuogopa kuishi ama kuwekeza katika maeneo hayo na hivyo kuyafanya yaendelee kuwa duni siku hadi siku.

Kwa mtu yeyote, ukimueleza maeneo kama Ujiji na Gungu mkoani Kigoma, Isevya mkoani Tabora, Bagamoyo , Rufiji na Tanga, taswira inayojengeka kichwani mwake moja kwa moja ni kuwa, hii ni miji iliyojaaa wachawi na washirikina. Na hii imejengeka kiasi kwamba, iwapo inatokea mtu amekosewa na mwenzake, tishio huwa ni kwamba, nitakuendea Ujiji kama siyo Bagamoyo, Rufiji na Kilwa.

Si rahisi kukuta mfanyakazi wa serikali aliyepangwa kufanya kazi mkoani Kigoma, kukubali kuishi Ujiji au Gungu hata kama ataambiwa bei ya pango kwa nyumba nzima ni Tsh 50,000 kwa mwezi. Mtumishi huyo yupo radhi kuishi Mjimwema ambako atalipa Tsh 200,000 kwa mwezi na ukimuuliza kwa nini hasa hataki kuishi Ujiji ama Gungu, atakueleza kuwa anaogopa kurogwa. Huu pia ni ubaguzi.

Profesa Mahmood Mamdani ametunga kitabu chake alichokipa jina la Good Muslim, Bad Muslim. Katika kitabu hicho anaelezea jinsi waislamu walivyogawanywa katika makundi. Kwa hapa Tanzania Good Muslim ni wale waislamu walio chini ya BAKWATA, ambao wanaiona BAKWATA kama mtetezi na mlinzi wa waislamu na Bad Muslim ni wale wote ambao hawataki msimamo wa BAKWATA na pia hawataki kuitambua BAKWATA, ambao wanaiona BAKWATA kama mnyonyaji na mkandamizaji wa haki za waislamu. Bad Muslims hawasikilizwi na muda wote wamekuwa wakiitwa walalamishi.

Lakini sasa kuna hili suala la kamatakamata ambalo limekuwa likiendeshwa na jeshi la polisi katika kudhibiti viongozi wa dini ambao wanahubiri “uchochezi”. Jambo hili lisipofanywa kwa umakini, linaweza kuingilia uhuru wa watu wa kuabudu. Majuzi nilikuwa natazama kipindi fulani katika TV. Mwanaharakati mmoja kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) alilalamikia matumizi ya maneno kama vile “kafir” na kuelezea kuwa si vizuri kuyatumia.

Tukumbuke kuwa neno hilo lipo katika kitabu kitukufu cha waislamu, , Quran na kulalamikia kutumika kwa neno hilo ni sawa na kusema liondolewe au lisitumike, kitu ambacho nina uhakika kuwa hakitawezekana kwani kwa mujibu wa mafundisho ya uislamu, dini yao ilikwisha kamilika na hakuna marekebisho yoyote ambayo yanaweza kufanyika.

Lakini pia, niwashukuru viongozi wetu wa dini, kama alivyosema Sheikh Alhad Mussa Salum, Sheikh mkuu wa BAKWATA wa Mkoa wa Dar es Salaam na Muadhama Askofu Kardinali PolycaRp Pengo, kuwa kuna haja ya kukutana kwa viongozi wa dini ili wajadili kwa kina, chanzo hasa cha migogoro na namna ya kuitatua. Na vikao hivyo ni vema vikianzia katika ngazi za vitongoji mpaka ngazi ya taifa.

Nimalizie makala yangu haya, kwa kuwaomba viongozi wetu na watendaji wa serikali kutopuuzia malalamiko ya watu wao. Wayafanyie kazi bila kujali, nani ameyaleta na huyo aliyeyaleta ana miliki nini au ana elimu gani. Na pia nikumbushe maneno ya rais wa zamani wa Iran Mohammed Khatami aliyeelezea majadiliano baina ya tamaduni (Dialogue among Civilizations) kama njia ya kuelewana na kuzuia machafuko yanayojiegemeza katika tamaduni.

0 comments:

Post a Comment