Tuesday, January 29, 2013

Kamanda wa Polisi Mkoa  wa Mtwara, Maria Mzuki amesema Polisi inawashikilia watu 44 wilayani Masasi kwa tuhuma za kujihusisha na vurugu zilizosababisha uhalibifu mkubwa mali za umma na watu binafsi ikiwamo Wabunge.

WABUNGE waliochomewa nyumba na mali zao katika vurugu zilizotokea Mtwara juzi; Anna Abdallah na Mariam Kasembe, jana waliangulia vilio walipotakiwa na gazeti la MWANANCHI kuzungumzia tukio hilo.

Nyumba za wabunge hao wa Viti Maalumu na mali zingine kadhaa za taasisi mbalimbali, ni miongoni mwa vitu vilivyoharibiwa katika vurugu hizo ambazo pia zilisababisha vifo vya watu wanne wilayani

Akizungumza kwa huzuni,  Anna alisema hajui sababu za uharibifu huo, hasa ikizingatiwa mwenyewe amekuwa huko kwa karibu siku tatu na hakuona dalili za uhasama wowote dhidi yake.

Anna ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho alivyotakiwa aeleze ilivyokuwa alisema kundi la vijana lilivamia nyumbani kwake saa 4:00 asubuhi:
Nina siku ya tatu hapa Masasi na nimeshiriki mkutano wa halmashauri kwa mwaliko na wakati wote, sikuhisi chochote hivyo siwezi kujua sababu ya chuki iliyofanya nyumba yangu ichomwe moto.

Wavamizi hao walipora kila kitu nyumbani kwangu yakiwamo mapazia, kabla ya kumwaga petroli kila chumba na kuwasha moto.

Kila kitu kiliteketea. Inatia uchungu kwani nyumba hiyo niliijenga kwa kudunduliza fedha kidogo kidogo nikiwa mkuu wa mkoa.

Hali si nzuri. Kila kitu kimeibwa na nyumba imechomwa moto, hakuna kilichobaki. Walichukua kila kitu na itanichukua muda mwingi kujua thamani halisi ya hasara iliyopatikana.
Naye Kasembe alipokea simu ya mwandishi wa habari hii kwa kilio na kuikata huku akisema:
Jamani niacheni… Mwenzenu naumia…!
Alipopigiwa tena baadaye, alisema anashangazwa na tukio hilo ambalo limemfika bila kutarajia na kumtia hasara kubwa. Akasema wakati wa vurugu hizo, ndugu zake akiwamo mama yake, walikimbia na kwenda kujihifadhi hotelini, lakini mpaka sasa hawajui wataishi vipi baada ya nyumba hiyo kuteketezwa kwa moto.
Wamepora kila kitu katika nyumba na kuichoma moto, sijui atakuwa nani huyu, kwani sina tatizo na wapiga kura wangu na sina mgogoro na mtu yeyote. Nashindwa hata kuhisi nani kafanya uchochezi.

Jana wanafamilia walilala hotelini na leo tupo nje ya gofu la nyumba yangu ambayo imeteketea kabisa kwa moto, tunasubiri majaaliwa mengine, lakini nimechanganyikiwa kwa kweli na sijui ni kitu gani hiki, siamini...

0 comments:

Post a Comment