Monday, December 10, 2012

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ametaja orodha ya watu waliohusika na uzembe katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akitaja mikataba hiyo katika awamu ya kwanza na watu waliohusika, Mnyika moja kwa moja alianza kwa kumtaja William Mhando kuwa alihusika na mikataba iliyozihusu Kampuni za M/S Santa Clara Supplies Company Limited pamoja na Kampuni ya M/S McDonald Live Line Techonology Limited. Wahusika wengine wa ufisadi huo ndani ya TANESCO, kuwa ni pamoja na Ofisa Ugavi wa shirika hilo, Haruni Mitambo, Mkurugenzi wa Fedha, Lusekelo Kisanga na kwamba wote walihusika na kuruhusu na kuidhinisha malipo kwa kampuni tajwa.  Wengine ni aliyewahi kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Robert ShemhiluFrance Mchalange, Naftari Kisiga, Sophia Msidai, Declain Mhaiki, Fatuma Chungo, Athanas Nangai, Elangwa Mgeni na wengine aliowataja kwa kifupi kwa majina ya S. Nkondola na N. Ntimba.

Akizungumza na gazeti la MTANZANIA, Mkurugenzi wa Kampuni ya MacDonald, Donald Mwakamele, alikana kuhusika na kuingia makubaliano na Mhando kwa ajili ya kazi yoyote ya shirika hilo na kuongeza kuwa, makubaliano aliyokuwa nao na Mhando ni kwa ajili ya kumsaidia kutafuta kazi nje ya nchi.

Alisema kitendo cha yeye kuhusishwa na Tanesco kinatokana na chuki binafsi kwake na Mhando zilizopo miongoni mwa baadhi ya watendaji wa shirika hilo (majina tunayo). Aidha alisema, kwa mtu yeyote mwenye ushahidi wa makubaliano aliyoingia na Mhando akiwemo Mnyika ajitokeze na yupo tayari kumlipa kiasi cha Sh milioni 20.

(via gazeti la MTANZANIA)


ORODHA YA UFISADI NA UZEMBE TANESCO AWAMU YA KWANZA NA MWITO WA KUTOA MAONI KUHUSU KUSUDIO LA KUPANDISHA BEI YA UMEME KWA MARA NYINGINE

Picture
Shirika la Umeme (TANESCO) linakabiliwa na ufisadi na uzembe unaoongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa upande mmoja na uendeshaji wa shirika kwa upande mwingine.  Ufisadi na uzembe huo unapunguza uwezo wa TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na unaongeza gharama na bei ya upatikanaji wa umeme hali inayoathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa kuchangia katika mfumuko wa bei na ongezeko la gharama za maisha. Mzigo wa ufisadi na uzembe katika TANESCO unajitokeza zaidi katika mikataba mibovu pamoja na ukiukwaji wa sheria za ununuzi wa umma, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 sehemu ya pili ya bunge (inayoundwa na wabunge) ndio chombo kikuu chenye madaraka na mamlaka kwa niaba ya wananchi ya kuisimamia serikali. Hata hivyo, katika kipindi cha kati mwaka 2008 mpaka 2012 maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo kuhusu umeme yamekuwa hayatekelezwi kwa wakati na kwa ukamilifu hali inayofanya tuhuma za ufisadi na uzembe kuendelea kujirudiarudia. Katika muktadha huo, ni muhimu kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi ibara ya 8 madaraka na mamlaka ni ya umma (serikali inafanya kazi kwa niaba tu) ipo haja ya kuanza kuunganisha ‘nguvu ya umma’ katika kushinikiza hatua kuchukuliwa kwa wahusika wa ufisadi na uzembe ili kuweka misingi bora ya uwajibikaji katika sekta ya nishati.

Ili umma uweze kuungana kuchukua hatua ni muhimu masuala yote ya ufisadi na uzembe yakaelezwa kwa uwazi kwa umma hivyo, katika mfululizo huu nitaweka hadharani orodha za watuhumiwa wa ufisadi na uzembe katika sekta ya nishati. Orodha hizi zinatolewa kwa awamu zikigusa kwa kuanzia mashirika na taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati na Madini na baadaye Wizara yenyewe na hatimaye Serikali kwa ujumla. Aidha, orodha hizi zitatolewa kwa awamu masuala kwa masuala na matukio kwa matukio, ngazi kwa ngazi.

Katika orodha ya awamu ya kwanza nitaanza na TANESCO kuhusu masuala na matukio yaliyohusu kampuni ya M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED pamoja na kampuni ya M/S McDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED. Orodha nyingine zitafuata katika awamu ya baadaye iwapo vyombo na mamlaka husika hazitachukua hatua ikiwemo juu ya tuhuma za ufisadi na uzembe katika matumizi ya dola milioni 54 (zaidi ya bilioni 86) katika ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.

Nimetoa majina haya hadharani ili umma uunganishe nguvu kwa njia mbalimbali kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya ufisadi na uzembe ili kuhakikisha nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria na maadili katika utumishi wa umma.

Mamlaka zinazopaswa kuchukua hatua ni pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sekretariati ya Maadili ya Umma zote kila moja kwa nafasi yake zichunguze ukiukwaji wa sheria katika masuala yaliyo kwenye majukumu yao na kuchukua hatua za ziada kwa kuzingatia pia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo nimeitumia kama rejea kwenye baadhi ya masuala katika orodha hii.

Aidha, kwa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeitisha Mkutano wa Taftishi Juu ya Marekebisho ya Bei ya Umeme za TANESCO ambao inakusudiwa bei ya umeme kupandishwa tena, ni muhimu masuala ya ufisadi na uzembe ndani ya TANESCO yakajadiliwa kwa upana na umma, ili kupinga gharama zinazotokana na hali hiyo zisiingizwe katika mahesabu ya kukokotoa bei.

Ikumbukwe kwamba tarehe 9 Novemba 2011 EWURA ilipokea Ombi la Dharura toka TANESCO na kupandisha bei kwa wastani wa asilimia 155 kuanzia tarehe 1 Januari 2012 na niliunganisha umma kupinga na hatimaye EWURA ikapunguza asilimia hiyo na kuruhusu nyongeza ya wastani wa asilimia 40.29 ambayo ndiyo inayotumika hivi sasa.

Hivyo, nitumie nafasi hii kuhimiza pia umma kujitokeza tarehe 10 Disemba 2012 kuanzia saa 4 asubuhi katika Ukumbi wa Karimjee Dar es salaam kwenda kutoa maoni kwa kuzingatia Taarifa ya Gharama za Huduma ya Umeme (Cost of Service Study) na zaidi kwa kupinga kuingizwa kwenye bei ya umeme gharama za uzembe na ufisadi ili kupunguza athari katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi miaka 51 baada ya Uhuru.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,


John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
09/12/2012
-------------------------------------------
(via)

ORODHA YA AWAMU YA KWANZA: JUU YA MASUALA NA MATUKIO YA UFISADI NA UZEMBE YALIYOHUSU MIKATABA YA MAKAMPUNI YA M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED NA M/S McDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED.


Masuala na matukio ya ufisadi na uzembe yaliyohusu mikataba ya makampuni ya M/s Santa Clara Supplies Company Ltd na M/s McDonald Live Line Technology Limited ambayo yamefanyika kinyume na sheria mbalimbali.

Kwa ushahidi wa nyaraka baadhi ya sheria zilizokiukwa ni pamoja na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 na sheria nyinginezo. Aidha, masuala na matukio ya ufisadi na uzembe katika mikataba hiyo yamefanyika kinyume na kanuni, miongozo na maadili ya Shirika la Umeme (TANESCO).

Ufisadi na uzembe umesababishwa na makosa mengine mbalimbali mathalani mgongano wa kimaslahi, utovu wa uaminifu, matumizi mabaya ya ofisi na makosa mengine yaliyo kinyume cha sheria na maadili ya viongozi na watumishi wa umma.

Orodha ya wanaotuhumiwa kuhusika katika ufisadi na/ama uzembe huo 18 ni kama ifuatavyo:

1.   Mhandisi WILLIAM GEOFREY MHANDO

Huyu alikuwa ni mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na ndiye mtuhumiwa mkuu wa ufisadi unaohusu mikataba tajwa.

Akiwa mkurugenzi mkuu wa TANESCO aliingia mkataba na kampuni ya SANTA CLARA kwa tenda No PA/001/11/HQ/G/011 kuleta vifaa vya ofisini, kwa kipindi hicho kampuni hiyo tajwa hapo juu ilikuwa inamilikiwa na wanahisa ambao ni familia ya Mhando mwenyewe.

Mkataba huo ulisainiwa na mkewe kama mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo ya CLARA, kitendo hicho cha mkurugenzi kuipatia kampuni ya mkewe tenda ni kinyume na maadili ya Tanesco kifungu cha 2.2, ni kinyume na Sheria ya Ununuzi ya umma kifungu cha 33, 73(3) na 73 (5) pamoja na sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 6 (d), (e) kutokana na kuwa na mgongano wa maslahi na utovu wa uaminifu.

Aidha kusaini kwa mkataba huo yeye akiwa mkurugenzi wa TANESCO ni matumizi mabaya ya ofisi, kwa kutumia ofisi ya umma kujinufaisha yeye pamoja na familia yake na kushindwa kusimamia sheria zinazoongoza na kusimamia ununuzi wa umma.

Kwa upande mwingine, aliingia katika makubaliano na Donald George Mwakamele (mkurugenzi na mwanahisa katika kampuni ya McDONALD)  makubaliano ambayo hayaruhusiwi na yenye mgogoro ( Conflicting Joint Venture Agrement) kinyume na maadili ya TANESCO na sheria nyingine za nchi nilizozitaja awali.

Lakini pia akijifanya ni mfanya biashara alisaini na makubaliano na kampuni hiyo makubaliano ya pande mbili ya kutafuta tenda, kununua, kujenga, kufanya matengenezo na kufanya miradi yote inayohusika na umeme. Katika kuwezesha hilo Mhando alikuwa na jukumu la kutafuta miradi ya umeme na endapo ikikamilika pande hizi mbili zinagawana mapato na faida inayotokana na miradi hiyo wakati huo huo yeye akiwa mtumishi wa TANESCO.

Pamoja na kufukuzwa kazi, umma unapaswa kuunganisha nguvu kutaka Mhando achunguzwe kwa makosa ya kijinai kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomhusu na kufunguliwa mashtaka ya kukiuka sheria za nchi.

2.   Bw. HARUN MATTAMBO

Huyu ni Afisa ugavi wa shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) amefanya uzembe kwa kushindwa kuhakikisha manunuzi yote yanayofanywa na shirika yanazingatia  taratibu na kutimiza sheria za manunuzi ya umma.

Aliruhusu kufanyika kwa ufisadi na ukiukwaji wa sheria katika kupatikana kwa zabuni na. PA/001/11/HQ/G/011 na kuathiri Shirika la Umeme (TANESCO).

Alipendekeza kampuni ya M/s Mc Donald ipewe mkataba pamoja na kuwa haikuwa imetimiza masharti ikiwemo kukwepa kuwasilisha mahesabu ya fedha yaliyokaguliwa ya mwaka 2009 kama sheria ilivyohitaji.

Matokeo ya uzembe wake wa kuruhusu ufisadi ni kulisababishia hasara Shirika la Umeme (TANESCO) kwa kuwa kampuni hiyo ya Mc Donald ilipatikana bila kushindanishwa na makampuni mengine yaliyokuwa na unafuu na yaliyotimiza masharti.

Umma uungane kutaka Matambo afukuzwe kazi mara moja, na kuchunguzwa kuhusu tuhuma za kufanya uzembe huo kwa lengo la kujinufaisha na kunufaisha washirika wake kwa ajili ya hatua za ziada za kisheria.
    
3.    Bw ROBERT SHEMHILU

Huyu aliwahi kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa TANESCO na anatuhumiwa kufanya uzembe ulioruhusu ufisadi.

Alifanya makosa ya kuruhusu malipo yaliyofanyika tarehe 5 Septemba 2011 kabla hata ya kusainiwa kwa mkataba na kuruhusu kuletwa kwa vifaa kabla hata ya kusainiwa kwa mkataba katika ya TANESCO na kampuni iliyopewa kinyemela zabuni ya kuleta vifaa.

Alifanya pia makosa ya kuilipa kampuni ya Mc Donald malipo ya juu ya asilimia 30 ya thamani ya mkataba wakati vifungu vya 26 na 54.1 vya mkataba huo (pamoja na kuingiwa kinyemela) vilielekeza malipo ya asilimia 15 tu.

Shemhilu pamoja na kusimamishwa  umma uunganishe nguvu kutaka, afukuzwe kazi mara moja na kuchunguzwa kwa ajili ya hatua za ziada.
     
4.   FRANCE MCHALANGE, NAFTARI KISIGA NA SOPHIA MSIDAI

Hawa walifanya uzembe wa kushindwa kusimamia Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na maadili kwa kupendekeza kwamba Kampuni ya SANTA CLARA ipewe zabuni ya kuuzia vifaa TANESCO pamoja na kufahamu kuwa kampuni tajwa ilikuwa haijatimiza masharti na kulikuwa na mgongano wa maslahi.

Umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka sheria ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma kuwajibika kutoa mapendekezo kwa kuzingatia sheria na maslahi ya umma.

5.   Mhandisi DECLAIN MHAIKI na Bw SUKE

Akiwa mtumishi wa umma alizembea na kukwepa kutoa taarifa  kuhusu kukiukwa kwa vigezo na masharti kuhusu zabuni na. PA/001/09/HQ/W/014 na kufanya kampuni ya McDonald Live Line Technology ipatiwe zabuni kinyume cha sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2004.

Aidha alichangia kufanya kampuni hiyo kupewa zabuni pamoja na kuwa haikuwa na uwezo wa kifedha na kuiwezesha kupewa malipo ya asilimia ya ziada kinyume na mkataba. Huyu naye umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka sheria na mkataba.

6.   Mhandisi D. MHAIKI, S.NKONDOLA, N.NTIMBA.Mhandisi CHEGERE, MAKIA NA MWITA.

Wote kama timu walifanya maamuzi yaliyosababisha kutolewa kwa mkataba na. PA/001/HQ/W/14 wa tarehe 11 Machi 2010 kwa kampuni ya Ms. Donald Live Line Technology bila kuzingatia uwezo wa kitaalamu, kifedha na masharti mengine na hivyo kukiuka sheria ya ununuzi ya umma na kushindwa kulinda maslahi ya taifa.

Hawa wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinadhamu ili kudhibiti maamuzi na mapendekezo ya wataalamu katika utumishi wa umma kuingiza mashirika ya umma na nchi katika mikataba mibovu ili kupanua wigo wa uwajibikaji.

7.   FATUMA CHUNGU, ATHANASIUS NANGALI, ELANGWA MGENI

Kundi hili limehusika katika majadiliano na kutoa mapendekezo yaliyowezesha kampuni ya McDonald kupewa mkataba kinyemela.

Iwapo kundi hili lisingefanya uzembe na kusababisha ukiukwaji wa sheria mchakato wa mkataba huo kati ya mwezi Machi mpaka Mei 2009 ungewezesha TANESCO kuingia mkataba na kampuni yenye uwezo na iliyotimiza masharti na kuepusha shirika hilo kupata hasara na kubeba gharama ambazo zingeweza kuepukika.

Ni muhimu wakachukuliwa hatua za kinadhamu ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa umakini na ueledi ili kuepusha TANESCO kuendelea kufanya majadiliano na kuingia mikataba mingine mibovu yenye kuongeza mzigo wa gharama kwa shirika na hatimaye ongezo la bei kwa wananchi.

8.   LUSEKELO KASSANGA (MKURUGENZI WA FEDHA)

Huyu alibariki ufisadi wa malipo yenye mkanganyiko katika TANESCO kwa kuilipa kampuni ya Santa Clara mapema kabla hata haijafanyiwa tathmini na kupatiwa zabuni.

Malipo yalifanyika kinyemela tarehe 5 Septemba 2011 wakati ambapo tathmini ya zabuni ilifanyika tarehe 23 Septemba 2011, maana yake ni kwamba malipo yalifanywa kabla hata kampuni husika haijapewa kazi kwa mleta vifaa asiye na uwezo na mwenye mgongano wa kimaslahi.

Kassanga anapaswa kufukuzwa kazi na kuchunguzwa kuhusu tuhuma za ziada za kunufaika kutokana na baadhi ya malipo yaliyofanywa kwa makampuni mbalimbali wakati akiwa mkurugenzi wa fedha ili aweze kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.

0 comments:

Post a Comment