Monday, December 31, 2012

Akizungumzia mgogoro ndani ya chama hicho wilayani Karatu, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe aliyegeuka kuwa mpatanishi wa miamba ya kisiasa wilayani Karatu alisema mgogoro huo umewasikitisha wananchi wa wilayani hapo.

Miamba ya siasa iliyokuwa kwenye mgogoro huo ni Mbunge wa Karatu Israel Natse, Mbunge wa Viti Maalum Secilia Pareso, Mwenyekiti wa Halmashauri Lazaro Maasai na Jubileth Mnyenye, ambao walikumbatiana kama ishara ya kumaliza tofauti zao.

Katika mkutano huo Mbowe aliwaambia miamba hiyo kwamba, kitendo chao cha kutofautiana ndani ya chama kimesababisha wananchi kuendelea kuumia na kukosa imani na chama hicho.

“Leo nimekuja kuzungumzia mustakabali wa kisiasa wa Karatu, ninajua mnahofu sana kuhusu mustakabali wa chama chenu. Naomba niseme leo kwamba, chama ninachokiongoza ni chama cha watu chenye kufanya kazi za watu. CHADEMA si mali ya Dkt. Slaa, Mbowe wala mtu yeyote hiki ni mali ya Watanzania wenye uchungu na nchi yao. CHADEMA ni chama chenye kujenga matumaini kwa wananchi,” alisema Mbowe na kuongeza: “CHADEMA hatujengi chama cha kujenga wafalme ndani ya chama, hakuna kiongozi aliyepo juu ya chama, katiba ya chama ndio chombo kinachotuongoza makabila yote ndani ya chama.”

Akizungumzia uamuzi uliofanywa na Kamati Kuu jijini Dar es Salaam ya kuwasimamisha uongozi kwa muda viongozi wa Karatu, ili kupisha uchunguzi, Mbowe alisema baada ya kukaa na kuzungumza nao sasa ameridhika na kuwarejesha kazini viongozi wote.

Alisema kwa muda mrefu sasa chama hicho kimekuwa kikipigania mambo muhimu na ya msingi kwa wananchi hata hivyo katika utekelezaji huo bado wanaamini kwamba, ndani ya CHADEMA pia hakuna malaika wote ni binadamu.

“Kihistoria Karatu ni ngome ya CHADEMA, naomba niwaambie viongozi hampo juu ya chama, inapotokea mmekiumiza chama basi lazima tule sahani moja na nyinyi. Kamati Kuu kule Dar es Salaam tulifanya maamuzi magumu kwamba, hawa wanaume wanaomenyana hapa Karatu hatuwezi kuwavumilia waendelee kukiumiza chama.

“Kiongozi yeyote anayetoka nje ya mstari tuna mchinjia baharini. Naomba viongozi wangu muelewe hivyo ndani ya Chama hakuna aliyepo juu. Hawa tungewachinjia baharini, lakini kwa vile wameifanyia CHADEMA mambo mengi ndani ya Karatu na Arusha, hatuwezi kuwachinjia baharini lazima tuthamini mchango wao. Tumekaa siku tatu tunazungumza na hawa wanaume kwa kina. Napenda kuwatangazia wananchi wenzangu wa Karatu hawa Tembo waliokuwa wakipigana hapa wamewaumiza mpaka Punda milia na Nyati hapa Karatu. Wanachama, kamati mbalimbali na madiwani hapa waligawanyika pande mbili ndani ya chama. CHADEMA tunaposigana tunampa nafasi adui CCM,” alisema Mbowe.

Akiwarushia makombora viongozi hao, Mbowe aliwaambia kwamba kuchaguliwa kwao kuwa viongozi hakumaanishi kwamba Karatu nzima haikuwa na viongozi wanaofaa kuongoza kwa nafasi walizonazo.

“Ndugu wananchi, nimekaa kwa siku tatu hapa Karatu kuzungumzia tofauti hizi, sasa naomba niwaambie kwamba, tumeyamaliza na miamba hii ya kisiasa imekubaliana kufanya kazi pamoja. Sasa naomba niwasimamishe hapa wote ili wawaombe msamaha nyinyi wananchi, kwani waliwakosea sana. Juzi na jana tumekesha hapa kwa ajili ya kuhakikisha tunamaliza tofauti hizi. Sasa kwa mamlaka niliyopewa na Kamati Kuu naomba niwatangazie wananchi kwamba, naurejesha uongozi huu madarakani kama walivyokuwa awali,” alisema.

Hata hivyo kabla ya kuwasimamisha viongozi hao Mbowe aliwataka watambue kwamba nafasi yao ya kuwa kwenye ofisi za umma, ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kujitumikia wao na maisha yao, “Hawa jamaa wametusumbua sana, hata kama watakuwa na hoja za kweli. Nataka leo wazungumze mbele yenu ujinga wa migogoro basi tena Karatu,” alisema Mbowe.

Akianza kuzungumza mbele ya wananchi hao Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Lazaro Maasai aliwaeleza wananchi wa Karatu kwamba, ana msamehe Mnyenye Saba mara Sabini, “Kwa yale yote niliyomkosea namsamehe Saba mara Sabini. Lakini pia kwa wananchi wa Karatu nawaomba mnisamehe kwa kuwakosea na kuwaumiza,” alisema Maasai.

Kwa upande wake Mnyenye aliwaambia wananchi kwamba, hakuna tena uhasama ndani ya Chama hicho Karatu kwani sasa ametambua tofauti kidogo zimeleta madhara kwa wananchi wanaokipenda chama hicho.

“Nimewakwaza sana wananchi wa Karatu na viongozi wangu wa Chama pengine kwa kutojua au kufuatana taratibu za Chama. Hakuna tena uhasama kati yangu na Lazaro. Ninawaomba mkiona ninakwenda tofauti msingoje mpaka Mbowe atoke Dar es Salaam, nipo tayari kujishusha au kuondoka kwenye uongozi,” alisema Mnyenye.

Katika hatua nyingine Mbowe alitumia fursa hiyo pia kuwapatanisha katibu wa wilaya ya Karatu na Mwenyekiti wa wilaya ambao nao walikuwa hawaelewani kiutendaji. Kana kwamba hiyo haikuwa imetosha Mbowe aliwageukia tena Mbunge Natse na Pareso, ambao nao walipandishwa jukwaani kwa ajili ya kuwaomba msamaha wananchi kutokana na tofauti zao, “Nikiri mbele yenu hapa kwamba, nitamsaidia Mbunge Natse kwanza huyu ni sawa na baba yangu, mchungaji wangu,” alisema Mbunge Pareso.

Kwa upande wake, Mchungaji Natse aliwaomba msamaha wananchi waliokuwa wamefurika kwenye viwanja hivyo, kwa kuwaambia kwamba siku zote hupata tabu ya kusimama mbele ya wananchi hao kutokana na kura nyingi walizompatia.

Katika hatua nyingine uwanjani hapo, Mbowe aliongoza harambee ya ujenzi wa ofisi mpya za wilaya za chama hicho kwa kukusanya michango mbalimbali kutoka kwa wananchi pamoja na viongozi wa chama na wabunge.

Mbowe alisema kwamba, amesikitishwa na kitendo cha wilaya hiyo kuendelea kupangisha ofisi wakati ndio wilaya yenye mabadiliko makubwa ya mageuzi ndani ya nchi, “Nimewaambia hawa viongozi waliokuwa kwenye tofauti zao, wao ndio watakuwa wasimamizi wakubwa wa mradi huu na kwa kuanzia mimi nachangia Sh Milioni 10, Dkt. Slaa Sh Milioni 5, Nassari ametoa Sh Milioni 2,” alisema Mbowe.

Mara baada ya kumaliza kuzungumza Mbowe, viongozi waliokuwa katika mgogoro walianza kupitisha bakuli kwa wananchi kwa ajili ya kukusanya fedha hizo ili fedha hizo ziweze kuingizwa katika ujenzi.


---
Taarifa via gazeti la MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment