Monday, December 31, 2012

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Singida, kimetoa ufafanuzi kuhusu sababu zilizomfanya aliyekuwa Diwani wa Iseke, Amosi Mughenyi, kujiuzulu.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na chama hicho katika viwanja vya Stendi ya Zamani, Singida Mjini, Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Singida, Shaban Lyimu, alisema Mughenyi alijiuzulu mwenyewe kwa kushawishiwa na viongozi wa CCM, pia kwa kushiriki kufanya kazi za kifisadi kwa kuchangisha wananchi michango haramu kinyume na sera za CHADEMA.
“CHADEMA haitakuwa tayari kuona mtu anafanya kazi za kifisadi na kuwahadaa wananchi kwa michango isiyo na halali kwa lengo la kujipatia kipato kama ilivyo kwa serikali ya CCM ilhali maendeleo ya kata huendeshwa kwa kodi na sio michango.
“Afadhali kujiuzulu kwa diwani huyo kuliko kuwapa shida wananchi ambao CHADEMA inapigania kuwakomboa,” alisema.
Wiki hii, diwani huyo alikaririwa akitoa tamko la kujiuzulu mbele ya waandishi wa habari mkoani Singida na akisema kuwa amefikia hatua hiyo kwa ridhaa yake mwenyewe.
Naye Mwenyekiti wa BAVICHA wa wilaya hiyo, Ibrahim Kalem, alimtaka mkurugenzi kuhakikisha hali ya usafi na kuweka mji safi, kwani kwa sasa mji huo umezidi kuwa na stendi nyingi zisizo na mpangilio maalumu.
“Mkurugenzi akomeshe uegeshaji wa magari katika stendi bubu iliyoko jengo la CCM, kwani iko kinyume cha utaratibu; jengo la utamaduni liwe wazi kwa shughuli za kitamaduni na mchakato wa malipo ya wananchi wa Kisasida waliotoa maeneo yao kupisha mradi wa umeme wa upepo urudiwe upya ili haki stahili itendeke,” alisisitiza.
Katika mkutano huo viongozi wa CHADEMA walieleza kulishukuru Jeshi la Polisi kwa kutumia busara kuamua ugomvi uliojitokeza baada ya CCM kuingia barabarani na gari ya matangazo kutangaza mkutano eneo ambalo CHADEMA walikuwa wameshapewa kibali kufanyia mkutano.

0 comments:

Post a Comment