Monday, December 31, 2012

Katibu wa Baraza la Vijana wa CHADEMA Mkoa wa Tanga, Deogratius Kisandu, ametangaza kujivua uanachama.

Uamuzi huo wa Kisandu umekuja siku chache baada ya kutangaza maandamano kwa nchi nzima kupinga hatua ya Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Wilbrod Slaa, kumiliki kadi mbili ikiwemo ya CCM.

Akizungumza jana na gazeti la MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu, Kisandu alisema hatua ya kujiondoa ndani ya CHADEMA imekuja baada ya viongozi wa Taifa wa chama hicho kumuandama kutokana na msimamo wake.
Kwa muda mrefu hasa baada ya kutangaza nami nitagombea nafasi ya urais nimeonekana kuwa ninatumiwa na CCM. Na hata nilipotoa tamko la kuitishwa maandamano kwa nchi nzima ya kutaka Dkt. Slaa, ajiuzulu kutokana na kumiliki kadi ya CCM, imekuwa ni chuki na uhasama baina yangu na viongozi.

Kwa hali hiyo nimetafakari kwa kina na leo hii (jana), ninatangaza rasmi kujivua nafasi zote za uongozi pamoja na unachama wa CHADEMA, huku bado nikibaki na dhamira yangu ya kuendelea kuwa mpigania haki. Nitabaki na msimamo wangu wa kugombea urais mwaka 2015 hata kwa kuwa mgombea binafsi bila kupitia chama chochote. Kwa sasa siwezi kusema nitaelekea chama gani ila baada ya muda ninaweza kusema ninaelekea chama gani ingawa si CCM.

Ninajua wazi sisi watu wa kanda ya ziwa ndani ya CHADEMA tumekuwa tukionekana kama virusi kwani alianza Shibuda, kutangaza nia ya kugombea urais, kila kona alipigwa vita na baadaye Zitto nchi nzima inajua hadi leo hii namna ambavyo anavyosakamwa ndani ya chama. Hata nami nilipotangaza hilo, viongozi wa kitaifa waliweza kuwatumia viongozi wa ngazi za chini katika mkoa huu na kwa muda mrefu sasa kumekuwa na hisia hasi juu yangu na Mkoa wa Tanga kwa ujumla, juu ya ushiriki wangu kwenye shughuli za chama.

Natambua kwamba wapo ambao tayari wameniona mnafiki, mamluki na msaliti kwasababu tu ya kutopenda kutambua ukweli juu ya mwenendo wa chama changu cha CHADEMA

alisema Kisandu.
Akizungumzia ziara za Vugu vugu la Mabadiliko (M4C) zimekuwa za kiupendeleo zaidi, bila kuzingatia maeneo ambayo hayakufikiwa na kampeni za Urais mwaka 2010.

Alisema Mkoa wa Tanga umekuwa ukitengwa sana na kutokuthaminiwa katika ujenzi wa chama, huku chama hicho kikijengwa kwa misingi ya kujitolea lakini kutokana na ubinafsi wa viongozi imekuwa ni kikwazo.

“Ninashindwa kuelewa vigezo vya M4C katika kuchagua viongozi wanaotakiwa kushiriki ziara za vuguvugu la mabadiliko (M4C). Inanishangaza kuona mwanachama aliyejiunga jana CHADEMA akitokea CCM, leo anapewa kipaumbele kuliko viongozi waliojenga chama kwa muda mrefu. Tumejenga chama kwa nguvu ya kujitolea hasa huku mikoani, wilayani na majimboni bila kulipwa chochote, leo hii tunaonekana hatufai hatuna maana,” alisema.


---
via gazeti la MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment