Wednesday, December 19, 2012


SPIKA wa Bunge, Anne Makinda


• Mangula atoboa siri ya uteuzi wake

na Mwandishi wetu


SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kujiondoa chenyewe madarakani kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi kutanguliza maslahi binafsi badala ya chama na wananchi kwanza.
Makinda alitoa kauli hiyo juzi wakati akiwasalimu wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Njombe, waliokutana mjini hapa.
Alisema utapeli ndani ya CCM unatisha na watu hawataki kujenga utamaduni wa ujamaa na kujitegemea na kusisitiza iwapo wanachama watashindwa kujitegemea, chama kitakufa.
Alisema hata rushwa kwenye uchaguzi wa CCM inachangiwa na baadhi ya viongozi wasiopenda kufanya kazi na kutegemea kuchuma pesa za rushwa kutoka kwa wagombea.
“Rushwa ndani ya chama inatokana na tabia hii ya watu kushindwa kufanya kazi halali za kujitafutia kipato na kuishia kuwarubuni wagombea na kuwaomba fedha kwa ahadi ya kuchaguliwa. Iwapo wana CCM wataendelea kuomba fedha katika uchaguzi ni mwanzo wa kuua chama na hata vyama vya upinzani haviwezi kuiua CCM ila CCM itajimaliza yenyewe kwa tabia yake,” alisema.
Alieleza kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya wapiga kura wa jimbo lake ambao wamekuwa wakimchangamkia na kumsalimia na mwisho wa salamu, huishia kuomba pesa.
Makinda amewataka viongozi wa CCM kurejea misingi ya kiapo cha mwachama na kukifanyia kazi kiapo hicho ambacho kinatamka wazi kuwa sitatumia cheo changu kwa maslahi yangu na iwapo kiapo hicho kitaendelea kukiukwa kwa baadhi ya viongozi wanaochaguliwa kugeuza nafasi zao ni mitaji ya kuombaomba fedha kwa wabunge, chama hicho hakitadumu.
“Mimi mwenzenu jana baada ya kumaliza mkutano wa mapokezi ya Mangula nilianza kucheza ngoma na muziki na wananchi waliofika katika mapokezi hayo, cha ajabu wengine walikuwa kukisalimia na kuniomba pesa ....sasa hii ni hatari sana kama watu wamekuja wenyewe katika mapokezi baada ya kumaliza mkutano, wanamvamia mbunge na kumwomba pesa,” alisema Makinda.
Kutokana na hali hiyo, Spika Makinda aliwataka wanachama wa CCM kufanya kazi na kuwa na shughuli nyingine za kuwaingizia kipato badala ya kuendelea kuwavizia wabunge na kuwaomba pesa na wasipopewa wamekuwa wakiwachukia na kukichukia chama.
Makinda aliwataka pia wajumbe wa mkutano huo kuwa na miradi ya kiuchumi au kujiunga katika kilimo badala ya kuendelea kuomba fedha kwa wabunge.
Alisema hivi sasa watu wamechoka kuombwa fedha na hata waliokuwa wakikisaidia chama, pia wamechoka hivyo lazima CCM ijitegemee kwa kuwa na miradi ya kiuchumi.
Wakati huohuo wajumbe wa mkutano huo wamemchagua kwa kura za kishindo mbunge wa jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe, kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa toka wilaya ya Njombe baada ya kupata kura 37 kati ya kura 45 zilizopigwa kati ya wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Njombe.
Akitangaza matokeo hayo katibu wa CCM mkoa wa Njombe, Hosea Mpagike, alisema katika wilaya ya Ludewa kulikuwa na wagombea watatu katika nafasi hiyo akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ludewa, Matei Kongo, aliyepata kura 25 na Damiani Mwapinga aliyepata kura 24 na washindi ni wajumbe Filikunjombe na Kongo.
Walioshinda katika ya wilaya ya Wanging’ombe na kura zao kwenye mabano ni Anaupendo Gombela (36) na Happiness Bomba (31).
Washindi kutoka wilaya ya Makete ni Elizabeth Haule (28) na Francis Chaula aliyepata kura 23.
Wakati huohuo, mbunge wa Ludewa, Filikunjombe, amewalipua watendaji wabovu serikalini, mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, bara, Philip Mangula.
Filikunjombe ambaye alipewa nafasi ya kusalimia katika mkutano wa mapokezi ya Mangula mkoani Njombe, alisema kuwa masikitiko ya wananchi juu ya serikali ya CCM yanatokana na baadhi ya viongozi wabovu ndani ya chama na serikalini ambao wamekuwa wakifanya kazi chini ya kiwango na kusababisha wananchi kukichafua na kukichoka chama tawala.
Hivyo alisema kuwa imani ya wana CCM kwa safu mpya ya uongozi chini ya Katibu Mkuu Abdalaman Kinana na Makamu Mwenyekiti Mangula na Makamu wake Zanzibar, Dk. Alli Mohamed Shein, na viongozi wengine ndani ya CCM ni matumaini mapya kwa wana CCM na tishio kwa vyama vya upinzani.
“Ndugu zangu wananchi wa Makambako na mkoa wa Njombe, chama chetu CCM ni chama kizuri sana na safu hii ya sasa chini ya Rais Kikwete, Mangula na Kinana ni safu ya uhakika na itakiwezesha kuendelea kuaminiwa zaidi na Watanzania ...ila tatizo ni viongozi wachache wa serikali wasiowajibika katika nafasi zao,” alisema.
Kwa upande wake Mangula mbali ya kusifu mapokezi aliyopata, alitoboa siri ya uteuzi wake kwamba alikuwa hajui chochote juu ya uteuzi huo na kwamba alishangaa sana kupokea simu ya Rais Kikwete na kumueleza kuhusu kusudio la uteuzi huo.
“Kweli mimi nilikwenda Dodoma katika Mkutano Mkuu wa CCM kama mualikwa ila nikiwa hotelini nilipokea simu ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete, akiomba kuniteua kuwa Makamu Mwenyekiti na baada ya kwenda ukumbini wajumbe wote walinipa kura zote za ndio...kweli namshukuru sana Mwenyekiti wangu na wanachama wote na sasa ni kazi zaidi na sitawaangusha,” alisema Mangula.
Alisema hatafanyakazi kwa kulipa kisasi kwa wana CCM waliokuwa hawaelewani naye.
  

0 comments:

Post a Comment