Thursday, November 15, 2012

Baraza la Famasi linapenda kutoa ufafanuzi  kwa umma  kuhusu Tangazo la Chuo Kikuu Cha Ekernforde - Tanga kuanza udahili (admission) wa wanafunzi katika ngazi ya cheti na diploma katika pharmaceutical sciences, katika gazeti la Mwananchi la tarehe 10 Oktoba 2012 toleo ISSN 0856-7573 Na. 04490.

Baraza la Famasi ni Taasisi ya Serikali iliyoko chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Famasi Na. 1 ya 2011. Baraza hili pamoja na majukumu mengine limepewa wajibu wa:-

  1. Kuhakiki na kupitisha (approval)  Mafunzo  na Mitaala  inayohusu taaluma ya famasi nchini kwa mujibu wa vifungu 4(i),(p) na 5(h)
  2. Kuhakiki, Kusajili na kupitisha Taasisi za Elimu na Mafunzo ya Taaluma za Famasi nchini, na
  3. Kusajili wataalamu wa taaluma ya famasi nchini .      

                                                                                               
Kwa kuzingatia Sheria ya Famasi, 2011, Baraza linapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa Chuo Kikuu Cha Ekernforde kilichopo Tanga Mjini hakijaidhinishwa wala kusajiliwa na Baraza  na hivyo hakitambuliwi wala hakikubaliki na Baraza kutoa mafunzo ya aina yo yote ile katika   taaluma ya  dawa (certificate, diploma or bachelor in pharmaceutical sciences). Vilevile hata mitaala yake ya kufundishia haijaidhinishwa wala kusajiliwa wa Baraza.

Kwa Taarifa hii, Baraza linawatahadharisha wananchi kutotumia chuo hiki kutokana na ukweli kuwa hakitambuliwi kisheria na Baraza la Famasi kwa vile hakijawasilisha taarifa wala kusajiliwa na Baraza. Taasisi yoyote  inayokusudia  kutoa  mafunzo ya dawa, ni lazima ipate idhini ya Baraza ili wanafunzi waweze kusajiliwa pindi watakapokamilisha mafunzo yao.

Baraza linasisitiza kuwa kutokana na Chuo hiki kutokidhi masharti na vigezo vya Sheria, wanafunzi  watakaosoma katika Chuo hiki   hawatatambuliwa wala kusajiliwa na Baraza hivyo kupoteza sifa ya kuajiriwa Serikalini,  Taasisi  binafsi, na hata kujiajiri.

Baraza linapenda kuwasisitizia wananchi ya kuwa kabla ya kumwandikisha mtoto wako katika chuo chochote kinachoendesha masomo ya fani ya famasi, ni muhimu mwenye chuo akuoneshe kibali cha Baraza.
  
Imetolewa na:
Msajili, Baraza la Famasi,
S. L. P. 31818,
Dar es Salaam.

Kwa mawasiliano, Simu: 022–2451007 au 0684/0755-881677/0655881676

0 comments:

Post a Comment