Thursday, November 8, 2012

MAELEZO YA HOJA BINAFSI JUU YA KUSITISHA UGAWAJI WA ARDHI HADI TATHMINI KINA ITAKAPOFANYIKA KUJUA KIASI CHA ARDHI KILICHO MIKONONI MWA WAGENI

[Chini ya Kanuni ya 54(1) na (2)]

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa Kanuni  namba  54(1) , (2)  na (3) ya  Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 naomba kutoa hoja binafsi ya kuitaka serikali  kusitisha zoezi  la ugawaji wa ardhi  kwa wawekezaji ( wa ndani na wa nje)  mpaka hapo tathmini  ya kina itakapofanyika  kuweza kubaini ni kiwango gani cha ardhi kiko mikononi  mwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika,

Katika miaka ya hivi karibuni, kufuatia mtikisiko wa uchumi duniani uliokwenda sambamba na upungufu wa chakula , tumeshuhudia wimbi kubwa la  wawekezaji kutoka nje ,wakinunua au kumilikishwa maeneo makubwa ya ardhi nchini, kwa maelezo kwamba wana nia ya kuwekeza kwa manufaa ya wananchi wenyeji  na Taifa  kwa ujumla , hali ambayo itaweza saidia upatikanaji wa ajira , kukuza uchumi na  kupunguza umasikini .

Kwa kadiri gharama za Chakula na uhitaji wa Chakula duniani unavyoongezeka ndivyo na kasi ya mahitaji ya ardhi yanavyoongezeka , wawekezaji  wanaona ardhi kama biashara nzuri na yenye tija katika miaka ya baadae. Na kwa nchi tajiri zinazoagiza vyakula toka nje ( China,Japan,Korea ya Kusini ,Saudi Arabia nk.) wanaona umiliki wa mashamba makubwa kama njia ya kujihakikishia usalama wa chakula katika nchi zao. Na wakati huo huo Makampuni binafsi makubwa ya kimataifa wanaiona hii kama fursa ya kujitanua kibiashara na kutengeneza faida kubwa.

Mheshimiwa Spika,

Inakadiriwa kwamba kati ya mwaka 2001 hadi 2010 kulikuwa na maombi ya ardhi zaidi ya hekta  milioni 203 katika nchi zinazoendelea. Hii ni sawa na  maombi ya hekta 55,616 kila siku katika kipindi cha miaka 101 Halikadhalika nchini Tanzania katika miaka ya karibuni takriban  hekta milioni nne zimeripotiwa ‘kuombwa’ na  wawekezaji wa nje  kwa kilimo cha mazao  ya mafuta (AGROFUEL) na Chakula. 

Mheshimiwa Spika,

Kasi ya maombi ya ardhi ,na hatimaye kumilikishwa ardhi   wageni, imegeuka shuruba kwa wananchi , wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo wadogo ambao wamejikuta wakiondolewa  kwa katika  maeneo yao ya asili  ili kuwapisha  wageni. Wengi wao wakiachwa hohe hahe, na katika lindi la umasikini mkubwa. Hii inatokana na ukweli kwamba kumekuwa na tafsiri ambayo sio sahihi, kwamba ardhi wanayopewa wawekezaji haina wenyewe/haina mtu /haitumiki . Wakati ukweli ni kwamba maeneo mengi kama sio yote yalikuwa yanatumiwa n a wakulima wadogo .

Mheshimiwa Spika,

Hali halisi inaonyesha kwamba , ni sehemu ndogo sana ya ardhi inayochukuliwa  na wageni inatumika kwa manufaa ya kutatua/kupunguza matatizo ya njaa katika nchi husika . Hali kadhalika maeneo mengi ardhi yanayochukuliwa na wawekezaji hao  huwa hayaendelezwi kama inavyopasa , na yale ambayo yanaendelezwa , yanaendelezwa kwa kiwango kidogo sana huku wananchi wengi wakiachwa pasi na ardhi ya kutosha kwa kilimo. Na katika hatua nyingine, wawekezaji baada ya kupata /kumilikishwa ardhi kwa bei ya kutupa, hawaitumii,wanasubiri ipande thamani  , kisha kuiuza kwa faida kwa wawekezaji wengine.

Mheshimiwa Spika,

Ninaliomba  Bunge lako tukufu , likubaliane na hoja ya kuitaka  Serikali kusitisha zoezi la ugawaji wa ardhi ili kuweza kutoa fursa ,kama nchi kuweza kujitahmini kwa kina, wapi tulikosea ili tuweze kujipanga upya kwa manufaa ya nchi na wananchi. Hii inatokana na ukweli kwamba hata wizara ya ardhi leo wakitakiwa kutoa taarifa sahihi ya ardhi kiasi gani iko chini ya miliki ya wageni,hawana takwimu sahihi,zaidi ya zile chache zilizopatikana kupitia Tanzania Investment Centre (TIC) na ambazo pia zimethibitika kuwa na mgogoro mkubwa kutokana na taratibu kutofuatwa.

Mheshimiwa Spika,

Mifano mingi inaonyesha kwamba  kumekuwa na ubabaishaji mkubwa sana na kuumizwa sana kwa wananchi , na  mbaya zaidi katika mazingira mengine serikali imekuwa kuwadi wa wawekezaji dhidi ya wananchi wake. Kuna haja kubwa kwa waheshimiwa wabunge kutambua kuwa matatizo ya ardhi yanayoikumba Rufiji, Kilombero, Bagamoyo, Kisarawe na lugufu yanaikumba pia Muheza, Pangani, Katavi ,Meatu, Kinondoni, Njombe na Ngorogoro. Hivyo basi kuna haja kubwa ya kujenga mshikamano  kwa kuunganisha nguvu ili kulinda maslahi na rasilimali za umma. Nitatoa mifano michache, kuonyesha uzito wa tatizo hili:

Bonde la Mto Rufiji (Rufiji River Basin)

Hili ni eneo lenye ukubwa wa Km za mraba 176,000. Linajumuisha Rufiji Delta, Luwero,Kilombero na Mto Ruaha..93% ya wakazi wa maeneo wanaozunguka  eneo hili wapatao 500,000 wanajishughulisha na kilimo, kama wakulima wadogo wadogo. Kutokana na umuhimu na unyeti   wa eneo husika kumekuwa na wimbi kubwa la makampuni ya kigeni, wakipeleka maombi moja kwa moja kwenye vijiji au kwa kupitia baadhi ya vyombo vya serikali (RUBADA- Rufiji Basin Development Authority) ambavyo vimeacha majukumu yake na kugeuka kuwadi wa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika,

Makampuni yafuatayo; ( SEKAB  Tanzania Ltd (Sweden), African Green OIL Ltd , SAP Agriculture Ltd (Turkey ), RUBADA na Korean Rural  Community Corporation , Kilombero Plantation  Ltd ( British) , Kilombero Valley Teak  Co. Ltd ( British) , Kilombero Sugar Co. Ltd  (South Africa) , Kilimo cha Yesu ( Uswiss), na Eurovistas (India)  ni kati ya makampuni yaliyomilikishwa ardhi iliyokuwa  inatumiwa na wanakijiji kwa shughuli za kilimo. Wengi wao wakitolewa kwa nguvu ili kuwapisha wawekezaji kwa kurubuniwa kwa kauli tamu.Wakiahidiwa kuletewa maendeleo. Ahadi ambazo nyingi zimegeuka za uongo huku tayari vijiji vikiwa vimepoteza uhalali wa kutumia ardhi yao.

Mheshimiwa Spika,

Taarifa zinaonyesha kwamba katika ukanda huu , ukiacha makampuni ya  Kilimo cha Yesu (Uswis) na Kilombero Sugar Co, kilombero Plantation Co na Kilombero Valley Teak(British), wawekezaji wengine waliokabidhiwa maelfu ya ardhi ya watanzania wameyaendeleza kidogo sana au kuyatelekeza kabisa mashamba ! inawezekana wakisubiri ardhi ipande thamani wawakabidhi wenzao kwa gharama kubwa .2

Kisarawe:

Sun Biofuels Ltd ni kampuni ya kiingereza inayojishughuliza na kilimo Jatropha . Wanahisa wake wakubwa  ni kampuni ya Sun Biofuels Plc ya Uingereza yenye hisa 88% , Julian ozanne ( mwingereza) mwenye hisa 10% na watanzania wawili, Daudi Makobore  na Herbert Marwa wenye hisa 2% (yaani 1% ).

Inasemekana mwekezaji huyu  alipanga kuwekeza  kiasi shilingi bilioni 25.3 za kitanzania, lengo likiwa kujenga mtambo wa kufulia mafuta  na kilimo cha Jatrofa ( pamoja na mihongo kwa ajili ya kuwalisha vibarua). Ilikadiriwa kutokana na uwekezaji huo zingepatikana ajira za kudumu 1,500 , na ajira za ziada kwa vibarua hasa wakati wa uvunaji.

Mwaka 2009 Kampuni ilifanikiwa  kupata eneo lenye ukubwa wa hekta 8,211 kutoka vijiji 11 vya ( Mtamba, Muhanga, Marumbo,Palaka, Kidugalo, Kurui (40% ya eneo la kijiji lilichukuliwa ),Mtakayo, Vilabwa , Mitengwe, Mzenga ‘A’ and Chakaye. Hata hivyo mwezi  Oktoba 2011, mradi husika ulisamama kutokana na ukosefu wa fedha, na mustakabali wa ardhi ya  kijiji haujulikani.

Mwanakijiji mmoja wa kijiji cha  Palaka , Kisarawe alinukuliwa akisema  kwamba walikubali kuwaachia ardhi wawekezaji kwa mdomo, pasi kuandikiana popote kwa sababu waliaziamini ahadi zao za kutoa huduma za jamii i.e maji, barabara,shule nk, lakini hakujua kiasi gani cha eneo lake kinapaswa kuchukuliwa kwa sababu hawakuwa na nyaraka zozote za kuonyesha mipaka ya shamba lake. Hakuwa anafahamu haki zake za kisheria,hivyo hakujua madhara ya kile alichokikubali mpaka alipopoteza ardhi yake yote bila  kulipwa fidia.3

Mwananchi mwingine wa kijiji cha Kurui, alinukuliwa akisema kuna tofauti kubwa kati ya makubaliano ya kutoa ardhi na kushiriki  katika mkutano wa kijiji. Anadai kwamba kushiriki kwao katika kikao cha kijiji ,kulichukuliwa kama kukubali kutoa maeneo yao . Hakuingia makubaliano na mtu yeyote kutoa eneo lake.4 Eneo lilichukuliwa na mwekezaji , majina ya mahudhurio yalitumika kama kielelezo kuonyesha kama waliafiki,wakati hawakufanya hivyo.

Rukwa:

Mheshimiwa Spika

Eneo hili ,linahusisha Hekta 80,317 (Katumba) na 219,800 ( Mishamo) kwa ajili  ya Kampuni ya kimarekani ya Agrisol . Majadiliano yanaratibiwa na viongozi wakubwa  sana Serikalini. Mradi huu umejikita kwenye uendelezaji wa mashamba makubwa , na matumizi ya mbegu zenye viini tete (GMO). Ili kufanikiwa kwa mradhi huu wakulima wadogo wadogo wapatao 162,000 walitakiwa kuhama kumpisha mwekezaji huyo wa kigeni.

Licha ya kelele nyingi kupigwa juu ya makosa ya kiufundi ambayo serikali inayafanya kwa kutaka kulikabidhi eneo kubwa na lenye rutuba kwa wageni , na licha aliyekuwa mshirika muhimu wa Agrisol IOWA State University College of Agriculture ,aliyekuwa mhimili muhimu wa mwekezaji huyu hasa katika kuwasaidia wakulima wadogo kujitoa baada ya kugundua kwamba mwekezaji huyu hana dhamira ya kuisaidia nchi na wakulima wadogo zaidi ya kujinufaisha kibiashara. Na kwamba alikitumia Chuo husika ili apate uhalali wa kukubalika kirahisi kama mwekezaji mahiri. Serikali inaonekana bado imeziba masikio!

Kigoma

Wawekezaji walionunua ardhi mkoa wa Kigoma ni Agrisol na FELISA.

FELISA amenunua ekari 3000 katika wilaya ya uvinza kijiji cha basanza kata ya uvinza. Wawekezaji hawa wamewakuta wakulima na wafugaji katika maeneo haya. Wafugaji na wakulima wakagoma kuondoka kwakuwa walikuwa wakiendesha maisha Yao kutegemea ardhi hiyo Huu ni ushahidi dhahili kuwa hakuna ziada ya ardhi ukilinganisha na mahitaji. Mwekezaji kwa kushirikiana na vyombo vya dola alianza zoezi la kuwatoa wananchi mwezi Mei mwaka huu akitumia vikosi vya mgambo kupiga wananchi, kuchoma nyumba, kuharibu mazao na halikadhalika kuwafungulia wananchi mashtaka!

USHAHIDI ZAIDI KUHUSU MGOGORO HUU TAYARI KUNA KESI MAHAKAMA YA MWANZO MWANDIGA KIGOMA KATI YA WAKAZI WANAOGOMA KUHAMA NA MWEKEZAJI.


AGRISOL

Mwekezaji huyu amepewa hekta elfu 10,000 eneo la Lugufu. Eneo hili ndio ili kuwa kambi ya wakimbizi. Na eneo hili ndio limetengwa kuwa Makao makuu ya wilaya . Kwa mujibu wa Mbunge wa Kigoma Kusini (ambaye eneo lenye mgogoro liko ndani ya jimbo analoliwakilisha), Mhe David Kafulila alipozungumza  na watendaji wa halmashauri walikiri kuwepo shinikizo kutoka ngazi za juu.

Na hii inatokana na mantiki ya kawaida tu kuwa uamuzi wa kumpa mwekezaji huyu Eneo hili ni Sawa na kuamua Makao makuu ya wilaya ya uvinza yazungukwe na shamba na mwekezaji. Hivyo mji ambao ni Makao makuu hautatanuka kwasababu utakuwa eneo dogo sana lililozungukwa na shamba. Nasema eneo dogo kwasababu mpaka sasa haijafahamika Makao hayo makuu yatawekwa wapi wakati eneo lote kashapewa mwekezaji. Labda serikali imwombe Agrissol eneo la kujenga wilaya.

Mheshimiwa Spika,

Zaidi ya mkanganyiko huo pia kuna tatizo la mahitaji ya ardhi, wakazi wa eneo la jirani,wanaotoka Uvinza na Mwamila wanahitaji kulima katika eneo hili lakini wanazuiwa. Taarifa ya mahitaji ya eneo hili kwa wakulima wakawaida ipo ofisi ya mkuu wa mkoa Kigoma.Mkuu wa Mkuu wa Mkoa anakiri kuwa ni tatizo, na kupendekeza labda watu walime kwa muda wakati mwekezaji hajafika. Wakazi mwamila walifanya jaribio la kutaka kulima mwaka huu wakafukuzwa.

Mheshimiwa Spika,

Mchakato mzima wa agrossol kupewa eneo halikuridhiwa na  wana kijiji,halmashauri na wataalamu walishinikizwa. Na isisitizwe kuwa uamuzi huu unakinzana na juhudi za serikali yenyewe kusukuma wananchi katika kilimo kwani wilaya ya uvinza Hivi sasa mbunge amekopa trekta nne ili kusukuma kilimo kwa yeye kulima na wananchi kulimiwa kwa bei ya chini kuliko bei ya serikali.Halmashauri awali ili kuwa na kituo chenye trekta mbili hapo lugufu Kama kituo cha huduma ya matrekta ya kilimo kwanza, pia halmashauri imenunua trekta tano kwa ajili ya kusukuma kilimo wilaya hii. Juhudi zote hizi ambazo ni matunda ya mkopo ya SUMA JKT, INAKWAMISHWA NA UAMUZI WA SERIKALI KUUZA ARDHI.

Mheshimiwa Spika,

Ni muhimu ikaeleweka kwamba,hakuna anayepinga umuhimu wa uwekezaji, lakini ni muhimu vile vile ikaeleweka kwamba hatutaweza kuendelea kama tukikabidhi kila kitu kwa wageni. Sote tunajua ni kwa namna gani dhahabu, almasi  na Tanzanite zimetumika kujenga uchumi wa mabeberu! Hatuwezi kufanya makosa tena kwenye rasilimali hii muhimu ya ardhi  inayopanda thamani kwa kasi sana! Uchumi hauwezi kuachwa uendeshwe na watu wa nje!

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na uwekezaji kutoka nje wa makampuni makubwa uchumi wa Tanzania unarekodiwa kukua kwa asilimia 7. Hiki ni kiasi kikubwa kinachoifanya nchi hii kuwa miongoni mwa nchi 20 kileleni kwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi dunia lakInI wakatihuohuo inasikitisha kuona nchi hii ni miongoni mwa nchi 20 duniani. Hii inatokana na ukweli kuwa kilimo kinachoajiri 70% ya watanzania kimeachwa, njia ya kuondoka kwenye mlinganyo(equation) hiyo ni ARDHI. wakulima wadogo wagawiwe ardhi, wawezeshwe zana na ufundi kwa kilimo.

Mheshimiwa Spika,

Mambo kadhaa yamejitokeza :

  1. Uvunjwaji wa haki za binadamu
  2. Kutokuzingatiwa kwa sheria inayotaka wananchi ,waarifiwe mapema washirikishwe na kupewa taarifa sahihi , ili wafanye uamuzi ulio sahihi kwa maendeleo yao (the principle of free ,prior and informed concent-FPIC)-kuhusiana na mradi husika.
  3. Mikataba iliyotawaliwa na usiri mkubwa, na wakati mwingine sheria za nchi kupuuzwa .
  4. Serikali kulipwa fedha kidogo sana. Wastani wa gharama ya kukodi ardhi ni shilingi 200 kwa hekta kwa mwaka. Na muda wa kukodisha ardhi kisheria ni miaka 99.Gharama hii haijalishi eneo shamba lilipo au mazao yanayozalishwa.
Mheshimiwa Spika,

Inawezekana kabisa Tanzania tukawa hatujafikia  hali mbaya kama ilivyo kwa nchi nyingine.....zaidi ya 30%  ya ardhi ya Liberia imekabidhiwa kwa wakulima wakubwa  wa Nchi za magharibi katika kipindi cha miaka mitano! Halikadhalika katika nchi ya Cambodia , inakadiriwa  linalokadiriwa kuwa 56-63% ya ardhi yote inayotumika kwa Kilimo iko mikononi mwa makampuni binafsi ya kigeni. Hivyo basi Serikali ya Tanzania ina fursa ya kujipanga mapema,kabla hali haijawa mbaya! Lazima kuwe na mjadala mpana wa kitaifa ili tuweze kupata njia bora ya kusonga mbele.Hatuta kuwa wa kwanza kufanya hivyo. Jirani zetu wa Msumbiji  wa Msumbiji wamefanya hivyo, halikadhalika serikali ya Papua New Guinea !

Ni muhimu kufanya maamuzi sasa . Maamuzi tutakayoyafanya sasa yatakuwa na athari chanya ama hasi kwa kizazi kijacho . Inakadiriwa ifikapo mwaka 2050 watanzania tutakuwa milioni 150, kama leo ardhi yetu tunagawa kwa wageni kwa muda wa miaka 99, tunaweka akiba gani kwa kizazi kijacho? Nini usalama wa Chakula na Uchumi kwa Tanzania ya kesho?

HOJA BINAFSI KUHUSU KUSITISHA UGAWAJI WA ARDHI KWA WAWEKEZAJI HADI TATHMINI YA KIASI CHA ARDHI ILIYOGAWANYWA UTAKAPOFANYIKA

[Chini ya Kanuni ya 54(3)]

Mheshimiwa Spika,

Kwa kuwa rasilimali ardhi ndio urithi pekee wa asili wa mtanzania katika kujitafutia riziki na kuendesha maisha yake;

Na kwa kuwa  idadi ya watu inaongezeka wakati ukubwa wa ardhi hauongezeki jambo ambalo linaonesha dhahiri kwamba kuna hatari ya kiasi cha ardhi kilichopo kisitosheleze mahitaji halisi ya wananchi;

Na kwa kuwa kumekuwa na ugawaji ardhi kwa wawekezaji hasa wa nje  usiojali mahitaji ya ardhi kwa wananchi siku za mbeleni;

Na kwa kuwa  imebainika kwamba  uwekezaji  katika ardhi unaofanywa na makampuni ya nje haujawasaidia wananchi kwa maana ya fursa za ajira na upatikanaji wa chakula kwa kiwango kilichoahidiwa na Serikali na makampuni hayo;

Na kwa kuwa ugwawaji huu wa ardhi kwa wawekezaji unakwenda sambamba na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na wananchi waliokuwa katika maeneo hayo kupigwa, kuvunjiwa nyumba zao na kufukuzwa bila kulipwa fidia;

Na kwa kuwa kwa kiasi kikubwa zoezi la ugawaji ardhi kwa wawekezaji linakiuka sheria za nchi ambazo zinataka wananchi waarifiwe mapema juu ya ugawaji huo wa ardhi na kushirikishwa kikamilifu ili waweze kufanya maamuzi sahihi kwa maendeleo yao jambo ambalo halifanyiki;

Na kwa kuwa mikataba ya ugawaji wa ardhi inafanyika kwa usiri mkubwa  jambo ambalo linaashria mazingira ya rushwa na kutia shaka kama maslahi ya nchi yanazingatiwa;

Na kwa kuwa  Serikali inapata kodi kidogo sana kutokana na uwekezaji katika ardhi ( yaani shilingi 200 kwa hekta kwa mwaka) na ikizingatiwa muda wa kukodisha ardhi kisheria ni miaka 99;

Na kwa kuwa asilimia 80 ya watanzania wanategemea ajira katika sekta ya  kilimo ambacho msingi wake ni ardhi;

Na kwa kuwa Ibara ya 63(2)(c) na (d) ya Katiba ya Jamjhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inasema kwamba: “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza; kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu na wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo; kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria”;

HIVYO BASI, naliomba Bunge liazimie:

  1. KWAMBA, zoezi la ugawaji ardhi kwa wawekezaji wa nje na ndani lisitishwe hadi hapo tathmini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiasi gani cha ardhi kipo mikononi mwa wawekezaji na wasio wawekezaji.
  2. KWAMBA, tathmini ya kina ifanyike kuweza kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliojipatia ardhi kinyemela kupitia serikali za vijiji kinyume na matakwa ya sheria ya ardhi Na. 5 ya mwaka 1999.
Mheshimiwa Spika,

Baada ya kusema hayo,

Naomba kutoa hoja.

…………………………………..

Halima James Mdee(Mb)

Jimbo la Uchaguzi-Kawe

05.11.2012

1  ILC ( 2011)  ‘Land Rights and the Rush for Land’, http://www.landcoalition.org/cpl/CPL- Synthesis-report. 

2 Land Grabbing in a post investment period and popular  reaction in the Rufiji River Basin. A Research Report by Haki Ardhi,2011. Study carried out  by Dr . Abunuwasi Mwami of the Department of Sociology , University of Dar es salaam and Dr Ng’wanza Kamata of the Department of Political Science , University of Dar es salaam

3 Participant in Community focus Group discussion , Palaka Village , Kisarawe  District , December 3 , 2010 cited in Frederic Mousseau et al . “Understanding  Land Investment Deals in Africa – Country Report Tanzania”

0 comments:

Post a Comment