Monday, October 22, 2012

 
Picture
Aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema (katikati) akiwa na Mawakili, Alute Mughway (kushoto) aliyesimamia kesi iliyomvua Ubunge na Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni wakili katika kesi ya kupinga kuvuliwa Ubunge wake, Tundu Lissu, katika msiba wao baba yao Alute na Lissu aliyefariki hivi kaibuni jijini Dar es salaam na kisha kuzikwa nyumbani kwao Singida. (picha ya Septemba 2012 via MjengwaBlog.com)
Uamuzi wa pingamizi zilizowekwa na mawakili wa pande zote mbili katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa CHADEMA, Godbless Lema utatolewa Jumatatu ijayo.

Awali wa upande wa majibu rufani katika kesi iliyomng’oa madarakani Lema, Alute Mughwai ambaye ni Wakili wa wanachama watatu wa CCM, aliiomba Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa hiyo iliyowasilishwa kwao kwa kuwa ni batili na ina makosa mengi ya kisheria.

Habari za uhakika kutoka katika vyanzo vya habari ndani ya mahakama na kuthibitishwa na mmoja wa wanachama hao waliofungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kupinga Lema kuwa mshindi katika Jimbo la Arusha, Mussa Mkanga vilisema kuwa pingamizi hizo zitatolewa uamuzi siku hiyo.

Mkanga alipoulizwa kama ana taarifa ya kusomwa kwa pingamizi hizo, siku hiyo alikiri kupewa taarifa na mahakama na kueleza kuwa siku hiyo watakwenda kusikiliza uamuzi wa pingamizi zao.

“Mimi na wenzangu kama walalamikaji tumeshapewa taarifa na mahakama juu ya siku na tarehe ya kusomwa pingamizi hizo na tuko tayari kwa hilo,” alisema Mkanga.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, George Hubert hakupatikana kuelezea taarifa hiyo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana, lakini habari za kimahakama zilithibitisha tarehe hiyo ya uamuzi.

Katika hoja zake za kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali, Mughwai aliwaeleza majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu Othmani Chande kuwa kesi hiyo kuwa ni batili kwa kuwa imekosa vitu muhimu vya kisheria, ikiwamo tarehe ya rufaa hiyo kuandaliwa, kulalamikia kipengele ambacho hakijamtoa Lema madarakani pamoja na kutokuwa na muhuri wa Mahakama Kuu iliyoidhinisha rufaa hiyo.

Mughwai alisema katika nakala ya hati ya kukazia hukumu iliyowasilishwa mahakamani hapo, haina tarehe ya kuandaliwa kwake hali inayotia wasiwasi iwapo itakuwa imeandaliwa ndani ya kipindi kinachotakiwa kisheria cha siku 60 tangu kutolewa kwa hukumu au la.

Alidai mbali na nakala hiyo kukosa tarehe ya kuandaliwa kwake, pia haikuwa na muhuri wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuthibitisha kuwa ni kweli imetolewa na mahakama hiyo kwa kuwa nakala hiyo ilikuwa na saini tu ya Jaji Gabriel Rwakibarila ambayo haithibitishi uhalali wake.

Naye Wakili wa waomba rufaa, Method Kimomogoro akijibu hoja hizo, alikiri kuwa ni kweli nakala hiyo ina upungufu na ni makosa ya kibinadamu ambayo hata hivyo hayana athari katika kesi ya msingi hivyo aliwaomba majaji kutupilia mbali pingamizi hizo.

Aidha, Wakili wa Serikali, Timon Vitalis aliunga mkono hoja zilizotolewa na Wakili Kimomogoro huku akidai  suala hilo la upungufu, lawama hazipaswi kuelekezwa kwa waomba rufani wala mawakili, bali zinapaswa kuelekezwa kwa mahakama ambayo ndiyo iliyoandaa hati hiyo.

---
Taarifa hii imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Ziro99

0 comments:

Post a Comment