Monday, October 22, 2012

Kambi  ya Upinzani Bungeni imewashitaki Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Naibu Waziri, George Simbachawene, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, ikitaka wawajibike kutokana na kupotosha ukweli katika kuelezea hali tete ya umeme nchini.

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, alisema viongozi na watendaji wa wizara hiyo pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamekuwa wakitoa matumaini potofu kwa wananchi kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini na uboreshaji wa shirika hilo.

Alisema wananchi wawe wanazipokea kwa tahadhari kauli hizo kwa kuwa hazielezi ukweli kamili kuhusu hali tete ya umeme nchini kutokana na kusuasua katika utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme.

“Kutokana na hali hiyo na kwa kuzingatia kuwa mamlaka na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa katiba ni kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi, nimemwandikia barua Spika wa Bunge ili Wizara ya Nishati na Madini iwajibike kueleza hali halisi katika mikutano ya kamati za Bunge inayoendelea hivi sasa,” alisema Mnyika.

Alisema kwa mujibu wa nyaraka alizokuwa nazo (Mnyika) kuanzia Septemba hadi Oktoba, mwaka huu, hali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini imekuwa tete kwa sababu mbalimbali, ikiwamo upungufu wa upatikanaji wa mafuta na gesi asili kwa ajili uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme.

Mnyika alisema hali hiyo imesababisha umeme kutoka kwenye mabwawa kuzalishwa zaidi ya kiwango kilichopangwa na kusababisha kushuka kwa kina cha maji, hali inayotishia uendelevu wa mabwawa kutokana na maelekezo ya wizara kwa TANESCO ya kuhakikisha mgawo wa umeme hautangazwi kwa namna yoyote.

Alisema amechukua hatua ya kuandika barua hiyo kwa spika kutaka atumie madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni ya 116 na kanuni ya 114 fasili ya 14 kukabidhi suala hilo lishughulikiwe na kamati nyingine miongoni mwa kamati za kudumu za Bunge zinazoendelea na vikao vyake hivi sasa.

“Kwa barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme na utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme lishughulikiwe na kamati nyingine kwa haraka kwa kuzingatia maelezo na maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati wa kuahirisha mkutano wa nane wa Bunge,” alisema.

Alisema atakabidhi sehemu ya nyaraka alizonazo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayoelekezwa na Spika kushughulikia suala hilo na iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa ataziweka hadharani kwa umma kupitia vyombo vya habari ili Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO wawajibishwe kueleza ukweli kwa ukamilifu.

Mnyika alisema mapitio ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa TANESCO yahusishe pia kamati ya kudumu ya Bunge itakayopewa jukumu hilo kuelezwa hatua iliyofikiwa katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika TANESCO kwa kuzingatia kuwa siku 60 zimepita, ambazo ilielezwa kuwa uchunguzi utakuwa umekamilika.

0 comments:

Post a Comment