Saturday, September 15, 2012


  • Waandishi Wetu - RAIA MWEMA.

    Toleo la 258 12 Sep 2012
    *Madai ya matumizi ya fedha chafu yaibuka
  • Udini na ukabila nao watajwa

ANATAJWA majina makubwa: Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Hamisi Mgeja, Anthony Diallo, James Lembeli, Clement Mabina, kwa uchache katika mchakato wa kutafuta kupitishwa kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya chama tawala CCM katika chaguzi za chama hicho zinazoendelea.


Taarifa zinasema kwamba pengine mpambano wa safari hii utakuwa mkali zaidi kwa kuwa ndio utakaoamua ni nani hasa wanasimamishwa na chama hicho katika kuelekea kumpata mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati huko Arusha anatajwa Lowassa kupambana na hasimu wake wa muda mrefu Dk. Salash Toure, mkoani Manyara uwezekano mkubwa mpambano huo utawakutanisha Sumaye na Mary Nagu; Diallo na Mabina (Mwanza) na Mgeja na Lembeli (Shinyanga) huku taarifa zikisema pia kwamba mchakato wenyewe umegubikwa na malalamiko ya matumizi ya fedha, uhasama wa kisiasa na hoja za kikabila.


Hali hiyo inajitokeza katika wakati ambao uongozi wa jumuiya za chama hicho unazua mvutano na mchuano mkali, kuanzia Umoja wa Wanawake (UWT), Umoja wa Vijana (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, mkoani Mbeya habari zinaeleza kuwapo kwa mawakala wa baadhi ya wanasiasa wanaotarajia kuomba ridhaa ya chama hicho kikongwe nchini kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.


Mwandishi wetu huko anaripoti kwamba baadhi ya makada wa CCM wamethibitisha kuwapo kwa mawakala hao na zaidi ya hapo, wengine wamekuwa na fedha wanazogawa kushawishi baadhi ya wajumbe na viongozi kupitisha majina ya wagombea wa kundi lao.


Hali ya Mbeya si tofauti sana na ilivyo mkoani Shinyanga ambako nako kuna uhasama wa kisiasa baina ya makundi ya kisiasa ambayo mzizi wake umesambaa hadi ngazi ya Taifa. Huko nako kunadaiwa ‘kumwagwa’ fedha ili kusaidia mtandao wa wanasiasa wanaolenga kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM 2015.


Katika Mkoa mpya wa Simiyu, wabunge wa sasa na wengine wastaafu kama ilivyo kwa Shinyanga, nao wamejitokeza kwa wingi wakitaka kuchaguliwa kuongoza chama hicho kikongwe ambacho kinakabiliwa na ushindani wa kisiasa kutoka upinzani na hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Waandishi wetu wanaripoti kutoka Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mbeya kama ifuatavyo:


CCM Mwanza

Kutoka Mwanza, mwandishi wetu anaripoti kuwa, wakati mchakato wa kupata wagombea na viongozi katika nafasi mbalimbali ndani ya CCM ukiendelea maeneo mbalimbali nchini, mkoani Mwanza mchakato huo umekumbwa migawanyiko ya kikabila na makundi yanayopigana vikumbo kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Mchujo wa kamati ya siasa ngazi ya Mkoa kupendekeza majina kwa Kamati Kuu ya chama hicho ngazi ya Taifa kwa ajili ya uteuzi wa wagombea katika ngazi ya mkoa na wilaya umelalamikiwa na baadhi ya wagombea ambao wanaamini wamechujwa au kuwekewa alama za chini katika mchakato huo kwa vigezo vya ukabila au makundi ya urais 2015.


Taarifa kutoka ndani ya vikao vya chama na kwa baadhi ya wagombea zinasema kuwa katika mchakato huo, taarifa za kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pia ilitumika katika kuwawekea alama za chini ili kuweza kufanikisha malengo ya kisiasa ya baadhi ya watu.


Mmoja wa waliojitokeza kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Mwanza (jina linahifadhiwa) amelieleza Raia Mwema kuwa katika mchakato wa kuwapa alama za mapendekezo kwa Kamati Kuu ya CCM, kulikuwa na hatua za makusudi kudhoofisha kundi la watu ambao si wazawa wa Mkoa wa Mwanza na hivyo kufanya uchaguzi huo uwe na kasoro za kikabila.


“Mimi nimeulizwa swali na kiongozi mmoja wa serikali kuwa nikichaguliwa nitaweza kudhibiti wimbi la Wakerewe na Wahaya katika siasa za Mwanza? Sasa hivi kama tumefikia hali hiyo tunatarajia nini? Hiki chama si tunakiuwa?”, alihoji mgombea huyu ambaye taarifa zinaeleza kuwa alipata alama C.


Kwa mujibu wa mgombea huyo, tatizo la ukabila liliwahi kuibuka huko nyuma na likadhibitiwa vilivyo lakini sasa limeanza tena kwa kasi.


Kwa upande wa wagombea wa nafasi za uenyekiti wilaya za Nyamagana na Ilemela, wimbi hilo pia halikuwaacha salama na tayari baadhi yao wamewasilisha rufaa zao kwa sekretariati kupinga uamuzi uliofikiwa na baadhi ya vikao vya mchujo.


Richard Rukambula ambaye anawania nafasi ya mwenyekiti Wilaya ya Ilemela anakiri kubaguliwa kikabila na tayari amewasilisha malalamiko yake kwa sekretariati ya chama hicho kupinga kasoro hiyo.


“Kamati ya siasa imekuwa na mambo ya ajabu sana, wanaendekeza ukabila na kuwabagua wagombea wengine. Nimewaandikia sekretariati na sasa nasubiri kamati kuu kuamua,” alisema.


Taarifa za ndani ya vikao hivyo vya chama vinaeleza kuwa katika nafasi ya mwenyekiti waliopatiwa nafasi za juu kwa maana ya alama nzuri ni mwenyekiti wa sasa anayetetea nafasi yake, Clement Mabina, aliyepewa alama B, mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa wa Mkoa huo anayewania nafasi ya uenyekiti, Anthony Diallo amepata alama B na Barnabas Mathayo ambaye pia amepewa alama B.


Wagombea waliobaki ama walipata alama C au za chini zaidi ili kupunguza uwezekano wa kuteuliwa kuwania nafasi walizoomba.


Annaser Mkiwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti Wilaya ya Ilemela ambaye anadaiwa kuwa mmoja wa waliopewa alama za chini kwa kuwa si mzawa wa mkoani Mwanza, anasema hana taarifa hizo lakini kama huo ndiyo ukweli anasubiri matokeo ya kamati kuu ili baadaye atoe msimamo wake.


“Kulikuwa na njama za hapa na pale, na hata hili la ukabila limejitokeza sana wakati wa kampeni hizi, lakini uamuzi wa vikao hivi (vya kuwapatia alama wagombea) ni siri na taarifa yao inakwenda kamati kuu, kama kuna watu tayari wanajua wana alama kiasi gani hilo nalo ni tatizo jingine kwenye mfumo wetu kama chama,” anasema.


Anasisitiza kuwa hawezi kufanyia kazi maneno ya kusikia na kwamba anaamini katika wagombea wote hakuna anayejua nafasi yake na amepewa alama kiasi gani, lakini matokeo ya kamati kuu yakija hapo atakuwa na jambo la kusema.


Hata hivyo, juhudi za mwandishi wetu kuwapata katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce Masunga na viongozi wengine wa vikao vya uamuzi hazikuweza kuzaa matunda kwa kuwa wapo katika ziara ya Waziri Mkuu inayoendelea mkoani hapa.


CCM Mbeya

BAADHI ya vigogo wa Chama cha Mapinduzi waliotarajiwa kujitokeza kwenye uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho kwa Mkoa wa Mbeya wamejiweka pembeni, huku wachache wakijitokeza kuwania nafasi za juu mkoani humo.

Hatua ya vigogo hao kukaa pembeni imeufanya uchaguzi huo kupoa kwa muonekano wake wa nje, lakini hali halisi ya duru za ndani ikiwa tofauti, ikielezwa kupanda kwa joto la uchaguzi.


Miongoni mwa vigogo waliotarajiwa kutikisa uchaguzi huo mkoani Mbeya ni pamoja na Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyewahi kuwa mbunge wa kuteuliwa katika Bunge la tisa, Thom Mwang’onda ambaye katika uchaguzi uliopita alichuana na Profes Mark Mwandosya katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kupitia Mkoa wa Mbeya.


Katika uchaguzi huo uliogubikwa na matumizi makubwa ya rushwa ya wazi wazi, Prof. Mwandosya alimshinda Thom Mwang’onda, mtoto wa aliyekuwa kachero namba moja nchini, pamoja na kuungwa mkono kwa nguvu na uongozi wa juu wa chama hicho na serikali mkoani humo.


Prof. Mwandosya safari hii anagombea nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Rungwe, ambako anatarajiwa kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mwanachama mwingine kijana, Richard Kasesela, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Madini nchini na pia ni mwenyekiti wa Shirikisho la Biashara Afrika.


Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Kasesela alipambana na Profesa David Mwakyusa katika kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho lakini aliangushwa na katika kura za maoni ambazo hata hivyo, matokeo yake yaliibua utata na malalamiko.


Hatua ya chama hicho kupeleka nafasi hiyo ngazi ya wilaya kunaelezwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa mkoani Mbeya kwamba imelenga kupunguza minyukano ndani ya chama hicho mkoani hapa.


Pamoja na kupoteza mvuto nje ya dura za chama hicho, joto la uchaguzi wa mwaka huu linaelezwa kuwa kali zaidi kutokana na kuhusishwa na harakati za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, huku vigogo wanaotajwa kuwa na nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete wakitajwa kufadhili baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali zinazowaingiza kwenye vikao vya juu vya uamuzi wa chama hicho.


Kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, kigezo cha elimu kinaelezwa kutokuwa na nafasi sana katika uchaguzi huo mkoani Mbeya, kinachozingatiwa zaidi ni upambe, mtu anayemhakikisha muwania urais mtarajiwa kura.


Kivutio kikubwa kipo katika nafasi ya mwenyekiti wa mkoa. Wabunge wawili wakiwa wamejitosa kuwania nafasi hiyo huku anayeishikilia, Nawab Mulla, akitangaza kutotetea nafasi yake hiyo.


Kujitoa kwa Mulla kutetea nafasi yake kumepokelewa kwa mitazamo tofauti, lakini kubwa linaloelezwa ni mwenyekiti huyo kutotimiza ahadi zake ambazo ni pamoja na kuleta utulivu ndani ya chama hicho. Mulla badala ya kuleta utulivu amejijengea taswira ya kuonekana ni kiongozi aliyezidisha mpasuko ndani ya CCM na pia anatajwa kushindwa kuanza ujenzi wa ofisi za chama za mkoa na ahadi yake ajira kwa vijana.


Kwa upande wa wabunge waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ya mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya ni Godfrey Zambia (Mbozi Mashariki) na Victor Mwambalaswa wa Jimbo la Lupa wilayani Chunya, wote wakitegemea kutumia zaidi kete ya misimamo yao bungeni kuhusu maslahi ya taifa.


Pamoja na wabunge hao, yupo pia aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mbeya Mjini, Allan Mwaigaga ambaye ni wazi atasafiria zaidi mafanikio yake, hasa katika ukarabati wa jengo la ofisi za chama hicho pamoja na kufufua gari la chama pasipo kutegemea fedha za wahisani.


Katika nafasi hiyo wamo wanachama wengine watano ambao ni Brown Mwangomale, Laurence Mfwango, Kura Mayuma, Reginald Msomba na Prince Mwaihojo.


Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Manganga Sengerema, anasema mwenendo wa uchaguzi ndani ya chama hicho kwa mkoani kwake ni mzuri na hadi sasa hakuna vurugu wala matumizi ya fedha.


Lakini katibu huyo anapingwa na baadhi ya wanachama wa chama chake ambao wanakiri kuwapo kwa matumizi ya fedha zinazodaiwa kutoka nje ya mkoa huo, zikihusishwa na wawania urais mwaka 2015.


“Watu wana uzoefu wa uchaguzi uliopita wa chama na Uchaguzi Mkuu, wanaendesha mambo yao kwa siri sana lakini nataka nikwambie, mawakala wao wapo wilayani kuhakikisha watu wao wanapita,” anasema kiongozi mmoja wa chama hicho ngazi ya wilaya, ambaye hata hivyo aliomba jina lake kutotajwa gazetini.


Katibu wa CCM Wilaya Mbeya Mjini, Ray Mwangwala analielezea joto la uchaguzi huo kuwapo zaidi kwenye nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho na ile ya mwenyekiti.


Katika NEC yupo mwanasiasa aliyezua utata katika uchaguzi mdogo Jimbo la Mbeya Vijijini, Sambwe Shitambala alipogombea kupitia CHADEMA na kushindwa lakini huku wafuasi wake wakiamini kuwa amewauza hivyo kutimkia CCM.


Jina jingine lenye kusisimua ni Kamanda wa Vijana wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Stephen Mwakajumilo, ambaye pia ni mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania, tawi la Mbeya. Katika Uchaguzi Mkuu uliopita alipambana na Prof. Mwandosya Jimbo la Rungwe Mashariki na kubwangwa kwenye kura za maoni.


Hata hivyo, anasema nguvu kutoka nje ya mkoa huo hazijajitokeza bado, hali anayoiona ikichangiwa zaidi na hatua ya uchaguzi waliyopo ambayo majina ya wagombea yanasubiriwa kutoka kwenye michujo ngazi za juu.


Kujitokeza kwa wabunge kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho tawala kunaelezwa kuviweka vyombo vya juu vya uamuzi vya chama hicho katika wakati mgumu kutokana na sheria na kanuni za chama hicho kuzuia.


Wilaya za Kyela, Mbozi, Chunya, Mbarali, Mbeya Vijijini, Ileje na Momba zinaelezwa kutokuwa na joto la kusisimua sana, ikilinganishwa na Mbeya Mjini, Rungwe na Mkoa.


CCM Shinyanga

Mwandishi wetu kutoka Shinyanga anaripoti kuwa, CCM mkoani humo kinazidi kujijeruhi kwa kadiri uchaguzi wake wa ndani unavyoendelea kutokana na kambi za uchaguzi za kisiasa ndani ya chama hicho kuendeleza wimbi la uhasama.

Hadi sasa uchaguzi uliokamilika ni ule wa Jumuiya za chama hicho ngazi ya shina hadi wilaya, ukifuatiwa wiki ijayo na ngazi ya chama wilaya.


Kila ngazi iliyomaliza uchaguzi, wagombea wamedaiwa kuwekwa na kuwezeshwa na wagombea watarajiwa wa ngazi zinazofuata kama hatua ya kujijengea mtaji wa kampeni.


Katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, nafasi inayotarajiwa kuibua mchuano mkali ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa. Katika nafasi hiyo, wanasiasa wakongwe na baadhi ya wabunge wa Bunge la sasa wamechukua fomu kuwania nafasi hiyo.


Wagombea kwa Mkoa wa Shinyanga ni Mwenyekiti wake wa sasa, Hamis Mgeja, ambaye atachuana na Mbunge wa sasa wa Jimbo la Kahama, James Lembeli.


Wengine ni Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Hassan Mwendapole, Erasto Kwilasa na Mbunge wa zamani wa Shinyanga Mjini, Leonard Derefa.


Mgeja na Lembeli, mahasimu wakubwa wa kisiasa kwa miaka kadhaa sasa, wanatarajiwa kuchuana vikali kama Kamati Kuu ya CCM itarejesha majina yao kwa ajili ya kupigiwa kura na wanachama.


Wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wilayani Kahama, Septemba 8, wiki iliyopita, Mgeja alikana mbele ya kiongozi huyo kuwa na uhasama wa kisiasa na Lembeli na kudai kuwa, anafahamu vyema hakuna mtu aliye na hatimiliki ya uongozi nchini na kwamba, uongozi ni ridhaa ya watu, sawa tu na watu wawili wanaochumbia mwali, anayekubaliwa ndiye mshindi na wengine wanapaswa kupotea.


"Sina uhasama wala ugomvi wa kisiasa na Lembeli. Lembeli ni ndugu yangu, tunachonganishwa na wapambe. Hawa wapambe ni sawa na machinga wa kisiasa, ni watu hatari sana, wanatugawa," alilalama Mgeja.


Duru za kisiasa mkoani Shinyanga zinampa Mgeja nafasi kubwa ya ushindi kutokana na mtandao wake mkubwa wa wapambe na wafadhili wa kisiasa.


"Mgeja ni mtu hatari sana, yuko kambi ya ufisadi ambayo ndiyo yenye nguvu na wakikosea tu jina lirudi wagombea wengine hawaoni ndani," alidai kada mmoja wa CCM ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya mwenyekiti katika moja ya wilaya za mkoa huo.


Kuhusu Lembeli anasema: "Ni mtu mwema na mwadilifu, lakini kwa bahati mbaya yeye ni wa kundi la wapambanaji dhidi ya ufisadi, hivi kwamba kura hazitatosha kwake."


Kada huyo wa CCM alibainisha pia kwamba, kwa kuwa Lembeli ni mbunge, kuna uwezekano jina lake lisirudi kwa sababu kwa saa chama hakioni sababu ya watu kuhodhi madaraka mengi, wakiwamo wabunge.


Ukiwaondoa Mgeja na Lembeli, wagombea waliobaki hawana ‘misuli’ ya kutosha katika siasa za Shinyanga kwa sasa. Na ikitokea kwamba Kamati Kuu ya CCM itaamua kukata mzizi wa uhasama wa vigogo hawa wawili ambao umeyumbisha siasa za mkoa huu kwa kutopitisha majina yao, basi nafasi ya mwenyekiti wa CCM mkoa huu itakwenda kwa mgombea asiyetarajiwa.


CCM mkoani Simiyu

Katika mkoa mpya wa Simiyu, mwandishi wetu anaripoti kuwa mpambano ni kati ya Lazaro Enock, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wilayani Meatu, Mbunge wa zamani Mkoa wa Shinyanga (Viti Maalumu), Joyce Nhamanilo; Mwenyekiti mstaafu wa CCM wilayani Bariadi, Charles Nkenyenge; Mwenyekiti mstaafu Wilaya ya Meatu na Mbunge wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Constantine Sementi Shillingi, Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk. George Nangale, Mbunge wa Busega Dk. Titus Kamani; Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Bariadi, Musolini Gwalugwa na Mbunge wa Meatu kwa vipindi viwili mfululizo hadi mwaka 2005, Jeremiah Mlyambate.

Inatabiriwa mpambano utakuwa mkali kati ya wagombea nyota wanne ambao ni Luhaga Mpina, Dk. Kamani, Dk. George Nangale na Joyce Nhamanilo. Wagombea waliobaki hawana nguvu kubwa ya ushindani wa kisiasa.


Na kama chama hakitapitisha majina ya wabunge, kama inavyonong'onwa basi, mchuano utakuwa ni kati ya Joyce Nhamanilo na Dk. George Nangale ambaye anapewa nafasi kubwa ya ushindi.


Wagombea Luhaga Mpina, Dk. Kamani na Dk. Nangale wanapewa nafasi kubwa kwa sifa yao ya kutofungamana na makundi hasimu ya kisiasa ambayo ni kambi ya kundi la watetezi wa "ufisadi" na kambi ya upambanaji dhidi ya ufisadi, ambayo yametokea kuyumbisha siasa za Kanda ya Ziwa; na zaidi ya yote, umri wao wa kati na uelewa wa siasa safi na matatizo ya wananchi na ya wanachama wa chama chao kwa ujumla.


Mikoa ya Shinyanga na Simiyu ambayo kabla ya mwaka jana iliunda mkoa mmoja wa Shinyanga, inakabiliwa na changamoto kutoka vyama vya upinzani vya CHADEMA na CUF, kwa hiyo, CCM kitahitaji viongozi makini zaidi wenye maono, uelewa mkubwa na mpana juu ya mchakato wa siasa nchini ili kukabiliana na hali hiyo. Kati ya majimbo manane ya uchaguzi ya Mkoa wa Simiyu, manne yanashikiliwa na wabunge wa vyama vya upinzani.


Majimbo hayo ni Maswa Magharibi (CHADEMA), Bariadi Mashariki (UDP), Maswa Mashariki (CHADEMA) na Meatu (CHADEMA).

0 comments:

Post a Comment