Saturday, September 15, 2012

UTAFITI uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa zaidi ya wajane 544 wametendewa vitendo vya kikatili, ikiwamo kubakwa na mashemeji zao kuanzia Januari hadi Julai, mwaka huu.

Utafiti huo unaonyesha kuwa kati ya hao, wajane 18 walirithiwa na kutakaswa wakati nane walilazimishwa kuingiliwa kinyume cha maumbile kwa imani ya kusafisha mikosi katika ukoo.

Taarifa ya utafiti huo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC), Theodosi Muhulo. Alikuwa akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari, iliyolenga kukemea vitendo vya kikatili na kibaguzi vinavyoendelea dhidi ya wajane.

Muhulo alisema utafiti uliofanywa na kituo umebaini kuwa baadhi ya wajane wamekuwa wakiporwa ardhi na mali walizoachiwa na waume zao pindi wanapofariki. Alisema utafiti huo ulifanywa kupitia kikosi kazi cha kamati ya mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW).

Alisema idadi hiyo ni kutoka katika vituo vya Dar es Salaam, Muleba, Karagwe, Kasulu Kigoma, Mara, Shinyanga na Songea.

“Takwimu kutoka Mara zinaonyesha kuwa wajane 55 walinyang’anywa ardhi zao baada ya waume zao kufariki, 23 walipewa mirathi kidogo, wajane 41 walifukuzwa baada ya waume zao kufariki kwa maambukizi ya VVU. Takwimu hizi ambazo ni za kuanzia Januari mpaka Julai 2012, pia zilijumuisha mashauri 174 kutoka Kitengo cha Wasaidizi wa Sheria, kilichopo Songea, yanayohusu wajane kunyimwa haki zao,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka Serikali kufanya marekebisho ya sheria za mirathi kwa kuwa mfumo dume uliopo unabagua na kukandamiza wanawake na kuchangia ukandamizaji wa kiuchumi.

“Vile vile sheria hizi zinakinzana na sheria mama ambayo ipo katika Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 12, 13 na 24 pamoja na mikataba mbalimbali ya Kimataifa, ambayo serikali yetu imeridhia. Mfumo huo wa mirathi unakiuka haki ya msingi ya usawa, umiliki wa mali na kuwa na maisha bora, familia na kutweza utu wa mwanamke, hususani wajane,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake na Ustawi wa Mtoto (TWCWC), Edda Mariki, alitoa wito kwa jamii kuondokana na mila potofu dhidi ya wajane na kuwatendea haki badala ya kuwanyanyasa.

“Mashemeji waache kubaka wajane kwa kutumia mfumo wa kurithi wajane, aidha jamii iondokane na dhana ya kuona wajane ni wachawi na wengine kusababisha kupigwa na kuuawa,” alisema.

Alizitaka taasisi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania ili kuondokana na mila potofu kwa ustawi wa jamii, kwani hicho ndiyo chanzo.



0 comments:

Post a Comment