Friday, August 31, 2012

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ilifanya kikao na wasafirishaji na kuweka mikakati ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe katika Mkutano wa Nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2012 uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, alipotangaza kukataza tabia ya abiria ya kushuka maporini na kujisaidia ‘kuchimba dawa’ ifikapo leo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye tangazo la SUMATRA kwa vyombo vya habari, itawalazimu abiria kuwa na kiasi cha fedha cha ziada kwa ajili ya kulipia huduma ya maliwato. Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema lolote kuhusu watoto na wale ambao wana matatizo ya kupata haja ndogo kila baada ya muda mfupi.

Kwa mujibu wa tangazo la SUMATRA vituo vilivyoainishwa katika barabara kuu tano ni:
Dar es Salaam - Mbeya

Vituo vilivyoainishwa ni mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa na Njombe. Vituo hivyo ni Ruvu iliko hoteli inayotoa huduma hiyo bure, Chalinze kuna hoteli inahudumia kwa Sh 200; stendi kuu ya mabasi ya Msamvu huduma inatolewa kwa Sh 200 na Ruaha Mbuyuni Hoteli ya Al Jazeera inatoa huduma bure. Kitonga, Hoteli ya Confort inahudumia bure, stendi ya Ipogoro malipo ni kati ya Sh 100 na 200, Mafinga abiria watalazimika kulipia kiasi kama hicho na Makambako malipo yatakuwa kati ya Sh 200 na 300.

Dar es Salaam - Mwanza

Magari yanapitia mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga, ‘dawa itachimbwa’ Msamvu, Gairo kuna hoteli ambayo inahudumia bure, Badueli umbali wa kilometa tatu kutoka Dodoma mjini pia huduma ni ya bure. Singida mjini iliko stendi ya mabasi huduma hiyo pia itapatikana kwa malipo ya Sh 200, kituo cha mabasi Nzega mjini huduma italipiwa Sh 200 na katika stendi kuu mjini Tabora malipo ni Sh 200 pia. Katika stendi kuu ya mabasi Shinyanga mjini, huduma hiyo italipiwa Sh 200 na kwa waendao Kagera kupitia Kahama huduma itapatikana stendi kuu ya mabasi kwa kati ya Sh 200 na 300 huku Mwanza mjini katika stendi kuu ya mabasi pia huduma italipiwa Sh 200. Kwa waendao Kagera baada ya kutoka Kahama, huduma zitapatikana Ushirombo kwa Sh 100 na Sh 500 ambapo pia watapata fursa ya kuoga, Chato Sh 200, Muleba Sh 200 na Bukoba Sh 200. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa abiria watokao Kigoma kabla ya kufika Kahama watahudumiwa Kasulu kwa Sh 200, Kibondo kwa Sh 200 na Runzewe kwa Sh 200 pia.
Dar es Salaam - Tanga

Abiria watahudumiwa katika kituo cha mizani Msata bila gharama yoyote sawa na Segera.
Dar es Salaam - Moshi, Arusha na Manyara

Huduma zitapatikana Korogwe katika hoteli mbili bila malipo na Mombo ambako pia kuna hoteli isiyotoza malipo. Lakini Same, Mwanga, Himo, Moshi Mjini na Boma Ng’ombe, huduma itatolewa kwa Sh 200 na Arusha huduma itapatikana stendi kuu kwa Sh 200 sawa na ilivyo kwa Manyara.
Dar es Salaam - Lindi-Mtwara

Eneo la Nangurukuru kuna hoteli iitwayo StarCom ambayo itatoa huduma bila malipo, ambapo Lindi huduma hiyo haitalipiwa huku Mtwara ikilipiwa Sh 200 ingawa haitoshelezi mahitaji.
 
 
MAHAKAMA ya Rufani imepanga kusikiliza shauri la umri wa msanii wa filamu Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, Septemba 17 mwaka huu mbele ya jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo ambao ni Jaji Bernard Luanda, Jaji January Msoffe na Jaji Katherine Oriyo.

Rufaa hiyo ni ile iliyowasilishwa na mawakili wa upande wa mashitaka wakiomba kupitiwa uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na Jaji Dkt. Fauz Twaibu ambao alikubali maombi ya Lulu kusikiliza maombi ya utata wa umri wake.

Siku ambayo Mahakama Kuu ilitarajia kuanza kusikiliza maombi ya uchunguzi wa umri wa Lulu, upande wa mashtaka ulidai kuwa umewasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya marejeo ya uamuzi huo, jambo ambalo lilifanya Mahakama Kuu iahirishe uchunguzi huo kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani. 

0 comments:

Post a Comment