Tuesday, July 3, 2012


Meneja Masoko wa Kampuni ya Selcom, Juma Mgora akiwaonesha wanahabari moja ya simu ya kutolea huduma ya kukata tiketi ya mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani kupitia huduma ya Selcom PayPoint. Huduma hiyo ambayo itapatikana katika maduka na sehemu mbalimbali nchini pia itawawezesha wananchi kununua tiketi kupitia mtandao wa Kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom. (picha via Ziro & Tina blog)
Kampuni ya Mobile Ticketing Ltd kwa kushirikiana na Selcom PAYPOINT na makampuni ya mabasi imezindua huduma mpya ijulikanayo "ticket popote na paypoint" itakayotumika kukatia ticketi za mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani kupitia mashine za selcom paypoint.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya PAYPOINT Bw.Costantine Kumalija alisema huduma hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa usumbufu kwa kuwa itamrahisishia mteja kupata tiketi kwa urahisi bila kusumbuliwa na wapiga debe kama ilivyo hivi sasa
.

"Mteja anachotakiwa kufanya ni kutembelea sehemu yoyote yenye selcom Paypoint na kutoa taarifa ya safari yake, ambapo taarifa hizo ni pamoja na basi analolihitaji,tarehe ya kusafiri, mahali anaposhuka ndani ya mashine na kisha kupata ticketi," alisema Bw. Kumalija.

Bw.Kumalija alisema mpaka sasa kampuni 10 za mabasi ambazo zinafanya safari za ndani na nje ya nchi zimethibitisha kujiunga katika mfumo huo.

"Huduma hii kwa sasa ni kwa Mkoa wa Dar es Salaam na mchakato utaendelea ili kupanua huduma hii kufikia mikoa yote nchini," alisema Bw. Kumalija.

Awali Bw.Kumalija alisema mashine hiyo hutumika kulipia huduma nyingine mbalimbali ndani ya jamii. 

0 comments:

Post a Comment