Monday, May 28, 2012

KATIKA gazeti la Tanzania Daima toleo la jana, kulikuwamo na habari inayoelezea mwanafunzi kujifungua mtoto na kisha kumtupa kwenye choo cha shule.
Habari hiyo inaeleza kuwa mwanafunzi aliyefanya tukio hilo ni wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Rwiche, Rehema Issa na kwamba tukio hilo liligunduliwa na baadhi ya wanafunzi walioingia chooni na kusikia sauti ya kichanga.
Imeelezwa kuwa katika kipindi chote cha ujauzito, wazazi na walimu hawakumgundua kwa kuwa alikuwa akihudhuria masomo yake kama kawaida.
Tunalaani tukio la mwanafunzi kufanya ukatili wa hali ya juu kiasi hiki cha kuondoa uhai wa kiumbe kisicho na hatia.
Tukio hili ni baya zaidi hasa ikizingatiwa limefanywa na mwanafunzi ambaye anatakiwa kuwa mzazi bora siku zijazo. Hili lisipokemewa ni hatari kwa taifa letu.
Lakini tujiulize inakuwaje mpaka mwanafunzi anapata ujauzito? Pamoja na tukio hilo, tunaamini kuwa suala hilo linachangiwa na watoto wetu kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi.
Siku hizi malezi kwa watoto wetu yamepungua kwa kiasi kikubwa, hivyo kuchangia hali kama hiyo na baadhi ya wazazi kuacha jukumu hilo kwa walimu pekee.
Wazazi na walezi wanapaswa kurudi katika mstari na kulea watoto wetu katika maadili yanayotakiwa, ili siku zijazo nao waweze kuwa walezi na wazazi bora. Jukumu la malezi wasiachiwe walimu peke yao.
Pia ili kukabiliana na hali hii na kuwaepusha watoto wetu wa kike kuingia katika makundi maovu na hatimaye kujikuta wakipata ujazito ni vema serikali ikaweka mkazo katika suala la ujenzi wa mabweni.
Watoto wengi wa kike wanakabiliana na changamoto mbalimbali hasa wanaposoma shule ambazo pia zipo mbali na majumbani kwao, hivyo kulazimika kupanga vyumba mitaani. Hali hii kwa kiasi kikubwa inaruhusu wanafunzi hawa kujiingiza katika matendo maovu.
Watoto wa kike wanaposoma, hasa wanapokuwa katika mazingira ya bweni wanakuwa salama, hata mitihani yao wanafanya vizuri, kwani wanakuwa wametulia.
Suala la ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi wa kike lisipozingatiwa linaweza kurudisha nyuma juhudi za kumwinua mtoto wa kike kielimu. Serikali ijengwe mabweni kwa wanafunzi wa kike ili iwanusuru na vishawishi mbalimbali na hatimaye kufanikiwa kumwinua kielimu.

0 comments:

Post a Comment