Monday, May 28, 2012

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeamua nafasi za uongozi wa Yanga zilizoachwa wazi baada ya kujiuzulu viongozi mbalimbali wa klabu hiyo zijazwe Julai 15
mwaka huu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Deogratius Lyato ilieleza kuwa kutokana na mazingira hayo Kamati ya Uchaguzi ya
Yanga ianze mchakato huo wa uchaguzi kuanzia Juni mosi mwaka huu kulingana na Katiba
ya Yanga ibara ya 28 inayozungumzia nafasi iliyo wazi.

Lyato alisema Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyokutana jana iliamua mchakato huo uanze na uzingatie kikamilifu kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF na kwamba nafasi zilizo wazi zitajazwa Julai 15 katika Mkutano wa uchaguzi ambao mahali patapangwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kwa kushirikiana na Sekretarieti ya klabu hiyo.

Alisema Mkutano wa Uchaguzi utakuwa na ajenda moja tu ya uchaguzi kujaza nafasi zilizo wazi za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa kuchaguliwa na kwamba Kamati ya Uchaguzi ya Yanga iandae na isimamie shughuli za uchaguzi kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Yanga kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF na Katiba ya Yanga ibara ya 45(1) na (2).

Alisema hatua ya kuiagiza Yanga iitishe uchaguzi inatokana na kupata ufafanuzi kutoka kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana juzi.

Kamati hiyo ya Sheria iliombwa kutoa mwongozo wa nini kifanyike ndani ya Yanga baada ya wajumbe wake kadhaa kujiuzulu, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ilikuwa imeomba mwongozo huo TFF.

Akitangaza muongozo huo kama walivyoombwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga mapema jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi kwa Wachezaji ya TFF, Alex
Mgongolwa alisema kujiuzulu kwa wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo
kunawaondolea nguvu ya kimaamuzi wajumbe waliosalia kwa mujibu wa Katiba ya klabu
hiyo na kwamba kwa sasa shughuli za uongozi wa klabu zitafanywa na Sekretarieti ya klabu hiyo mpaka Mkutano Mkuu utakapoitishwa kujaza nafasi hizo.

Alisema Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu hiyo ambao hawajatangaza kujiuzulu ni pamoja na Salumu Rupia, Titto Ossoro, Sarah Ramadhani na Mohamedi Bhinda hawana nguvu za kimaamuzi na hivyo hawawezi kuongoza klabu hiyo mpaka mkutano mkuu utakapofanyika.

Mgongolwa alisema ili wajumbe hao wawe na nguvu ya kimaamuzi kwa mujibu wa Katiba ya Yanga ni kwa idadi yao inapaswa kuwa asilimia 50 na kwa sababu wajumbe waliojiuzulu ni wengi kuliko waliobakia, wanakosa nguvu ya kimaamuzi.

Alisema hata wajumbe watatu walioteuliwa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo kabla hajajiuzulu ni
batili kwa mujibu wa Katiba ya Yanga kwani uteuzi huo unafanywa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambapo idadi yao tayari ilikuwa haikidhi kufanya uteuzi huo kwani wajumbe waliojiuzulu walikuwa wengi.

Wajumbe kadhaa wa Kamati ya Utendaji ya Yanga walitangaza kujiuzulu kuongoza klabu hiyo hivi karibuni akiwemo Mwenyekiti Lloyd Nchunga kutokana na sababu mbalimbali.

0 comments:

Post a Comment