Monday, May 28, 2012

•  Mbowe akemea wanaoeneza udini, ukabila 
LICHA ya Jeshi la Polisi kutoa amri wananchi na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wasiandamane kuelekea katika viwanja vya Jangwani jana kuhudhuria mkutano wa hadha ra wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), viwanja hivyo vilifurika umati wa wananchi kwa kiasi kikubwa huku utulivu ukitawala.
Umati huo ulianza kuingia uwanjani hapo majra ya asubuhi huku kukiwa na vibanda 16 vilivyokuwa vikisimamiwa na vijana kutoka vyuo vikuu ambao ni wanachama wa CHADEMA kwa ajili ya watu kujiunga na chama hicho na wengine kurudisha kadi za vyama vingine.
Kutokana na zoezi hilo la kurudisha kadi na kupata wanachama wapya, jumla ya watu 3,124 walijiunga na CHADEMA jana katika viwanja hivyo akiwamo mzee Raphael Koimere, aliyekuwa kada maarufu wa CCM.
Majira ya saa 9:20 mchana msafara wa wapanda pikipiki zaidi ya 200 uliwasili uwanjani hapo huku wengine wakiwa na mabango ya kuhamasisha na kuelezea kasoro za kufanyiwa kazi.
Miongoni mwa mabango hayo yaliyosema: ‘Jimbo la Ilala linawaangusha Watanzania katika mageuzi ya kweli kwa kuwa mipango yote ya ufisadi huanzia hapo na kutekelezwa katika ofisi zilizo katika wilaya hiyo’.
Mabango mengine yalisomeka: ‘Shibuda ulikuja CHADEMA kwa mkopo na sasa hatukutaki, rudi ulikotoka’, ‘Tunamuomba CAG akague hesabu katika ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala na jingine likiwatahadharisha CCM muda wao wa kuwa madarakani umekwisha waanze mazoezi ya kuwa wapinzani wa kudumu, kama si kupotea katika ramani ya kisiasa ya Tanzania.
Majira ya saa 9:30 mchana viongozi mbalimbali wa CHADEMA walianza kuwasili uwanjani hapo wakiwamo wabunge wa chama hicho wakiongozwa na John Mnyika, Mbunge wa Ubungo.
Baadhi ya viongozi waliowasili uwanjani hapo ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema, wanasheria maarufu nchini Mabere Marando, Profesa Abdallah Safari na Edson Mbogoro, huku wanachama waliojiunga na CHADEMA hivi karibuni kutoka mkoani Arusha James ole Milya na Ally Bananga wakiwa ni miongoni mwa watu waliokaa meza kuu.
Ilipofika saa 9:54 Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA aliwasili uwanjani hapo huku akifuatiwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, hali iliyoamsha shangwe kubwa kutoka kwa wananchi waliokusanyika uwanjani hapo.
Baada ya kuketi viongozi hao, mkutano ulifunguliwa kwa dua kutoka kwa viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo na kisha baadhi ya viongozi wakaanza kuzungmza huku viongozi watatu wakiwa ndio wasemaji wakuu katika mkutano huo, ambao ni Freeman Mbowe, Dk. Willibrod Slaa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu.
Mbowe akemea udini, ukabila
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, akihimiza kuwekwa mbele kwa masilahi ya taifa badala ya vikundi vya watu wachache.
Alisema ni wakati wa Watanzania kutambua haki zao na kuwaonya viongozi wa serikali ili kuacha mtindo wa kuligawa taifa kwa dhana ya udini, ukabila na ukanda.
“Ninaliongea hili kwa kuwa kuna watu sasa hawajui hatima yao na wamebaki katika kukumbatia suala zima la udini, ukanda na ukabila kuligawa taifa, mimi ninawaambia Watanzania, sisi CHADEMA kama chama kinachojipanga kuchukua dola tunamhitaji kila mmoja mwenye sifa ya Utanzania, pasipo kujua dini yake, kabila lake, wala anatoka ni eneo gani la nchi,” alisema Mbowe.
Akizungumzia utata wa kauli mbalimbali za baadhi ya wanachama ndani ya CHADEMA, Mbowe alisema hawataweza kumvumilia mtu yeyote mwenye dhamira ya kuvuruga umoja ndani ya chama hicho kwa masilahi yake na kundi lake.
Akizungumza kwa hisia kali, pasipo kutaja jina la mtu, licha ya maongezi hayo kuonekana yakimlenga Mbunge John Shibuda, Mbowe alisema: “Hatua ya kuifikisha CHADEMA hapo ilipo ilianza miaka 20 iliyopita na kwamba akitokea mtu wa kuivuruga, taratibu za kumuwajibisha zitafuatwa.
“Kauli ya chama ni makini, hakitayumbishwa na propaganda za mapandikizi na hata wasio na nia nzuri na nchi. Tutafanya maamuzi mazuri kwa njia ya haki na tusimfikirie mpuuzi mmoja kutuharibu, yeyote atakayechezea moto utamchoma,” alisema Mbowe.
Akilizungumzia Jeshi la Polisi na hali ya amani, Mbowe alisema jeshi hilo liache kutumika kwa masilahi ya CCM na badala yake lifanye kazi kwa maadili ya jeshi hilo.
Alisema licha ya uchokozi unaofanywa mara kwa mara na viongozi wa CCM kwa kulitumia Jeshi la Polisi kuvuruga amani ya nchi, chama hicho kitakuwa cha mwisho kuelekea katika uvunjifu huo wa amani.
“Ndugu zangu Polisi watambue njia ya kuelekea amani ya kudumu ni kuheshimu demokrasia, wasitumie ofisi zao kunyanyasa, kuwatesa na kuwapiga wananchi, hali hii ikome kuanzia sasa,” alisema Mbowe.
Akitumia nukuu ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mbowe alisema serikali yoyote inayotumia nguvu na majeshi kwa ajili ya kuulinda utawala wa kidhalimu, ndiyo inayowafundisha raia wa nchi hiyo kutumia nguvu kuwapinga.
Alisema harakati za mabadiliko yanayofanywa sasa na chama hicho kupitia kaulimbiu yao ya (M4C) ni maandalizi ya kushika dola mwaka 2015 na kuwataka wananchi kushiriki kwa kila namna katika harakati hizo.
Dk. Slaa atoa mikoba
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema taifa lipo katika hali ngumu ikiwamo, mfumuko wa bei, unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha kunakochangiwa na na matumizi mabaya ya serikali.
Alisema jambo jingine linalochangia hali ngumu ya maisha ni pamoja na rais kuwa na mamlaka makubwa ya uteuzi pasipo kushauriana na mtu, hali inayomfanya aonekane kama mungu mtu.
“Serikali ina matumizi makubwa kiasi cha kupelekea taifa katika umasikini na hakuna mwananchi wala wabunge kuhoji na akapatiwa jibu, kwani ukihoji unaambiwa mamlaka ya rais hayahojiwi, si wewe na mimi wala wabunge na mawaziri wake,” alisema Dk. Slaa.
Akielezea zaidi, Dk. Slaa alisema, rais amekuwa akigawa vyeo kwa kutumia mamlaka yake vibaya katika nafasi mbalimbali ikiwamo kwa waliompa hifadhi, marafiki, ndugu na wale waliomsaidia kuingia Ikulu huku akihoji ukubwa wa baraza la mawaziri.
Alitolea mfano Uingereza kuwa waziri mkuu, ana mamlaka ya kuchagua mawaziri 20 tu, na akizidisha zaidi ya hapo atalazimika kumlipa kwa hela yake ya mfukoni na si kodi za wananchi.
Aidha, aliwataka wabunge wa chama hicho kutetea masilahi ya wananchi watakapoingia katika Bunge la bajeti litakaloanza Juni 12 na kwamba kama watazomewa na watu wasitake wananchi watetewe, litakuwa ni jukumu la wananchi kuwazomea wakirudi katika majimbo yao.
Lissu
Ilipofika zamu ya Tundu Lissu kuzungumza, wananchi walimlazimisha avue kofia yake aina ya ‘Pama’ ili waweze kumuona na alipofanya hivyo wakalipuka kwa shangwe kwa kuimba ‘jembe, jembe, jembe’ hadi Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) aliposimama na kuwaomba watulie.
Akihutubia mkutano huo, Lissu alijikita katika suala zima la wananchi kufahamu umuhimu wa Katiba na kuweza kutoa maoni yatakayohitimisha utawala wa kichifu nchini.
Alisema licha ya suala hilo kupigiwa kelele na watu mbalimbali serikali ya CCM imekubali mchakato huo kwa hila huku ikitunga sheria hovyo ya kuupeleka bungeni, wakitumia wabunge waliopo kwa kuamini wapo wengi na hivyo watapitisha kwa masilahi yao na chama chao.
Aliongeza kuwa hata hatua ya kuzuia masuala ya muungano yasijadiliwe ni njia moja wapo ya matumizi mabaya ya madaraka, kwa kuwa suala hilo haliwezi kutenganishwa na Watanzania.
Aliwataka wananchi kuhakikisha tume ya maoni ya Katiba itakapowafikia wawe na ujasiri wa kuuliza nafasi ya Tanganyika katika Serikali ya Muungano kwa kile alichosema mpaka sasa baada ya Zanzibar kurekebisha katiba yao Tanzania haijulikani ina nchi ngapi, wakuu wa nchi wangapi na maamiri jeshi wangapi.
Alisisitiza Watanzania wasisite kutaka kuwepo kura ya maoni kuangalia kama yaliyofanyika Zanzibar ni sawa kwa ustawi mzima wa muungano.
Aidha, Lissu alisema kwa utaratibu wa sasa bunge litakapokaa kama bunge la katiba ni wazi CCM na washirika wake watakuwa zaidi ya 400 na kutaka suala hilo lihusishe watu wa kada mbali mbali pasipo kujali vyama vyao kwa ajili ya kupig kura hiyo katika bunge la katiba.
Akizungumzia mamlaka ya uteuzi, Lissu alisema yanatumika vibaya kwa kuwa katika Bunge tayari kuna theluthi moja ya wabunge ambao kazi yao ni kugonga meza kwa ajili ya kupongeza kila kitu kwa kuwa hawawajibiki kwa wanchi.
Lema
Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini Godbles Lema, akizungumza katika mkutano huo alisema yupo kwenye ‘honeymoon’ na kwamba wakati wowote atarudi kazini kuwatumikia wananchi wa Arusha.
Alisema kwa hali ilivyo sasa siyo lazima kufika mwaka 2015 kama viongozi wa serikali wataendelea kufanya ubadhirifu unaosikika kila kunapokucha.
Alibainisha hali hiyo ya ubadhirifu ndiyo inayosababisha kuwepo na machangudoa, majambazi na hata omba omba licha ya kuwa ni nchi tajiri na inayoshika nafasi ya tatu kwa kuwa na almasi zilizo bora kidunia.
Naye Mbunge wa Ilemela, Ezekia Wenje, alisema nchi ya Tanzania ni kubwa kuliko Mtanzania yeyote aliyeko CHADEMA, CCM na hata vyama vingine na kwamba kila mmoja ana wajibu wa kutunza amani.
Kwa upande wake, Halima Mdee, alisema umati wa watu uliojitokeza katika mkutano huo unaashiria kuwa Dar es Salaam, hakukaliki kwa upande wa CCM, na kuondoa dhana waliyokuwa wakijivunia CCM kuwa Dar ni ngome yao.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO LA JUMAPILI YA LEO HII

0 comments:

Post a Comment