Monday, May 7, 2012Leon Bahati
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amesema Rais Jakaya Kikwete hajavunja kipengele chochote cha sheria kuwateua wabunge na kuwapa Uwaziri kabla hawajaapishwa kuwa wabunge.

Kauli hiyo ya spika imekuja kipindi ambacho uamuzi wa Rais kuteua baadhi ya wabunge na kuwapa uwaziri, ukiwa umeibua mjadala huku baadhi ya watu akiwamo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe naye akisema mkuu huyo wa nchi amevunja katiba kwani waliteuliwa bila kiapo cha Bunge.

Lakini, akifafanua kuhusu utata huo, Makinda alisema alichofanya Rais Kikwete ni sahihi kwa sababu aliowateua amewapa uwaziri ili wawajibike katika serikali yake.

Kwa mujibu wa Makinda, wateule hao wakishaapishwa kuwa mawaziri, wana haki ya kuanza kufanya kazi za uwaziri kwenye wizara walizopangiwa.

Mawaziri wote walioteuliwa kushika nafasi mpya katika baraza la mawaziri wanatarajiwa kuapishwa leo Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Makinda alisema mawaziri hao hawataweza kuhudhuria shughuli za bunge hadi hapo watakapokula kiapo cha utii kwa mhimili huo wa dola wa kutunga Sheria na Kuisimamia Serikali.

"Kitakachowafunga ni kwamba hawawezi kuingia Bungeni bila kuapishwa," alisema Makinda.

Wabunge wapya walioteuliwa na kupewa uwaziri ni Profesa Sospeter Muhongo aliyepewa Wizara ya Nishati na Madini na manaibu wawili wa Wizara ya Fedha; Janeth Mbene na Saada Mkuya Salum.

Mawaziri hao ni miongoni mwa wabunge wanne walioteuliwa kwa mujibu wa mamlaka ya rais aliyopewa na Katiba ambapo amepewa nafasi 10 za uteuzi.

Mwingine aliyeteuliwa kuwa mbunge ni Mwenyekiti wa chama cha siasa cha upinzani cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

Kuhusu ni lini wabunge hao wapya wataaapishwa, Spika Makinda alisema kwa mujibu wa kanuni za bunge wataapishwa kabla ya kuanza vikao vya bunge lijalo la Bajeti litakalofanyika mjini Dodoma Juni kuanzia 12, mwaka huu.

"Kanuni za bunge ziko wazi kwamba wabunge wapya wataapishwa kwenye kikao kinachofuata cha Bunge," alisema Makinda.

Walichosema Mbowe, Kafulila
Mbowe akihutubia mamia ya wafuasi wa Chadema katika viwanja vya Unga Limited, juzi alitumia fursa hiyo kuponda uteuzi wa Baraza la Mawaziri akisema Rais Kikwete amevunja katiba kwa kuwateua watu ambao hawajaapishwa kuwa wabunge kushika nafasi za uwaziri.

Licha ya kuvunja katiba kwenye uteuzi, Rais pia amekiuka kwa kuwateua
Wazanzibari kwenye wizara ambazo siyo za Muungano kama Afya aliyokabidhiwa na Dk Husein Mwinyi.

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema Rais Kikwete amekiuka katiba kwa kuteua wabunge wateule kuwa mawaziri.

Kafulila alisema katiba inamuelekeza Rais kuteua mawaziri miongoni mwa wabunge na mbunge hutambuliwa kwenye nafasi hiyo baada ya kuapishwa.

“Nashangaa hawa hawajawa wabunge lakini amewateua kuwa mawaziri,” alisema Kafulila ambaye amekuwa akivutana na uongozi wa chama chake cha NCCR mahakamani kutetea uanachama wake.

Mmoja wanasheria
Mmoja wa wanasheria maarufu nchini aliyebobea katika masuala ya Katiba ambaye aliomba jina lake kutotajwa gazetini, alisema Mbunge aliyeteuliwa  anaweza kuteuliwa kuwa waziri moja kuwa waziri bila hata kula kiapo cha utii cha ubunge.

Gwiji huyo wa sheria, alisema kiapo anachokula mbunge ni kwa ajili ya shughuli za Bunge pekee lakini, mbunge akiteuliwa anaweza kufanya shughuli zozote zile nje ya bunge ikiwamo za uwaziri kama ameteuliwa kushika wadhifa huo.

0 comments:

Post a Comment