Monday, May 7, 2012

Peter Saramba, Arusha
WAKILI Method Kimomogoro amekamilisha na kuwasilisha mahakamani rufaa ya kupinga hukumu iliyomvua ubunge wa jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema huku akiainisha hoja 18 za kupinga kukata rufaa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kimahakama zilizopatika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, rufaa hiyo iliwasilishwa Ijumaa ya Mei 4, mwaka huu tayari kwa ajili ya kuwasilishwa kwa msajili wa Mahakama ya rufaa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusajiliwa.

Akizungumza ofisini kwake jana, Wakili Kimomogoro alithibitisha kukamilisha na kuwasilisha rufaa hiyo mahakamani tayari kwa ajili ya kupangiwa jopo la majaji wa kuisikiliza.

Pamoja na hoja za rufaa, kitabu hicho cha rufaa chenye kurasa 985 ina mwenendo mzima wa shauri, vielelezo na viambatanisho vyote vilivyowasilishwa Mahakama Kuu.

“Kimsingi ni rai yangu kuwa mtukufu Jaji Rwakibarila (Gabriel) hakutolea uamuzi mambo na hoja za msingi zinazofanya hukumu yake kukosa hadhi kisheria, kuitwa hukumu, hayo ni miongoni mwa hoja za msingi nilizoanisha kwenye rufaa niyowasilisha mahakamani juzi,” alisema Wakili Kimomogoro.

Kwa mujibu wa hati ya rufaa hiyo, hoja ya kwanza hadi nne zinapinga uamuzi wa Jaji Aloyce Mjulizi aliyesikiliza shauri hilo katika hatua za awali kwa kutupa pingamizi za awali zilizowasilishwa na upande wa utetezi kwenye kesi ya madai namba 13 iliyofunguliwa na wapiga kura watatu waliopinga ushindi wa Lema.

Miongoni mwahoja hizo ni kuwa wadai, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo hawakuwa na haki kisheria kufungua shauri hilo kwa sababu hakuna haki yao iliyovunjwa kisheria kama wapiga kura.

Wakili Kimomogoro aliyemwakilisha Lema na mawakili wa Serikali, Timon Vitalis na Juma Masanja walidai aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Batilda Burian ndiye alikuwa na haki kisheria
kulalamikia ushindi na maneno ya kashfa yanayodaiwa kutolewa dhidi
yake na Lema.

Hoja ya tano hadi 18 zinapinga hukumu ya Jaji Rwakibarila ambapo katika suala la hukumu yake kukosa hadhi kisheria, wakili Kimomogoro anadai hakutolea maamuzi athari za wadai kushindwa kuwasilisha mahakamani CD zinazomwonyesha Lema akitoa maneno ya kashfa na udhalilishaji walizodai kuwa nazo katika hati yao ya madai.

Kimomogoro anadai Jaji alikosea kwa kutotumia hata kesi moja kama rejea kati ya kesi kadhaa zilizotajwa na mawakili wa pande zote mbili za wadai na wadaiwa.

Jaji Rwakibarila ambaye ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga pia anadaiwa kukosea kisheria kwa kukubali na kuegemea ushahidi wa mdomo pekee katika hukumu yake bila kuwepo ushahidi wa mazingira, Video wala maandishi kuunga mkono ushahidi wa mdomo.

Mrufani pia anadai Jaji alikosea kwa kutumia viwango na vigezo tofauti kwa mashahidi wa upande wa wadai na utetezi kwa kukataa ushahidi wa Leman na mashahidi wake kwa madai kuwa walikuwa na maslahi kwa sababu ni wanachama na viongozi wa Chadema lakini akakubali ushahidi wa wanachama na viongozi wa CCM kutengua matokeo.

Hoja nyingine ni kuwa hata kama Lema angetiwa hatiani kwa madai yaliwasilishwa mahakamani, bado Jaji hakustahili kutumia kifungu cha 114 cha sheria za uchaguzi kuripoti uamuzi wake kwa Mkurugenzi wa uchaguzi kwani makosa hayo hayahusiani na vitendo vya rushwa wala jinai ambavyo humzua aliyehukumiwa kupiga kura wala kugombea uongozi
kwa miaka mitano.
 


0 comments:

Post a Comment