Tuesday, May 29, 2012

MSANII mkongwe wa Hip Hop nchini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), amepania kukonga nyoyo za mashabiki wake watakaohudhuria tamasha la Usiku wa Sugu, huku akiahidi kutoa sh milioni 2 kati ya tatu atakazolipwa kwa shoo hiyo kusaidia Mfuko wa Elimu Jimbo la Mbeya.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, katika mkutano wa kuutambulisha ‘Usiku wa Sugu’ utakaofanyika Jumapili Juni 3 kwenye Ukumbi wa kisasa wa burudani jijini, Dar Live, ulioko Mbagala Zakheem, Sugu alisema kwa kuwa ni mara ya kwanza kwake kutumbuiza hapo, atahakikisha anaacha gumzo miongoni mwa watakajitokeza.

“Nilianzia maisha Mbagala na nilitokea huko kwenda kumbi za starehe usiku katikati ya jiji (Posta). Jumapili narejea tena huko nikiahidi kufunika kama kawaida ya shoo za Vinega, huku nikipanga kutumia pato binafsi kusaidia Mfuko wa Elimu jimboni kama nilivyoahidi wakati nikiomba kura,” alifichua Sugu.

Akizungumzia usiku huo, Meneja Matukio wa Dar Live maarufu kama Uwanja wa Taifa wa Burudani, Abdallah Mrisho, aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi, kushuhudia vitu vikali kutoka kwa Sugu na washirika wake.
Aliongeza kuwa katika usiku huo, Sugu atasindikizwa na wasanii Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Juma Kassim ‘Sir Nature’, Danny Msimamo na Maujanja Supplies, huku Sugu mwenyewe akiongeza kuwa mkali wa aina hiyo ya muziki Fred Maliki ‘Mkoloni’ atakuwapo ukumbini.

CHANZO CHA HABARI: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment