Thursday, December 12, 2013

WanaBAHARI,

Salaam. Ni matumaini yangu kwamba mawazo yangu kwa ufupi yatasaidia kuanzisha mjadala kuhusu wapi tunapokosea kama nchi kiuongozi.

Nchi yetu inakwama sehemu nyingi, kiuchumi, kijamii, kisiasa etc. Tangu kuchaguliwa kwangu kama Diwani kuna jambo ambalo limejidhihirisha. Nimekuwa muumini wa ujenzi wa uongozi thabiti ngazi za chini badala ya kuangalia uongozi wa juu.

Siku zote naamini bila kurudi kwenye ngazi za chini hatuwezi kuendelea na kelele zetu zitakuwa kazi bure.

Viongozi wa kuchaguliwa ni Mwenyekiti wa Kitongoji (kwa mijini Mwenyekiti wa Mtaa), Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani, Mbunge na Raisi. Hawa wanatakiwa wafanye kazi kama cheni (chain) bila kujali itikadi zao.

Lakini uwezo wa hao wote ni tatizo. Mfano halisi ni kama ifuatavyo. Mwenyekiti wa Kitongoji anatakiwa akae na wananchi aandae mpango wa maendeleo. Wengi hawawezi.

Kwenye kata yangu hakuna Mwenyekiti wa Kitongoji hata mmoja amefika kidato cha nne. Wengi kuandika ni shughuli. Asilimia 80 ya Wenyeviti hao hawajafika Dar es Salaam zaidi ya miaka 10. Hawana access na TV kuona kwingineko duniani nini kinatokea. Mawazo yao kuhusu maendeleo ni maisha wanayoishi.

Anayefuata kupokea Mpango wa Maendeleo ni Mwenyekiti wa Kijiji. Hawa wote matatizo ni yale yale ya Wenyeviti wa Vitongoji.

Diwani ni mimi. Angalau ninapata nafasi kusoma na kusikia wanaBAHARI wanasema nini, naangalia TV kuona wenzetu wanafanya nini. Nina elimu (sio kigezo kikuu) inayonisaidia kuchambua baadhi ya mambo au kutafuta msaada.

Mbunge ni waziri. Ni PHD holder.

Raisi ni Degree holder. Ni Raisi.

Tukianzia juu kwenda chini ni wazi mawazo na utekelezaji unakwama mara baada ya Diwani. Mawazo na wanachoelewa walio juu ni tofauti na wale wa chini. Matokeo yake ni siasa na ubabaishaji. Mbaya zaidi ni pale ambapo walio juu wanakosa mawazo sahihi.

Serikali za Vijiji zimetelekezwa. Utendaji wake ni mbovu sana. Viongozi hawana uwezo na wanaongoza kwa uzoefu. Hawana mawazo endelevu. Hawana vitendea kazi. Mazingira yao ya kazi ni duni sana.

Mbunge anaenda na LandCruiser kumtembelea Mwenyekiti na Diwani ambaye hana hata baiskeli. Mwenyekiti na Diwani ambaye anafanya kazi kwa kujitolea!

Serikali za vijiji hazitunzi kumbukumbu za fedha. Miradi inatekelezwa hovyo hovyo. Mara ya mwisho Kijiji kimoja kimekaguliwa miaka mitatu iliyopita.

Hayo ni baadhi, naamini mnayajua mengine.

Wengi wetu tunatamani na kupigania nafasi za juu. Ubunge. Kuingia mjengoni. Kata, Vijiji na Vitongoji hakuna anayetaka. Hakuna maslahi wala sifa na heshima huko chini.

Vyama vya siasa na vyenyewe vinaendekeza mfumo huo huo. Wanachama wanaojiunga navyo wanataka nafasi za ubunge na kama ni uongozi ndani ya chama basi wilayani, mkoani na taifa.

Kuna unafiki wa hali ya juu katika uongozi wa nchi hii. Hakuna ukweli wala nia ya dhati ya kuleta maendeleo. Haiwezekani eti lengo ni kuiondoa CCM madarakani. Hili sio lengo. Ni nia. Lengo ni maendeleo kwa wananchi. Ni lazima tujenge vyama vyetu kuanzia kwenye kaya, mtaa, kitongoji na kijiji. CCM imeshindwa kufanya hivyo kwa miaka 50. Ndio maana wananchi wanataka mabadiliko.

Wito wangu kwa wanaJF wenye nia njema ni kufikiria upya vitongoji, vijiji na kata zetu. Wote wenye uwezo turudi huko. Sio kwa nia ya kuja kuwa wabunge bali kusaidia ukombozi wa mtanzania.

Halmashauri za miji na wilaya zimejaa viongozi wasio na uwezo ndio maana wanaiba na kutafuna fedha za wananchi.
Hakuna mpango wowote wa maana utakaojadiliwa na badala yake wanaweka maslahi yao mbele. Tukomeshe haya yote kwa kuingia kwenye nafasi za uongozi ngazi za chini. Vinginevyo maisha ya mtanzania yataendelea kuwa ya tabu daima.

Mungu tubariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment