Saturday, September 14, 2013


WAKATI viongozi mbalimbali wa CHADEMA wakiwasili mjini Dodoma kuungana na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, katika rufaa ya kupinga ubunge wake inayoanza kusikilizwa leo, mbunge huyo amekataa uamuzi CCM kutaka kuifuta kesi hiyo.

Juzi CCM kupitia kwa wakili wake, Godfrey Wasonga, iliwasilisha barua katika Mahakama ya Rufaa Dodoma na nakala kwa Lissu ikiomba mahakama hiyo kuifuta kesi hiyo.
 
  Kwa mujibu wa wakili huyo, sababu ya kuomba kufutwa kwa kesi hiyo ni walalamikaji wote kujitoa na kuapa mahakamani kuwa hawakuwa tayari kuendelea na kesi hiyo.
 
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema kuwa viongozi kadhaa wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, wajumbe wa Kamati Kuu na wabunge kadhaa wa chama hicho tayari walikuwa wamewasili mjini Dodoma.

Hata hivyo, akizungumzia kesi hiyo, Lissu alisema kuwa hatakubali ‘withdrawal’ isipokuwa anataka ‘dismiss with cost’.

Lissu alisema kuwa Wasonga atalazimishwa kulipa gharama kwa kuwa hati ya kiapo cha Selema ni ya mwezi Juni 25, mwaka huu, na kwamba kutaka kuiondoa siku mbili kabla ni uhuni.
 
Shabani Selema na Paskali Hallu ni wanachama wa CCM wakazi wa kijiji cha Makiungu, mkoani Singida, ambao walifungua kesi ya msingi ya kupinga ubunge wa Lissu.
 
Lakini baada ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kumtangaza Lissu kama mbunge halali, walikubaliana na hukumu hiyo ya Aprili 27, mwaka huu.
 
Mara kadhaa wananchi hao wamenukuriwa wakimlalamikia Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuwa anawashinikiza kuendelea na rufaa hiyo licha ya kwamba walishajitoa.
 
Akizungumza na gazeti hili juzi, Wasonga, ambaye alikuwa akiwatetea wanachama hao katika kesi hiyo, alisema kuwa baada ya kuwasiliana na wateja wake walimwambia hawakuwa tayari kuendelea na kesi hivyo.
 
“Ni kweli walalamikaji wote wamejitoa na mimi kama wakili sioni haja ya kuendelea; nitakuwa namwakilisha nani?
“Niliongea nao jana hakuna; mwenye nia ya kuendelea na kesi,” alisema.
 
Rufaa hiyo imepangiwa kusikilizwa katika Mahakama ya Rufani na Jopo la Majaji watatu, Salumu Massati, Engela Kileo na Natalia Kimaro.
 
Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa rufaa hiyo, mahakama ilitarajiwa kusikiliza pingamizi zilizotolewa na upande wa walamikiwa ambao ni Lissu na jamuhuri za kupinga rufaa hiyo na jopo hilo la majaji litatoa maamuzi.
 
Tayari Lissu alitoa hoja saba za kupinga rufaa hiyo, ambazo ni mkata rufaa Seleman ambaye ndiye mlalamikaji namba moja kupinga kwamba hajakata rufaa kwa hati ya kiapo ya Mei 24 mwaka huu.
 
Alisema hoja nyingine ni notisi ya kiapo kutopelekwa kwa mjibu rufaa ambaye ni yeye kinyume na masharti ya kanuni ya 84 (1) ya Kanuni za Adhabu za Mahakama ya Rufaa Tanzania za mwaka 2009.
 
“Vile vile nakala zote rekodi za rufaa hazijathibitishwa usahihi wake na wakata au wakili kinyume na masharti ya Kanuni ya 96 (5) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa Tanzania za mwaka 2009.
 
“Rufaa hii pia imepitwa na muda wake kwa sababu hati ya ucheleweshaji iliyotolewa na Msajili wa Mahakama Kuu haijasainiwa, haina tarehe wala muhuri kinyume na Kanuni ya 90 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania za mwaka 2009,” alisema.
 
Lissu aliongeza kuwa walalamikaji walitakiwa kukata rufaa siku sitini baada ya notisi ya rufaa kutolewa na kwamba tarehe ya mwisho ya kukata rufaa ilikuwa Julai 3 mwaka jana lakini rufaa hiyo ilikatwa Mei 7 mwaka huu.
 
“Hoja nyingine ni kwamba rufaa hiyo si halali kwa kuwa imeacha nyaraka muhimu ikiwemo maombi ya mwenendo wa shauri wa kusamehewa gharama za dhamana,” alisema.

Lissu alisema pia katika rufaa hiyo, amri iliyomshindisha kesi si halali kwa kuwa haionyeshi tarehe ambayo amri hiyo ilitolewa kinyume na kanuni ya 9 ya Kanuni za Masijala za Mahakama Kuu za mwaka 2005.
 
Alisema pia wakata rufaa wamesindwa kuwasilisha mahakamani hoja za maandishi za kuunga mkono hoja za rufaa yao ndani ya siku 60 au kuomba muda wa kuziwasilisha.
 
Pia hoja nyingine ni kushindwa kuwasilisha hoja hizo za maandishi kinyume cha Kanuni ya 106 (1), (2) na (9) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania za mwaka 2009.
 
Kesi ya kupinga ubunge wa Lissu ilianza kusikilizwa Machi 12, 2012 na Jaji wa Mahakama Kuu, Moses Mzuna, aliyetoa hukumu April 27, mwaka huu, na kumtangaza Lissu kuwa mbunge halali wa Singida Mashariki kwa kigezo kuwa hoja zote zilizotolewa na wanachama hao wa CCM hazitoshi kutengua au kubatilisha ubunge wake.

-Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment