Tuesday, September 10, 2013


DODOMA. 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitatumia nguvu ya umma kuikataa Katiba Mpya endapo CCM na Serikali yake: “vitaendeleza hila na ubabe katika mchakato unaoendelea.”

Pia chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimeitaka Serikali kuboresha Daftari la Kudumu la Wapig
akura kabla ya upigaji wa kura ya maoni ya Katiba Mpya huku kikisema kinyume chake suala hilo litaibua mgogoro mkubwa.
Kauli hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika katika mahojiano yaliyofanyika Mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Mnyika alisema baada ya CCM kuhodhi muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kulifanya Bunge la Katiba liwe ni hodhi ya chama hicho tawala karata pekee waliyobakiwa nayo ni kura ya maoni... 

“Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ndiye atakayeteua wajumbe 166 kutoka taasisi na makundi na kufanya Bunge zima la Katiba kuwa na wajumbe zaidi ya 600.”
Alisema kwa sasa, Tanzania Bara hakuna utaratibu wa kikatiba wa namna ya kuendesha kura ya maoni na kuongeza.
“Wenzetu Zanzibar katika Katiba yao wanao mfumo wa kura ya maoni, sisi haupo ni lazima tutengeneze sheria ya kura ya maoni ya Katiba Mpya na Sheria ya kura ya maoni ya Muungano,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema Kamati ya Bunge la Katiba, Sheria na Utawala inapaswa kuanza kukutana kwa dharura kupata maoni ya wadau kuhusu kura ya maoni na ianze na Zanzibar ambayo haikushirikishwa.
“Kamati ianze sasa, isisubiri Bunge la Oktoba 29 maana kati ya mambo yaliyoifanya Serikali kuondoa muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni ni mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Muungano,” alisema.
Alisema pia Tanzania inahitaji kuwa na Katiba ya mpito ambayo itaweka chombo huru kitakachosimamia upigaji wa kura ya maoni badala ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mbowe alisema Serikali ya CCM inatumia hila na ubabe kuhakikisha inapatikana Katiba Mpya itakayobeba masilahi ya chama hicho kwa gharama yoyote.
 “Endapo CCM itaendelea na hila zake hizi niwaambie Chadema tumejipanga… Tutatumia teknolojia ya kisasa kuwafikia Watanzania hata ikibidi kutumia helikopta nne ili waikatae wakati wa kupiga kura ya maoni,” alisema Mbowe na kuongeza: “Hila yoyote itakayotokea kwenye Katiba tutahamasisha Watanzania kuikataa, wasifikiri wanachokifanya ni salama kwao… Wanageuza mchakato kuwa wa kichama badala wa wananchi.”
Alisema msimamo wa CCM kukataa mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu si wa wanachama wake wa kawaida, bali matakwa ya viongozi wake wa juu. MWANANCHI.

0 comments:

Post a Comment