Wednesday, April 17, 2013

Picture
Katibu wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo, Badi Darusi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo
Na Mwandishi wa TheHabari

WASHIRIKI wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wamejitokea na kulalamikia mchakato mzima wa upatikanaji wajumbe wa mabaraza ya Katiba uliofanyika maeneo mbalimbali hivi karibuni. Wawakilishi hao ambao baadhi yao walishiriki kugombea nafasi mbalimbali za uwakilishi, wametoa malalamiko hayo leo jijini Dar es Salaam walipokuwa wakizungumza na vyombo anuai vya habari.

Akizungumza katika mkutano huo na wanahabari, Katibu wa jukwaa hilo, Badi Darusi kutoka TOWSF, alisema kulikuwa na dosari nyingi katika uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya uliofanyika hivi karibuni, hivyo kuitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba ifanye tathmini ya zoezi zima na kuangalia namna ya kuondoa kasoro hizo.

Alisema kwa baadhi ya maeneo baadhi ya wasimamizi wa mchakato huo ngazi za mitaa waliingiza itikadi za vyama, dini na pia kuwepo kwa mazingira ya rushwa hivyo kushauri kuna kila sababu ya mchakato huo kwa mkoa wa Dar es Salaam urudiwe upya ili haki itendeke.

Alisema vyama vya siasa vilikuwa vinatumia fursa ya kufanya kampeni chafu kinyume na utaratibu na muongozo uliowekwa na Tume ya Taifa ya mabadiliko ya Katiba, na kuongeza kuwa katika baadhi ya mitaa waliongeza sifa ya kuwa mwanachama wa chama fulani ili uchaguliwe kuwa mjumbe wa baraza la katiba jambo ambalo ni kinyume na maelekezo yaliyotolewa na tume.

“Tumeshtushwa sana na namna mchakato huu ulivyogubikwa na kasoro mbalimbali ambazo zisipochukuliwa hatua madhubuti tunaweza tukawa na katiba ambayo haitokani na wananchi. Mchakato huu uligubikwa na vitendo vya udini, siasa, rushwa, vitisho na ubaguzi wa kijinsia. Hali hii ilipelekea baadhi ya watu waliokuwa na sifa za kuwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba kuenguliwa kimakosa kutokana na utashi na maslahi binafsi ya watu wachache,” alisema Darusi.

Aidha alitolea mfano katika mitaa ya Msakuzi, Kata ya Mbezi na Mtaa wa Mbagala Rangitatu kata ya Charambe wagombea wa ujumbe wa mabaraza ya katiba ambao hawajulikani misimamo yao katika siasa waliulizwa wazi wazi kuwa wao ni wafuasi wa chama gani na baadhi ya viongozi wa mitaa ambao ndio walikuwa wasimamizi wakuu wa mchakato huo.

“Mfano hai ni kata ya Mabibo yenye wakazi 72,000 (sensa ya 2002) imeshindwa kupata wajumbe wa mabaraza ya katiba kwa sababu ya wajumbe 7 wa baraza la maendeleo la kata (WDC) kushindwa kuafikiana eti kila mmoja akitaka mtu wa chama chake ndio awe mjumbe wa baraza la katiba la wilaya ya kinondoni kinyume na maelekezo na muongozo wa kuwapata wajumbe hao uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Hali hii inawafanya wakazi wa kata ya mabibo kukosa uwakilishi katika baraza la katiba la wilaya,” alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa mchakato huo pia uligubikwa na vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji wa jinsia uliofanya na baadhi ya viongozi wa mitaa na vyama vya siasa, kwenye baadhi ya mitaa wasichana waliokuwa na umri wa miaka 18 hadi 35 walienguliwa katika kundi la vijana na kuwekwa katika kundi la Wanawake watu wazima kinyume na utashi wa mtu binafsi aliyegombea. Mfano ni mtaa wa Mbagala Rangi Tatu kata ya Charambe.

Hata hivyo waliiomba Serikali na Tume ya Mabadiliko ya Katiba zichukue hatua madhubuti za kukabiliana na vitendo vya udini vinavyoshika hatamu kwa mgongo wa mchakato wa katiba mpya ili kuhakikisha katiba haiundwi kwa itikadi za mazingira hayo.

Alisema endapo mchakato huo utarudiwa walipendekeza Kamati ya Maendeleo ya Kata isiwe na dhamana ya kuwachagulia wananchi wajumbe wa mabaraza ya katiba kwani wengi wanaongozwa na utashi wa kisiasa na wananchi pekee ndio wawe na dhamana ya kuwachagua wawakilishi wao.

“Tume ya Mabadiliko ya Katiba iangalie namna mpya ya kuyashirikisha makundi ya watu walio pembezoni kwenye mabaraza ya katiba ili kuwa na uwakilishi katika kujadili rasimu ya katiba. Mfano muongozo uliotolewa na tume hauja ainisha ni namna gani watu wenye ulemavu watashikiriki katika kuingia kwenye mabaraza ya katiba ya wilaya.”

Mchakato wa katiba mpya usiendeshwe kwa haraka kwani unawafanya wananchi walio wengi wasiwe na taarifa sahihi kuhusu kinachoendelea katika  mchakato huu wa uundaji wa katiba mpya. Tume ya katiba iangalie mfumo wa kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu mwenendo wa mchakato wa katiba mpya nchini kwani taarifa nyingi hazifiki kwa wananchi walio wengi na kwa wakati.
Picture
Baadhi ya wajumbe wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo, wakizungumza na waandishi wa habari leo

TAMKO DHIDI YA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA, NGAZI YA KATA NA MITAA.


Washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)  tunatoa tamko hili baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya wilaya kuanzia ngazi ya Mtaa hadi Kata. Tumeshtushwa sana na namna mchakato huu ulivyogubikwa na kasoro mbalimbali ambazo zisipochukuliwa hatua madhubuti tunaweza tukawa na katiba ambayo haitokani na wananchi.

Mchakato huu uligubikwa na vitendo vya udini, siasa, rushwa, vitisho na ubaguzi wa kijinsia. Hali hii ilipelekea baadhi ya watu waliokuwa na sifa za kuwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba kuenguliwa kimakosa kutokana na utashi na maslahi binafsi ya watu wachache.

Katika mchakato huu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya msukumo na utashi wa kisiasa ndio uliokuwa unaongoza katika kuwapata wajumbe hao. Kwa mfano katika mtaa wa Msakuzi kata ya Mbezi na Mtaa wa Mbagala rangi tatu kata ya charambe wagombea wa ujumbe wa mabaraza ya katiba ambao hawajulikani misimamo yao katika siasa waliulizwa wao ni wafuasi wa chama gani na baadhi ya viongozi wa mitaa na kata ambao ndio walikuwa wasimamizi wakuu wa mchakato huu.

Lakini pia vyama vya siasa vilikuwa vinatumia fursa ya kufanya kampeni chafu kinyume na utaratibu na muongozo uliowekwa na Tume ya taifa ya mabadiliko ya katiba. Kwa mfano katika baadhi ya mitaa waliongeza sifa ya kuwa mwanachama wa chama fulani ili uchaguliwe kuwa mjumbe wa baraza la katiba kinyume na maelekezo yaliyotolewa na tume. Mfano hai ni kata ya Mabibo yenye wakazi 72,000 (sensa ya 2002) imeshindwa kupata wajumbe wa mabaraza ya katiba kwa sababu ya wajumbe 7 wa baraza la maendeleo la kata (WDC) kushindwa kuafikiana eti kila mmoja akitaka mtu wa chama chake ndio awe mjumbe wa baraza la katiba la wilaya ya kinondoni kinyume na maelekezo na muongozo wa kuwapata wajumbe hao uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Hali hii inawafanya wakazi wa kata ya mabibo kukosa uwakilishi katika baraza la katiba la wilaya.

Mchakato huu pia uligubikwa na vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji wa jinsia uliofanya na baadhi ya viongozi wa mitaa na vyama vya siasa. Mfano kwenye baadhi ya mitaa wasichana waliokuwa na umri wa miaka 18 hadi 35 walienguliwa katika kundi la vijana na kuwekwa katika kundi la Wanawake watu wazima kinyume na utashi wa mtu binafsi aliyegombea. Mfano ni mtaa wa Mbagala Rangi Tatu kata ya Charambe.
Mchakato huu wa kuwapata wajumbe wa baraza la katiba la wilaya uligubikwa na dhana nzima ya udini baina ya Wakristo na Waislam. Hali hii inapelekea kuligawa taifa letu kwa misingi ya dini na kama hatua madhubuti za kukabiliana na hili hazitachukuliwa mwelekeo wa nchi yetu utakua mbaya kwani jambo hili linaua umoja wa kitaifa uliojengwa na waasisi wa taifa hili.

Kutokana na tuliyoyaeleza hapo juu tunadai yafuatayo:

i. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ifanye tathmini ya zoezi zima la upatikanaji wa wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya na iangalie namna gani ya kuondoa kasoro hizi ili kuwapata wajumbe halali wa mabaraza haya.

ii. Serikali na Tume ya Mabadiliko ya Katiba zichukue hatua madhubuti za kukabiliana na vitendo vya udini vinavyoshika hatamu kwa mgongo wa mchakato wa katiba mpya.

iii. Mchakato wa upatikanaji wa wajumbe wa mabaraza ya katiba kwa mkoa wa Dar es Salaam urudiwe upya kwani ulikuwa na kasoro nyingi na haukuwa wa haki.

iv. Kamati ya Maendeleo ya Kata isiwe na dhamana ya kuwachagulia wananchi wajumbe wa mabaraza ya katiba kwani wengi wanaongozwa na utashi wa kisiasa na wananchi pekee ndio wawe na dhamana ya kuwachagua wawakilishi wao.

v. Tume ya Mabadiliko ya Katiba iangalie namna mpya ya kuyashirikisha makundi ya watu walio pembezoni kwenye mabaraza ya katiba ili kuwa na uwakilishi katika kujadili rasimu ya katiba. Mfano muongozo uliotolewa na tume haujaainisha ni namna gani watu wenye ulemavu watashikiriki katika kuingia kwenye mabaraza ya katiba ya wilaya.

vi. Mchakato wa katiba mpya usiendeshwe kwa haraka kwani unawafanya wananchi walio wengi wasiwe na taarifa sahihi kuhusu kinachoendelea katika  mchakato huu wa uundaji wa katiba mpya.

vii. Tume ya katiba iangalie mfumo wa kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu mwenendo wa mchakato wa katiba mpya nchini kwani taarifa nyingi hazifiki kwa wananchi walio wengi na kwa wakati.

Mwisho, Tume ni lazima itambue mchango wa wanahabari katika mchakato mzima wa uundaji wa Katiba Mpya Tanzania na kuhakikisha makosa yaliyofanyika ya kuwasahau wanahabari katika uundaji wa mabaraza ya katiba ya wilaya yasijirudie tena katika uundaji wa vyombo kama Mkutano Mkuu Maalum wa Katiba, Bunge Maalum la Katiba.

Imesainiwa na kutolewa kwa niaba ya washiriki wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS) na:
    JINA                TAASISI ANAYOTOKA
1. Liwile Mahamoud     Tabata Youth Center
2. Hamad Masudi        Jipange Women Group
3. Janeth Biseko       TAKIWOYA
4. Abela Kamulali      TEYODEN
5. Rehema Mayuya       TAKUMATA
6. Mary Laus Mbawala   Jipange Women Group
7. Kedmon  Semwali     Mabibo Youth Movement
8. Samaha Semanga      Jipange women Group
9. Amina Mcheka        Mburahati
10. Nantaika Maufi     Community Care
11. Janeth Mawinza     Jipange Women Group
12. Badi  Darusi       TOWSF
13. Hawa Assed         Jipange Women Group
14. Celina Ndomba      Community Care

Nantaika Maufi                                  Badi  Darusi
...........................                     .........................
Mwenyekiti                                       Katibu

0 comments:

Post a Comment