Saturday, April 27, 2013

Kwa mujibu wa Wakili, Mwanasheria Humphrey Mtui, makosa ambayo Mbuge wa Arusha Mjini, (Godbless Lema, ambaye kwa sasa yupo korokoroni) yanatarajiwa kusomwa kizimbani hapo siku ya Jumatatu na kushitakiwa kwayo yote yakiwa chini yq uchochezi, ni:-

  1. Kuwaambia Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu alipoenda Chuoni hapo kuwatuliza kuwa ‘dhambi kubwa kuliko zote ni woga‘ na 'Haki hutafutwa na kupiganiwa ikiwa jambo unalolipigania ni la msingi na linafaa kupiganiwa, (Worth fighting for)'. 
  2. Kutamka "Tumemtafuta Mkuu wa Mkoa juu ya matatizo yenu na mlivyoshuhudia hapa amechukua muda mrefu na kuingia kama vile anaingia kwenye send-off. Hawa ndiyo viongozi wetu ambao hawajali matatizo ya wananchi."
  3. Kutamka na kuwaambia wanafunzi kuwa "Mimi Mbunge wenu nipo sambamba nanyi hadi mpate haki yenu na Ikiwa Mkuu wa Mkoa hatakuja hapa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi wa Mkoa, nitawaongoza hadi ofisini kwake ili mpate majibu na haki yenu kwani ni haki yenu ya msingi kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo niliapa kuilinda Bungeni, na pia inaruhusiwa kwa mujibu wa kanuni na kifalsafa katika utekelezaji wa utawala bora wa kidemokrasia ambao msingi wake ni kusikilizwa na kulinda haki za binadamu."

MillardAyo.com imezungumza na Mkewe Lema na kuandika yafuatayo:

Taarifa za sasa kutoka Arusha ni kwamba Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi Arusha na kuhojiwa kwa tuhuma za uchochezi wa vurugu za Wanafunzi wa chuo cha Uhasibu dhidi ya Mkuu wa Mkoa Arusha juzi.

Taarifa za uhakika kutoka kwa mke wa Mh. Lema sasa hivi ni kwamba Polisi wamekataa kutoa dhamana yake na kusema mpaka jumatatu ndio itajulikana.

Mke wa Lema akiongea na millardayo.com alisema “jana usiku saa sita kasoro watu walikuja kugonga nyumbani kwetu tukamtuma kijana aende kutazama ni kina nani, aliporudi akasema ni Polisi... sisi hatukuamini na tulikataa kwa sababu hatukujua kama ni Polisi kweli au ni watu wanataka kuitumia hiyo nafasi kufanya uhalifu, mimi nimeshinda Polisi kutwa nikifatilia gari mbona chochote hakikutokea?”

“Baada ya muda kusogea ikabidi Lema aanze kuwapigia marafiki, jamaa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA, kabla ya hapo pia tuliamua kupiga kengele ya kampuni ya ulinzi ambao muda mfupi baadae walikuja na gari yao huku Polisi wakiendelea na vitisho kwamba watapiga mabomu na kuvunja ukuta la sivyo Lema ajisalimishe, Viongozi wa CHADEMA na marafiki walipowasili wakamshauri Lema ndio akajitokeza wakati huo ni saa tisa usiku”

“Alipojitokeza Polisi walimchukua na mimi nikaondoka nao. Tulipofika kituoni walimtaka Lema kutoa maelezo lakini alikataa na kusema mpaka mwanasheria wake aje hivyo akapelekwa rumande, asubuhi tulipoamka na kuanza kufatilia.
R.C.O alisema yuko kwenye kikao na haongei na yeyote isipokua Mwanasheria wa Lema, walipomaliza kikao saa nane maelezo yakaanza kutolewa huku Mwanasheria akiwepo na kazi ikamalizika jioni saa 11 ambapo Polisi wamekataa kutoa dhamana mpaka Jumatatu.”

“Shitaka kubwa lililo mbele yake ni uchochezi na kauli ambayo anadaiwa Lema kuitoa mbele ya Wanachuo cha Uhasibu kwamba dhambi kubwa kuliko zote ni woga, na hata leo kwenye maelezo Lema amewaambia watu wa Arusha mjini hivyo hivyo, kwamba dhambi kubwa kuliko zote ni woga.”

Kwa kumalizia, Mke wa Mbunge Lema amesema, “gari letu lililokuwa linashikiliwa na Polisi tumerudishiwa baada ya kutakiwa kulipia elfu 50 ya wale waliolivuta, gari liko zima kabisa. Toka nimeolewa na Lema nimeshuhudia akienda polisi zaidi ya mara 20, mara yake ya kwanza kushuhudia anapelekwa polisi ni wakati wa kampeni za Ubunge."

0 comments:

Post a Comment