Sunday, February 3, 2013

Wakati hatma ya ubunge wa Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ikisubiriwa kama alivyoahidi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amejitokeza akionesha kuunga mkono hoja ya Mbunge huyo kuhusu mitaala.
Akiwa bungeni wiki hii, Mbatia alisema Serikali haina mitaala ya elimu na kama itaweza kuiwasilisha bungeni, yeye atakuwa hana budi ila kujiuzulu ubunge.

Serikali kwa upande wake kupitia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, iliahidi kupeleka nakala 300 za mitaala hiyo ili igawiwe kwa wabunge na kuthibitisha madai ya Mbatia kuwa ni batili.

Wakati Serikali ikitoa ahadi hiyo, Mbatia alisimamia hoja yake, akisema Wizara haina mitaala na akaahidi dhahiri kwamba iwapo itaoneshwa, atakuwa tayari kujiuzulu ubunge.

Katika hatua nyingine, Lowassa katika mahafali ya 13 ya sekondari ya Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana, akiwa mgeni rasmi, alisema kuna udhaifu katika elimu nchini kutokana na mitaala mibovu ambayo inaandaa wahitimu kutafuta na si kutengeneza kazi.

“Ubovu wa mitaala ya elimu unawatengeneza kuwa watafuta kazi, lakini ni vema zaidi mitaala ikabadilishwa, ili hata wahitimu wanapomaliza masomo yao wawe watengeneza kazi na si tegemezi tena,” alisema Lowassa.

Alisema mitaala inahitaji kubadilishwa ili kusaidia wanafunzi wawapo shuleni na wamalizapo wajiendeleze kimaisha kwa kutengeneza kazi zao binafsi.

Wakati hayo yakiendelea, wabunge wa upinzani waliazimia kupeleka taarifa kwa Mamlaka ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge  kutaka Waziri Kawambwa  ajiuzulu kwa kudanganya Bunge au Mamlaka iliyomteua imfukuze kazi.

Katika Mwongozo wa Spika  juzi, baada ya malumbano yaliyosababisha yeye na wabunge wa upinzani kususa Bunge, Mbatia alitaka Waziri Kawambwa awasilishe nakala siku hiyo ili kujiridhisha nani alisema uongo.

“Nilitamka rasmi, kwamba kama ipo (mitaala) niko tayari kuondoka katika nafasi hii,” alisema Mbatia.

Akitoa Mwongozo, Naibu Spika Job Ndugai alisema: “Kwa dai lake anaomba Mheshimiwa Waziri Kawambwa alipokuwa anachangia hoja yake kijitabu alichokionesha kuhusu mitaala, alitaka kiwekwe mezani.”

Ndugai aliendelea: “Na uhakika kutoka serikalini ni kwamba Mheshimiwa Waziri ameshaagiza Dar es Salaam kutoka kwa wachapaji, nakala 300 kwa ajili ya  wabunge na zitaletwa Februari 6, wiki ijayo…mitaala hiyo itakuwa katika ofisi ya Bunge; naomba subira tutafika mahali tu pa kuelewana.”

Mbatia katika hoja yake alisisitiza kwamba hadi mwaka 2011, nchi haikupata kuwa na mitaala rasmi ya kitaifa kwa ajili ya elimu ya shule za msingi au sekondari.

Alisisitiza kwamba, hapajawahi kuwapo andiko mahsusi la mtaala wa elimu kwa taifa na kusema Taasisi ya Elimu imekuwa ikiajiri wakuza mitaala kwa zaidi ya miaka 15 bila kutoa mitaala yoyote katika namna ya andiko mahsusi.

Kwa mujibu wa Mbatia, nyaraka za Wizara ya Elimu zina ainisho la dhana ya mitaala ambalo kwa kiasi fulani linatoa mtazamo usiowezesha kutambua mitaala inayotakiwa kuwapo kwa mapana.

Waziri Kawambwa alipokuwa akijibu hoja juu ya mitaala, alisisitiza kwamba ipo na tangu nchi ipate uhuru, imebadilika mara nne na kutaja miaka ya mabadiliko kuwa ni 1967, 1979, 1997 na 2004-2009.

Mjadala kuhusu mitaala ulijitokeza kutokana na hoja binafsi ya Mbatia bungeni Alhamisi kuhusu udhaifu ulio katika sekta ya elimu nchini.

Kwa upande wake, Lowassa  alisema kuna udhaifu mkubwa katika sekta ya elimu nchini, unaosababishwa na ubovu wa mitaala.

Alikitaka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuacha kugombana na Serikali badala yake kikae ili kukubaliana jinsi ya kutatua migogoro baina yake na Serikali.

“Elimu isaidie wahitimu kutengeneza kazi, kwa sababu nchini hakuna ajira na kama hakuna matokeo yake ni mabomu kulipuka, kwa mfano wa Misri, sasa tusipokuwa makini na hapa kwetu yatalipuka mabomu ya aina hiyo,” aliongeza.

Aliipongeza hatua ya Serikali kurudisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa wanafunzi wanaohitimu kabla ya kuendelea na vyuo vikuu, huku akiwasisitiza wanafunzi kuwa mafunzo hayo yatawajengea utaifa na uzalendo wa nchi yao hivyo wasiwe na wasiwasi.

“Maombi yalikuwa ni vijana 40,000 lakini kwa sasa Serikali imepeleka vijana 5,000, kwa mwakani ihakikishe inapeleka vijana wote,” alishauri.

Aidha, aliongeza kuwa wanafunzi hao wamepata bahati ya kumaliza katika shule yenye jina kubwa - Benjamin William Mkapa - ambaye alikuwa Rais wa Awamu ya Tatu, aliyeongoza nchi kwa uadilifu mkubwa na kuacha nchi ikiwa ya amani na mshikamano kwa Tanzania Bara na Visiwani.

“Mkapa alikuwa kiongozi shujaa, alikuwa muwazi na mkweli na mpaka sasa bado ni shujaa kwani kutokana na uongozi wake, alikuwa msuluhishi wa migogoro ya nchi mbalimbali,” alisema Lowassa.
Shukurani kwa: Picha (zote) blogu ya Nyakasagani; Taarifa ya maandishi blogu ya Ziro99

0 comments:

Post a Comment