Tuesday, January 1, 2013

MBUNGE wa Mchinga mkoani Lindi, Said Mtanda (CCM), amebeza maandamano ya wananchi wa Mtwara yaliyofanyika hivi karibuni kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.

Hata hivyo Mtanda hakuweza kukubaliana na madai ya waandamanaji hao ya kutaka gesi hiyo isipelekwe Dar es Salaam na badala yake ibaki Mtwara kwa maelezo kuwa, rasilimali hiyo ni ya Watanzania wote bila kujali itokako.

Alisema maandamano ni haki iliyotolewa na Katiba na hana shida na maandamano hayo iwapo yalifuata taratibu kwa ajili ya kuelezea hisia zao.

“Wananchi wenzetu kote nchini hawatatuelewa endapo tutadai kwamba gesi hiyo itumike Mtwara au Kusini pekee. Suala la msingi hapa ni kuangalia ni namna gani wananchi wa mkoa huo na kusini watakavyonufaika na gesi hiyo,” alisema Mtanda.

Alitolea mfano nchi ya Trinidad &Tobago, huko Amerika ya Kusini, ambayo inanufaika na gesi kwa kuiuza nchini Marekani na nyingine kuzalishia mbolea na umeme. Aliitaja pia Urusi kuwa nayo inanufaika na gesi hiyo kwa kuisafirisha na kuiuza nje na kusema kwamba hiyo ni aina mojawapo ya faida za gesi. Alisema tatizo lililojitokeza hadi maandamano hayo kufanyika ni hali ya wananchi kukosa elimu sahihi juu ya matumizi ya rasilimali ya gesi na mgawanyo wake.

“Tatizo hapa ni kwamba wananchi wa Mtwara hawajapewa elimu, ni vema kila kiongozi atimize wajibu wake katika kutoa elimu, wananchi wanataka kufahamu watafaidika vipi na hii gesi? Mimi hivi karibuni nilifanya ziara jimboni niliwaeleza waende katika Tume ya Katiba mpya, kile ni chombo cha Serikali wakatoe maoni yao kuhusu rasilimali hii ya gesi. Nikiwa bungeni nimelisema sana suala hili na matokeo yake tulikubaliana na Rais Kikwete kwamba wananchi wa Kusini waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 99, 000. Tumefanya hivyo ili kutoa fursa kwa wananchi wengi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, kufaidika na umeme huo wa gesi. Hii ni gharama ndogo zaidi kuliko mikoa mingine nchini,” alisema Mtanda.

Mtwara inatarajia kuwa na Kiwanda kikubwa cha Saruji ambacho kitakuwa kikubwa kuliko kile cha Wazo Hill kilichoko Dar es Salaam na viwanda vingine vya mbolea. Alivitaka vyombo vya habari nchini kusaidia kutoa elimu juu ya umuhimu wa nishati hiyo ya gesi kwa faida ya kujenga uchumi wa Taifa na kuepusha migogoro isiyokuwa na tija.

Kuhusu wabunge wa Mikoa ya Kusini, kushindwa kuungana na kutoa tamko baada ya kutokea kwa maandamano hayo, alisema: “Kwanza hakuna umoja wa wabunge wa kusini, isipokuwa kuna umoja wa wabunge wa Mkoa wa Mtwara, ambaye Mwenyekiti wake ni Mama Anna Abdallah. Umoja wa wabunge wa Mkoa wa Lindi Mwenyekiti wake ni Membe. Sasa kama unataka maoni zaidi watafute hao, lakini mimi msimamo wangu ni huo.”

via Mtanzania


0 comments:

Post a Comment