Sunday, December 2, 2012

MWEZI Aprili, 2008, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu kwa kipindi hicho, Andrew Chenge, almaarufu Mzee wa Vijisenti, akihojiwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini kuhusu tuhuma za kumiliki kiwango kikubwa cha fedha, kilichokadiriwa kuzidi dola za Marekani milioni moja katika akaunti yake iliyopo Kisiwa cha Jersey huko nchini Uingereza, alijibu kwa kusema kwamba, fedha hizo kwa viwango vyake zilikuwa ni vijisenti tu, na kusisitiza kuwa suala la kumiliki kiasi gani cha fedha si hoja ya kuzungumza, kwani kila mtu ana kiwango chake cha pesa.
Waandishi wa habari walilazimika kumuhoji kiongozi huyo kutokana na habari iliyokuwa imechapishwa takribani wiki moja kabla ya siku hiyo katika gazeti la The Guardian la nchini Uingereza kuwa, katika uchunguzi uliofanywa na taasisi ya kuchunguza makosa makubwa ya jinai nchini humo (SFO), Chenge alihusishwa na kashfa iliyoihusu Kampuni ya BAE Systems kutokana na mkataba wa kuiuzia Tanzania rada kwa matumizi ya kijeshi kwa bei ya sh bilioni 70.
Baada ya vyombo vya habari vya hapa nchini kuweka hadharani yale majibu ya Chenge ya vijisenti, Watanzania wengi tulipatwa na mshangao mkubwa sana, kwa kumshangaa kiongozi huyo kuziita pesa zote hizo kuwa kwake ni vijsenti tu!
Kwa hakika mshangao huo haukutugusa Watanzania wa kawaida tu, bali hata mkuu wa nchi na yeye inaelekea alishtushwa pia, ndiyo maana akakubali kiongozi huyo ajiuzulu nafasi yake ya uwaziri wa Miundombinu.
Kwa ujumla Chenge hakueleweka kabisa mbele ya macho na masikio ya wengi wetu, alipodiriki kusema zaidi ya shilingi bilioni moja za Kitanzania kuwa ni vijisenti wakati asilimia kubwa ya Watanzania hatuna uwezo kabisa wa hata kuziona tu hizo pesa. Hali hiyo ilituacha na maswali mengi sana bila majibu!
“Hivi kama hizo dola milioni moja yeye anasema ni vijisenti tu, je, hizo ambazo yeye anaweza kuziita shilingi zingekuwa ngapi na za sura ipi?” Hili ni moja kati ya maswali ambayo wengi wetu tulikuwa tukijiuliza bila ya kupata majibu kwa kipindi kirefu sana.
Leo hii nadiriki kusema kuwa, kumbe Chenge hakukosea kusema zile dola za Kimarekani milioni moja ambazo kwa wakati ule zilikuwa ni kama bilioni moja na nusu za Kitanzania, zilikuwa ni vijisenti tu kwa maana wapo vigogo wa serikali hii hii ya Tanzania wenye mabiloni ya dola za Kimarekani zaidi ya milioni 186, kiwango ambacho ni takribani shilingi milioni 300 za Kitanzania.
Sasa ukijaribu kufanya hesabu hata ile iliyo ndogo kabisa ya ulinganifu kati ya hizo bilioni moja za Chenge na hizi bilioni 186, bila shaka utakubaliana na mimi kuwa hizo za Chenge ni vijisenti tu kama alivyosema mwenyewe hapo awali na tukashindwa kumwelewa alikuwa na maana gani.
Ni dhahiri Chenge alikuwa anajua kuwa wapo Watanzania wengine wenye pesa za kutisha ukilinganisha na za kwake, ndiyo maana kutokana na tofauti kubwa kati ya pesa yake na ya hao wengine, akajiona kuwa zake yeye ni kama vijisenti tu na siyo shilingi za kutisha.
Kama tulivyoelezwa kuwa katika orodha hiyo ya Watanzania wenye pesa katika benki za nchini Uswisi, hakuna hata mmoja mwenye vijisenti vidogo kama vya Chenge, wapo watano wenye dola za Marekani milioni 56 (sawa na takriban sh bilioni 90 za Kitanzania), dola milioni 30 (sawa na sh bilioni 48), mwingine dola milioni 20 (sh bilioni 32) na wengine wawili wa mwisho kila mmoja anamiliki dola milioni 10 (sh bilioni 16).
Katika orodha ya walioweka fedha nchini humo, pia wamo wafanyabiashara wanaomiliki kiasi cha dola kati ya milioni mbili na saba.
Habari hizo zilikuwa zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha sh bilioni 315.5 zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Kwa mchanganuo huo, ni dhahiri hizo za Chenge ni vijisenti tu.
Mzee wa vijesenti ibuka huko ulipojichimbia utudhihirishie kuwa uliposema vijisenti ulikuwa una maana ya dhati na si kuwadhihaki Watanzania, kwani kweli tumesikia kuwa wapo Watanzania wenye shilingi na si vijisenti kama vyako. Hayo siyo mambo, usikae kimya mafichoni, njoo uwataje ni akina nani hao?

0 comments:

Post a Comment