Friday, November 2, 2012

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema hatua ya kufukuzwa kazi pekee kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), William Mhando, haitoshelezi, bali yeye na wenzake alioshirikiana nao wanapaswa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), alisema hayo kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari kupitia mtandao wa kompyuta, ikiwa ni siku moja baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, kutangaza kumwachisha kazi Mhando baada ya kukutwa na hatia ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Mnyika alisema baada ya kufukuzwa kazi, serikali inatakiwa kurejea katika hotuba aliyoitoa bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya kutaka Mhando pamoja na wenzake walioshirikiana nao katika kashfa hiyo wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Pia aliitaka Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, kueleza hatua, ambazo imezichukua kwa watendaji wengine wa shirika hilo, ambao walishirikiana na Mhando.

“…Na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za haraka, nitaiweka hadharani taarifa ya kamati iliyoundwa na bodi hiyo kuchambua taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kueleza hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya bodi yenyewe,” alisema Mnyika.

Alitaka hatua dhidi ya Mhando na wenzake waliohusika, kutogeuzwa kuwa kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa serikali kwa ujumla wake, kwani taarifa za utendaji wa TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika, zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na vya Baraza la Mawaziri pia.

Alisema ili ukweli wa kina ujulikane, Kambi Rasmi ya Upinzani imependekeza Bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta kwa ajili ya mitambo ya umeme.

Alitaka uchunguzi huo umshirikishe CAG katika kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi kwa malipo yaliyofanywa na kampuni ya BP, ambayo kwa sasa ni Puma, Oryx na Camel Oil,  ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme.


---
Habari hii imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la NIPASHE

0 comments:

Post a Comment