Wednesday, November 14, 2012

Ndugu zangu,

Mwalimu Julius Nyerere aliamini, kuwa fedha ni matokeo , na wala si msingi wa maendeleo. TANU kama Chama kikaamini hivyo, na umma nao uliaminishwa hivyo. Mwalimu alifikiri kama Aristoteles, mwanafalsafa wa Uyunani ya Kale.

 Aristoteles aliamini, kuwa fedha kama yenyewe haimpi mwanadamu furaha, lakini, malengo ya kutumika kwake yakiwa mazuri inampa mwanadamu furaha na maisha bora.

 Tafsiri yake, kamwe katika siasa fedha haiwezi kuwa malengo, bali nyenzo ya kufikia maendeleo, hivyo, ni matokeo pia. Bila shaka, Mwalimu Nyerere alimsoma na kumwelewa vema Aristoteles.

Lakini, tunafanyaje pale fedha kama nyenzo inapotumika kama malengo, hususan kwenye dhamira ya kujitafutia vyeo vya kisiasa, na hivyo kujinufaisha binafsi? Leo usiku nilifuatilia ‘ Live’ ( TBC1) Mkutano Mkuu wa CCM pale Kizota, Dodoma.

Kuna nilichokiona, na naamini kuna wengine wengi wamekiona nilichokiona. Na fikra zangu kwa wakati fulani zilielekea kwa Mwana- CCM kwa jina la Philip Mangula. Amechaguliwa kwa asilimia mia moja ya kura kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Bara.

 Mangula hakuwa na mpinzani. Nikajiuliza, ingekuwaje kama nafasi ile ingekuwa inagombewa na zaidi ya mtu mmoja? Maana, nilikuwemo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa St. Dominic, Iringa, Septemba 10, 2007. Ni kwenye Mkutano wa CCM Mkoa wa Iringa.

Nilimsikia Philip Mangula akitamka; “ Isifike mahali CCM ikatangaza tenda za uongozi!” Hiyo ilikuwa ni kauli nzito kutolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa CCM. Mangula aliyatamka hayo wakati akitoa hotuba ya kushukuru wajumbe. Alishindwa nafasi ya Uenyekiti wa Mkoa, na aliambulia kura 332. Mangula aliyatamka mazito hayo kunako saa nne za usiku.

Nakumbuka kimya kizito kilitawala ukumbini mle mara ile Bw. Mangula alipotamka sentesi ile. Mwandishi wa habari aliyekuwa karibu nami alinigeukia na kuniuliza; " Hivi anamaanisha nini?". Nadhani ni wengi mle ukumbini, katika ukimya ule walikuwa wanajiuliza: " Hivi anamaanisha nini?". Kauli ile ya Mangula ambayo wakati huo, niliamini kabisa kuwa ingekuwa ya mwisho katika hadhara kubwa kama ile, iliniachia tafsiri nyingi.

Tafsiri ya kwanza na ya msingi kabisa ni kuwa; Mangula alitaka kusema kuwa hakuridhika na matokeo ya uchaguzi. Pili, Mangula aliposema " Natoa taadhari isije tukafika mahala chama kikatangaza tenda ya uongozi wa udiwani na ubunge, kwamba mwenye dau kubwa ndiye atakayechukua nafasi".

Yawezekana kabisa, kuwa Mangula alitaka kusema kuwa chama chake tayari kilishafika hapo, au labda, Mangula aliingia kwenye kinyang'anyiro kile ili kujionea ni kwa kiasi gani chama chake kilichafuka kwa rushwa. Wakati leo hii nikifuatilia ‘ Live’ Mkutano wa CCM pale Kizota Dodoma, nikiri, kuwa kuna nilichojifunza kutoka kwa wajumbe wale wa Mkutano Mkuu wa CCM.

Ni wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka kwenye jamii hii hii. Na miongoni mwao, kuna waliomnyima kura Mangula pale Iringa Septemba 10, 2007, na leo wamempa Mangula asilimia mia kwa mia ya kura! Naam, kuna ya kujifunza.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
www.mjengwablog.com


0 comments:

Post a Comment