Thursday, October 18, 2012

ALIYEKUWA Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Muhimbili (MUHAS), Gervas Shayo na mwenzake Charles Jackson, wameomba Mahakama Kuu Dar es Salaam, iingigilie kati sakata la kufukuzwa kwao.

Shayo na wenzake walifukuzwa chuoni hapo Juni 21, mwaka jana kufuatia mgomo wa wanafunzi wa udaktari chuoni hapo, wakituhumiwa kuwa ndiyo walioandaa, kuratibu na kutekeleza mpango wa vitendo vya ukiukaji wa kisheria katika maeneo ya mlalamikiwa (Chuo).

Hata hivyo, juzi Shayo na Jackson kupitia kwa Wakili Peter Kibatala wamefungua maombi mahakamani hapo, chini ya hati ya dharura, wakiomba kibali cha amri ya mahakama kufuta uamuzi wa chuo kuwafukuza masomo. Katika maelezo ya maombi yao waliyoyawasilisha mahakamani hapo, walalamikaji hao wamedai kuwa, uamuzi wa chuo hicho kuwafukuza haukuwa sahihi.

“Hatukuridhishwa na uamuzi wa majibu, maombi na taratibu zilizotumika kufikia uamuzi huo.”, wanadai walalamikaji hao katika hati yao ya maelezo na kubainisha sababu nne za za kutokulidhika na uamuzi huo.

Kwanza, wanadai kuwa wakati wa usikilizaji wa mashtaka yao chuoni hapo, walinyimwa haki ya kuwakilishwa na taasisi yao na sababu ya pili wanadai kuwa, walitiwa hatiani kwa kosa ambalo hawakuwa wameshtakiwa nalo.

Katika sababu ya tatu, wanadai kuwa adhabu waliyopewa haikuwa halali na kwamba, ilikuwa ni kubwa zaidi kulinganisha na adhabu waliyopewa wenzao wengine ambao nao walitiwa hatiani kwa makosa hayo.

Katika sababu ya nne, wanadai kuwa taratibu zilizotumika kuwaadhibu zilikuwa kinyume kabisa na kanuni za haki asili.

Wakifafanua zaidi, wanadai kuwa Aprili 16, mwaka huu walipewa na mlalamikaji taarifa na maelezo ya mashtaka na kwamba, nao wakatoa maelezo yao ya utetezi.

Wanaongeza kuwa Mei 8, mwaka huu  wote walipewa taarifa ya kuhudhuria kikao cha nidhamu ili kusikiliza mashtka yao na kwamba, baada ya hapo Juni 21, mwaka huu walipewa uamuzi wa kufukuzwa masomo. Katika hati ya kiapo chao, walalamikaji hao wanadai kuwa kabla ya kuwafukuza, Desemba 15 walisimamishwa masomo kwa tuhuma za kupanga, kuratibu na kutekeleza vitendo hivyo vya uvunjaji sheria chuoni hapo.

Walalamikaji hao wanatetewa na Kibatala, ambaye ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), katika utaratibu wa chama kutoa msaada wa kisheria kwa watu mbalimbali wanaohitaji msaada huo.

--
Habari imeandikwana James Magai via MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment