Tuesday, October 30, 2012

Imeandikwa na Maulid Ahmed, Dodoma via HabariLeo

BAADA ya wafanyakazi na baadhi ya wabunge kulalamikia Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012 inayozuia mwanachama kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, Serikali imeridhia wafanyakazi kujitoa kwenye mifuko hiyo na kupewa mafao yao kama ilivyokuwa awali.

Chanzo cha habari kutoka serikalini, kimebainisha kuwa katika mkutano wa tisa wa Bunge la 10 unaoanza leo, Serikali itawasilisha tamko lake la kuruhusu fao hilo la kujitoa.

Taarifa hizo zinabainisha, kuwa Tamko la Serikali litakalotolewa bungeni, litafuta barua ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA), Irene Isaka iliyobainisha kuwa Serikali imefuta fao hilo la kujitoa na kuzuia wanachama kuchukua mafao yao.

“Serikali imeona kisheria haiwezekani kuzuia mfanyakazi kujitoa kwenye mfuko wowote, hivyo imeamua kuwasilisha taarifa yake rasmi ya kufuta muswada wake iliokuwa iuwasilishe ambao ulionekana una upungufu na hivyo kuifuta barua ya SSRA,” kilisema chanzo cha habari.

Barua ya SSRA itakayofutwa na tamko hilo, iliyokwenda kwenye mifuko hiyo ya hifadhi za jamii, ilikataza wafanyakazi kupewa mafao wanapojitoa hadi watimize miaka 55 ya kustaafu kwa hiari au kwa lazima miaka 60.

Gazeti hili (HabariLeo) Jumatatu Oktoba 29, 2012 lilipomtafuta Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka kwa ajili ya ufafanuzi, simu zake hazikupatikana.

Ofisa Habari wa Bunge, Prosper Minja alipoulizwa kuhusu taarifa za fao hilo kuwasilishwa bungeni alikataa kusema lolote, akidai taarifa za shughuli za Bunge zitatolewa leo kwa wabunge na waandishi wa habari na hapo ndipo itakapojulikana.

Hatua ya Serikali imekuja baada ya Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM), kuwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka Bunge liazimie kuitaka Serikali iruhusu fao la kujitoa liendelee.

Hata hivyo, wabunge waliazimia mambo manane ikiwamo fao hilo la kuzuiwa kujitoa lirekebishwe pamoja na barua ya Mkurugenzi Mkuu wa SSRA kufutwa.

Mbali na hoja binafsi pia Jafo alitaka kuwasilisha muswada binafsi wa kutaka fao hilo lirejeshwe, lakini muswada huo ulikataliwa kwa sababu Azimio la Bunge lilishapitishwa na kamati inayohusika na masuala ya hifadhi ya jamii ndiyo ilitakiwa ipeleke muswada.

Hata hivyo Jumatano iliyopita, wabunge walipewa muswada wa Serikali wenye lengo la kuufanyia marekebisho Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012 lakini marekebisho hayo yalihusu Mfuko wa Pensheni wa PPF pekee, kuruhusu wanachama kujitoa na kupewa mafao.

Mbunge Jafo aliliambia gazeti hili kwamba; “muswada huo tuliona una upungufu na hatukukubaliana nao, kwani ulikuwa unaletwa bila hati ya dharura, maana yake utasomwa kwa mara ya kwanza na baadaye Bunge lijalo utasomwa tena, lakini tumepanga kesho (leo) tupinge hilo.”

Hata hivyo, tayari Serikali imeonekana kubaini upungufu wa muswada huo na ndiyo maana inatarajia kueleza wabunge nia ya kupeleka tamko bungeni kuruhusu wafanyakazi kujitoa na kupewa mafao kama ilivyokuwa awali kabla ya aheria hiyo ya mwaka 2012.

Minja alisema jana kuwa, Kamati ya Uongozi chini ya Mwenyekiti wake, Spika Anne Makinda imeshakaa na kupanga shughuli za Bunge na leo baada ya kipindi cha maswali na majibu, vikao vya kamati mbalimbali za Bunge na za vyama vya siasa zitakutana na baadaye wabunge wataelezwa ratiba ya shughuli za Mkutano wa Tisa wa Bunge la 10.

0 comments:

Post a Comment