Wednesday, October 10, 2012

Habari hii ni kwa mujibu wa Fadhili Abdallah, HabariLeo, Kigoma --- POLISI mkoani Kigoma wamewapa kipigo mahabusu kutoka Gereza la Bangwe mjini Kigoma waliogoma kushuka kwenye karandinga, hivyo kusababisha vurugu kubwa kwenye Mahakama ya Mkoa mjini hapa.

Kutokana na kipigo hicho, mahabusu Maneno Kichako alipigwa na kuumizwa na hatimaye kupoteza fahamu hivyo kukimbizwa Hospitali ya Mkoa ya Maweni kwa matibabu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai amekiri kuwapo kwa vurugu hizo, na kuongeza kuwa kwa taarifa alizonazo, mahabusu huyo hakuumia kutokana na kipigo cha askari, bali alianguka kutoka kwenye ngazi za karandinga lenye namba STH 2929 lililowachukua kutoka mahabusu ya Bangwe mjini hapa.

Awali mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa baada ya karandinga la Polisi kuwasili mahakamani hapo, mahabusu hao waligoma kushuka na badala yake walianza kupiga kelele huku wakifunga mlango wa kutokea katika gari hilo ili kuzuia askari kushindwa kuwashusha.

Hali hiyo iliwalazimu askari walioongozana na gari hilo kulipeleka Kituo Kikuu cha Polisi mjini Kigoma na hapo walianza kupewa kipigo ili kuwafanya kulainika na kuruhusu ratiba ya siku kuendelea.

Kutokana na fujo walizofanya mahakamani, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa, Emanuel Mrangu amewahukumu kifungo cha miezi sita mahabusu watatu wanaotuhumiwa kwa makosa ya mauaji, kwa kufanya fujo wakilalamika kesi yao kuchukua muda mrefu bila kutolewa hukumu.

Waliohukumiwa kifungo hicho ni Maneno Kichako, Majuto Dunia na Haruni Petro ambao inadaiwa walikuwa vinara wa mgomo wa kushuka na kufanya fujo wakishinikiza wenzao kutoingia mahakamani.

Mrangu aliwahukumu kifungo hicho cha miezi sita jela watuhumiwa hao kwa kosa la kufanya fujo mahakamani na kusema kuwa kama walikuwa na madai yao kuhusu kucheleweshwa kwa mwenendo wa kesi zao, walipaswa wapeleke malalamiko hayo kwa kufuata taratibu za kimahakama, lakini si kufanya fujo mahakamani na hivyo kesi mbalimbali zilizokuwa zikiendeshwa kusimama kwa muda.

Aidha, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mrangu alisema amewasiliana na uongozi wa Magereza Mkoa kuona namna gani suala kama hilo linapatiwa ufumbuzi ikiwamo mchakato wa kesi kuchukua muda mrefu huku akitoa angalizo la kuwataka maofisa Magereza kuandika barua za maombi wa mwenendo wa kesi kukumbusha kushughulikiwa kwa kesi ambazo zimechukua muda mrefu bila kumalizika.


0 comments:

Post a Comment