Tuesday, October 30, 2012

Habari imeandikwa na Nurdin Selemani Ramadhani via RFI Kiswahili

Watu watatu wamepoteza maisha nchini Kenya katika Mji wa Kisumu kufuatia kuzuka kwa machafuko kutokana na kuuawa kwa mwanasiasa maarufu katika eneo hilo kitu ambacho kilizusha hasira kwa wafuasi wake walioingia barabarani na kuanzisha fujo.

Watu hao watatu wanatajwa kupoteza maisha wakiwa kwenye duka lao lililoshika moto wakati Jeshi la Polisi likiendelea na juhudi zake za kukabiliana na waandamanaji wenye hasira waliovamia mitaa ya Kisumu.

Ghasia zilizuka Jiji Kisumu baada ya kuzagaa kwa taarifa za kuuawawa Mwanasiasa Shem Onyango Kwega ambaye alitangaza nia ya kugombea ubunge kwenye Uchaguzi utakaofanyika hapo mwakani mwezi Machi.

Kwega inatajwa aliuawa na watu wenye silaha wasiojulikana kitu ambacho kilichangia hasira kwa wanachama wa Chama Cha ODM ambacho kinaongozwa na Waziri Mkuu Raila Odinga.

Kwega alikuwa ni Mwenyekiti wa ODM huko Kisumu na kuungwa mkono na wafuasi wengi na kwenye tukio la kuuawa kwake kilisababisha mkewe kushambuliwa na anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospital ya Kisumu.

Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Polisi katika Mkoa wa Nyanza Joseph Oli Tito amethibitisha kuibuka kwa vurugu hizo na kusababisha vifo vya watu watatu ambao walikuwa kwenye duka moja.

Tito amekanusha Jeshi la Polisi kuhusika kusababisha vifo vya watu hao baada ya mashuhuda kusema bomu la machozi walilorusha ndilo lilisababisha kuzuka kwa moto huo wakati vijana hao wakiwa ndani.

Afisa huyo wa Polisi amesema wanaamini kilichochangia kutokea kwa vifo hiyo ni hitlafu ya umeme ambayo ilizuka kwani vifo hivyo vilitokea wakati wao wakiwa mbali na eneo linalotajwa.

Mji wa Kisumu ulikuwa ni moja ya maeneo ambayo yalikumbwa na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja kwenye vurugu zilizokuwa zinapinga ushindi wa Rais Mwai Kibaki.0 comments:

Post a Comment