Sunday, October 21, 2012

JESHI la Polisi Zanzibar limesema halihusiki ka kupotea kwa kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho, Farid Hadi Ahmed ambaye alionekana usiku juzi majira ya saa 2.15 na kuonana na familia yake hapo Mbuyuni.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo Ziwani Mjini, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa alisema jeshi lake halihusiki kwa namna yoyote ya kuchukuliwa kwa Shekhe Farid katika mazingira ya kutatanisha.

“Jeshi la Polisi linakanusha kuhusika katika sakata la kutekwa kwa kiongozi wa Uamsho... tunamhoji kujua ukweli katika tukio hilo zima,” alisema Mussa.

Shekhe Farid alihojiwa na Jeshi la Polisi baada ya kujisalimisha kufuatia kuwepo kwa taarifa za kupotea katika mazingira ya kutatanisha na kupelekea kuibuka kwa fujo na vurugu kutoka kwa wafuasi wake.

Hata hivyo, haijafahamika kama Jeshi la Polisi litachukuwa hatua gani baada ya kumaliza kazi za kufanya mahojiano na kiongozi huyo wa Uamsho, ambapo katika siku nne ya kutoweka kwake matukio mbalimbali yaliibuka ikiwemo kifo cha polisi mmoja na wananchi kufanya vitendo vya uporaji wa mali.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo Mbuyuni, Farid alisema hakutekwa, lakini alichukuliwa na Jeshi la Polisi na vikosi vya Usalama wa Taifa wakimhoji kuhusu harakati zake za kuitetea Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano.

---
via HabariLeo.co.tz

0 comments:

Post a Comment