Friday, October 19, 2012

Mabina apinga ushindi wa Diallo
Habari imeandikwa na David Azaria, HabariLeo, Mwanza

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina ameyakataa matokeo yaliyompa ushindi aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo na kutangaza kukata rufaa Makao Makuu ya chama hicho tawala akipinga kupoteza wadhifa huo.

Mabina alitangaza nia ya kupinga matokeo hayo juzi saa moja usiku kwenye Uwanja wa CCM Kirumba baada ya Diallo kutangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, William Lukuvi kuwa mshindi kwa kura 611 kati ya kura 998 zilizopigwa.

Mabina alipata kura 328. Akizungumza wakati wa kuwashukuru wanaCCM, Mabina alisema hakuridhika na matokeo ya uchaguzi huo kwa madai kuwa baadhi ya wagombea akiwamo mshindi walikiuka kanuni za uchaguzi kwa kufanya baadhi ya matendo ambao ni kinyume cha Kanuni za uchaguzi wa CCM.

“Sikuridhika na sitaridhika na matokeo ya uchaguzi huu, kwa sababu baadhi ya kanuni zimekiukwa na, rushwa zimetembea kwa wingi, lakini kibaya zaidi baadhi ya wagombea walikuwa wakizunguka na kufanya mikutano ya kampeni kinyume na kanuni na kuzungumza na wagombea, hili ni kosa ambalo pamoja na mengine yananifanya nisikubaliane na matokeo,” alisema na kuongeza: “Nakusudia kukata rufaa kwa Kamati Kuu ili niweze kupata haki yangu kwa sababu naona imepokonywa kwa makusudi na naamini kwamba Kamati Kuu itanitendea haki kwa sababu ushahidi ninao.”

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa zamani alipata wakati mgumu kwa kuzomewa na hivyo kukatisha maelezo yake mara kwa mara na wapigakura kumtaka ashuke jukwaani, lakini aliendelea kutoa maelezo huku akiwaambia kuwa hata wakizomea, ni lazima akate rufaa hata kama yeye hatagombea.

Kwa upande wake, Lukuvi alisema anachofahamu na anachoamini ni kwamba uchaguzi huo umeanza na kukamilika vizuri ambapo haukuwa na kasoro yoyote kama ambavyo kura zimeonesha, ingawa alibainisha kuwa rufaa ni haki ya mgombea yeyote anayeona hakuridhika na mwenendo wa uchaguzi.

Alipoulizwa kuhusu tuhuma alizotwishwa na Mabina za ukiukwaji wa kanuni, Diallo alisema anaamini Mabina atakuwa amepata mshituko kutokana na matokeo ambayo hakuyategemea ndiyo maana ametamka maneno hayo, na kwamba akitulia na akili kukaa sawasawa, hatakuwa na mawazo hayo.

Rushwa yavunja uchaguzi CCM Pwani
Habari imeandikwa na Julieth Ngarabali, Mwananchi, Kibaha

TUHUMA za kushamiri kwa vitendo vya rushwa katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM mkoani Pwani, juzi vilimlazimisha mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Mwinshehe Mlao kuvunja mkutano huo.

Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike kwenye Jengo la Mkuu wa Mkoa wa Pwani, uliahirishwa saa chache, kabla ya upigaji kura kuanza kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba baadhi ya wajumbe walikuwa wakitoa na kupokea rushwa ili kushawishi ushindi wa baadhi ya wagombea.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza aliwaeleza wajumbe hao kuwa amepata taarifa kutoka vyombo vya usalama kuwa uchaguzi huo umegubikwa na vitendo vinavyoashiria kuwapo na rushwa.

Akiahirisha mkutano huo jana, Mlao alisema amelazimika kusitisha uchaguzi huo hadi utakapotangazwa tena, kutokana na baadhi ya wajumbe kukidhalilisha chama kwa kujihusisha na rushwa, “Kwa haya yaliyotokea lazima tuwasiliane na wenzetu makao makuu. Baada ya kusema haya natangaza kuahirisha kikao hadi tarehe ya uchaguzi itakapotangazwa tena,” alisema Mlao.

Akizungumza katika mkutano huo, Mahiza alilaani kitendo hicho akisema kuwa kimeidhalilisha CCM na ofisi yake.

Awali Mahiza alisema kuwa alipata taarifa kutoka kwa maofisa wa Takukuru kuhusu kuwapo kwa mazingira ya rushwa yanayofanywa na wajumbe wa mkutano huo na baadaye alifika katika ukumbi wa mkutano, “Baada ya kupata taarifa kuhusu mazingira ya rushwa, nilitoka nje na kweli ukumbini sikukuta watu. Niliposhuka chini niliwakuta wajumbe wengi wakiwa wamesimama makundi. Sikujua na wala sikushuhudia nani aliyekuwa anatoa rushwa ila maofisa wangu wameliona hilo," alisema Mahiza na kuongeza:  "Najua nitabeba lawama kubwa sana, nitatukanwa sana na baadhi yao, lakini hili sitalivumilia.”

Nafasi iliyodaiwa kuwa ndiyo iliyokuwa ina wagombea waliokuwa wakichuana vikali zaidi ni katibu wa uchumi ambayo wagombea wake ni, Imani Madega na Haji Abuu Jumaa.

Baada ya kuahirishwa kikao hicho,  Mahiza alifanya kikao cha ndani na wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa (NEC) wa mkoa huo, Ridhiwan Kikwete na Rugemalila Lutatina.

Alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema, " Waseme wenyewe wa Pwani. Kama imetokea leo siwezi kupata taarifa leo...," "...Kama imetokea wataleta taarifa, zikifika tutakuwa na cha kuzungumza, lakini leo waache waseme wao kwanza."

0 comments:

Post a Comment