Saturday, September 22, 2012

Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA Mbelgiji Tom Saintfiet amefukuzwa usiku huu, baada ya kutofautiana sera na uongozi wa Yanga na sasa Fredy Felix Minziro, aliyekuwa Msaidizi wake, atakaimu nafasi yake.
Habari zaidi, kuhusu kufukuzwa kwa kocha huyo, Yanga itatoa taarifa rasmi kesho asubuhi saa 3:00, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.Mapema leo mchana, uongozi wa Yanga ya Dar es Salaam, ulitangaza kuisimamisha kazi Sekretarieti nzima ya klabu, akiwemo Katibu Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu, kutokana na kile ilichoeleza utendaji usioridhisha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba maamuzi hayo yamefuatia kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika tangu saa 5:30 leo hadi saa 9:30.
Wengine wanaokumbwa na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu mengine.

“Tumesitisha mikataba ya sekretarieti nzima, pia tumefanya marekebisho, tumemtoa Meneja wa timu na muda si mrefu tutamtangaza Meneja mwingie pamoja na sekretarieti mpya,”alisema Sanga. 
Aidha, Sanga alisema Kocha Mbelgiji, Tom Saintfieti anapewa onyo kali kwa kuzungumza ovyo na vyombo vya habari.“Tumekwishakutana naye mara kadhaa kumpa utaratibu wa kuzungumza na vyombo vya habari, sasa tutamuandikia barua ya kumkumbusha wajibu wake na kuzingatia wajibu wake, kutozungumza na vyombo vya habari holela,”alisema.

Kwa ujumla maamuzi haya yanakuja baada ya Yanga kuanza vibaya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikiambulia pointi moja tu katika mechi zake mbili za awali, kutokana na sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Jumamosi na Jumatano ikachapwa mabao 3-0 Morogoro Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.Sasa beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Lawrence Mwalusako atakaimu nafasi ya Katibu wa klabu hiyo, kufuatia kusimamishwa kwa Celestine Mwesigwa, wakati kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Johnson Chambua atakuwa Meneja mpya wa klabu hiyo, akirithi mikoba ya Hafidh Saleh.

Habari kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba viongozi hao wapya watatangazwa wakati wowote kuanzia sasa kurithi nafasi za viongozi walioondolewa madarakani, kutokana na kile kilichoelezwa utendaji usioridhisha.
Nafasi nyingine za Mhasibu mpya, iliyoachwa wazi na Philip Chifuka itakuwa chini ya dada mmoja, aliyetajwa kwa jina moja tu, Rose aliyekuwa akifanya kazi ofisi hiyo kwa muda mrefu, wakati Msemaji wa klabu iliyoachwa wazi na Louis Sendeu, inaelezwa atapewa mdogo wa mke wa Ridhiwani Kikwete, aliyehesabu kura za Abdallah Bin Kleb katika uchaguzi mdogo wa klabu, Julai 14.

Saintfiet amefungwa mechi mbili Yanga katika mechi 14 alizoiongoza timu hiyo tangu ajiunge nayo, Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic.Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi.  

REKODI YA SAINTFIET YANGA
1.     Yanga Vs JKT Ruvu             (Kirafiki)                    2-0
2.     Yanga Vs Atletico (Burundi, Kagame)               0-2
3.     Yanga Vs Waw Salam (Sudan, Kagame)          7-1
4.     Yanga Vs APR (Rwanda, Kagame)                     2-0
5.     Yanga Vs Mafunzo (Z’bar, Kagame)                 1-1 (5-3penalti)
6.     Yanga Vs APR (Rwanda, Kagame)                     1-0
7.     Yanga Vs Azam (Kagame)                                    2-0
8.     Yanga Vs African Lyon (Kirafiki)                         4-0
9.     Yanga Vs Rayon (Kirafiki, Rwanda)                   2-0
10.                        Yanga Vs Polisi (Kirafiiki, Rwanda)        2-1
11.                        Yanga Vs Coastal Union    (Kirafiki)        2-1
12.                        Yanga Vs Moro United      (Kirafiki)        4-0
13.                        Yanga Vs Prisons    (Ligi Kuu)                  0-0
14.                        Yanga Vs Mtibwa (Ligi Kuu)                     0-3

0 comments:

Post a Comment