Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Singida Mohammed Likwata akizungumza na mwandishi wa habari wa AIM MEDIA (hayupo pichani).
Mfanyabiashara wa bodaboda akivunja sheria ya usalama barabarani ya kupakia zaidi ya abiria moja kama alivyonaswa kwenye kituo kikuu cha mabasi mjini Singida.(Picha zote na Ayoub Mangi).
Na mwandishi wetu
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Singida Mohammed Likwata amewaonya madereva wa boda boda kuacha mara moja tabia ya kutumia pombe aina ya konyagi viroba, kwa madai kuwa inachangia ajali za barabarani.
Likwata ametoa onyo hilo wakati akizungumza na AIM MEDIA juu ya utaratibu wa kikosi cha Usalama barabarani kuendelea kutoa elimu ya sheria za usalama barabani kwa madereva wa bodaboda mkoani Singida.
Amesema uchunguzi uliofanywa na kikosi chake, umebaini baadhi ya madereva wa boda boda wana tabia ya kunywa pombe kali ya viroba (konyagi) wanapokuwa kwenye vituo vyao, wakisubiri abiria.
Amesema ni kosa kisheria kuendesha chombo cha moto ukiwa umelewa kwa hiyo dereva wa boda boda akikamatwa anatumia viroba wakati wa kazi, atakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Pombe inaweza pia kuwasababishia wao wenyewe, abiria na watumiaji wengine kupata madhara makubwa ikiwemo kifo na uharibifu wa mali kama ajali itatokea.
Katika hatua nyingine, Likwata amewataka wamiliki wa piki piki zinazofanya biashara za kusafirisha abiria, kutoajiri madereva ambao hajapata mafunzo ya udereva.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa usalama barabarani mkoani Singida pekee una boda boda 231.