Wednesday, June 13, 2012

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kuanzia sasa litaanzisha utaratibu wa kuwakatia bima ya afya michezoni wachezaji watakaoitwa kuunda kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars).

Uamuzi huo ambao ni sehemu ya mkakati kuwatia hamasa wachezaji na kuwajengea uwezo wa kujituma, umekuja siku chache tangu Stars iibuke na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia katika mchezo wa kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, msingi mkuu wa hatua hiyo pia unalenga kutoa fursa ya kupatiwa matibabu mazuri wachezaji wa Stars wanapopata matatizo ya afya.

Tenga alisema anaamini ili mchezaji aweze kuiwakilisha vizuri nchi yake, suala la afya bora na matibabu ya uhakika anapopata matatizo ni mambo yasiyokwepeka kutekelezwa.
Aidha, katika kuwaongeza hamasa na kujituma kusaka ushindi, kuanzia sasa wachezaji watakuwa wanapata asilimia 15 ya mapato ya uwanjani, asilimia 7 iwapo watatoka sare na hawatapata kitu wakipoteza mchezo.
 
"Kiini cha uamuzi huu ni kuwaongezea hamasa vijana wetu, na TFF itaendelea kuwajengea mazingira mazuri yatakayowafanya kucheza kwa kujituma kusaka ushindi kwenye mashindano mbalimbali.
"Tunafahamu bado tuna kazi kubwa mbele yetu na hata hapa tulipofikia ni baada ya kubadili mwelekeo unaosisitiza nidhamu na uwajibikaji wa pamoja," alisema Tenga.

Aidha, Tenga alisema TFF itajivika jukumu la kuwatafuta wataalamu mbalimbali wa masuala ya maisha na saikolojia ili kuzungumza na wachezaji wa Stars na lengo ni kuwawezesha kujiamini na kujitambua.
Kuhusu mchezo wa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia, Tenga alisema: "Kwa hakika uwezo walionyesha wachezaji unastahili pongezi kwa kuweza kucheza dakika 90 bila kuchoka tofauti na siku nyingine."

Pia alipongeza taswira ya uzalendo iliyoonyeshwa na mashabiki wa soka walioshuhudia mechi hiyo ya Stars kwa moyo wa shikamano uliotambua utaifa tofauti na hapo awali ambapo baadhi walikuwa wakizomea.
Amewataka kuendelea kufanya hivyo katika mechi zote hata kama timu hiyo ikifanya vibaya sababu haiwezi kuwa inashinda kila siku.
"Ningeomba na Jumamosi mjitokeze kwa wingi kuishangilia timu yetu ya taifa wanawake (Twiga Stars) itakapocheza na Ethiopia," alisema bosi Tenga.

0 comments:

Post a Comment