Monday, June 18, 2012

WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imesema kuwa umasikini uliokithiri miongoni mwa jamii ni moja ya chanzo cha wimbi kubwa la watoto wa mitaani.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Elisante ole Gabriel, alitoa kauli hiyo juzi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyoandaliwa na Shirika la Hope for the Children Organization.

Akizungumza kwa niaba yake, ofisa mwandamizi wa idara hiyo, Focas Kapinga, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa jukumu la kuwalea watoto hao ni la Watanzania wote.
Kwamba umasikini umekuwa ukichangia hali hiyo ya watoto wa mitaani kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kuzihudumia familia zao ipasavyo, matokeo yake watoto huamua kukimbilia mitaani kwa matumaini ya kupata maisha bora.

Kapinga alisema kuvunjika kwa ndoa kumekuwa kukisababisha familia kushindwa kukidhi mahitaji muhimu kwa watoto, kama vile elimu, chakula, mavazi hali inayowalazimisha kuondoka majumbani kwao.
Alibainisha kuwa, wizara hiyo ndiyo yenye jukumu la maendeleo ya vijana, wakiwemo watoto, na kwamba dhamira yao ni kukabiliana na mambo yanayosababisha watoto kukimbilia mitaani.
“Wizara imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa kama vile UNICEF, ILO, UNEPA, UNDP na ya watu binafsi yaliyoko nchini na taasisi za dini katika kutimiza azma yake,” alisema.

Kapinga alibainisha kuwa, jitihada hizo ni pamoja na utoaji wa elimu ya ujasiriamali, stadi za maisha na mikopo kwa vijana yenye masharti nafuu.
Awali Mkurugenzi wa Hope for the Children Organization, Joyce Mang’o, alisema pamoja na mipango mingi ya serikali, lakini bado imekuwa ikitoa mchango hafifu wa kupambana na tatizo hilo.
Alisema sheria zilizopo hazilengi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa asasi na watoto pia, jambo linalosababisha asasi kuwa na utendaji hafifu usiokidhi haja na matakwa kwa wahusika.

0 comments:

Post a Comment