Monday, June 11, 2012












Nyota wa Argentina,Lionel Messi
NEW JERSEY, Marekani
MSHAMBULIAJI Lionel Messi alifunga mabao matatu katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Brazil, ambapo Argentina iliichapa Brazil 4-3.

Katika mechi hiyo Brazil ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Romulo katika dakika ya 23 huku Uwanja wa MetLife ukiwa umejaa mashabiki wa soka 81,994.

Lakini Mesi aliisawazishia Argentina katika dakika 31 na kufunga bao la kuongoza katika dakika 34.

Mchezaji wa Brazil, Oscar aliisawazishia timu yake bao katika dakika ya 56 na Hulk akaipatia Brazil bao la kuongoza ya 72.

Dakika tatu baadaye Argentina walisawazisha bao hilo mfungaji akiwa Federico Fernandez akiunganisha kona iliyopigwa na Sergio Aguero.

Katika dakika ya 84, Messi alichukua mpira katikati ya uwanja na kusogea nao, ambapo alipiga shuti la umbali wa mita 21 ambalo lilikwenda moja kwa moja nyavuni na kuiandikia Argentina bao la nne la ushindi.

Wakati huo huo katika mechi za kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa nchi za Marekani ya Kusini, timu ya Chile iliichapa mabao 2-0 Venezuela huku mabao ya Chile yakifungwa na Matias Fernandez na Charles Aranguiz.

Matokeo ya mechi nyingine za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia ni kwamba Bolivia iliichapa Paraguay mabao 3-1 wafungaji wa Bolivia wakiwa Alcides Pena na Pablo Escobar aliyefunga mabao mawili. Bao la Paraguay lilifungwa na Cristian Riveros.

0 comments:

Post a Comment