Tuesday, June 12, 2012

Sosthenes Nyoni
HAKUNA shaka ushindi wa mabao 2-1 walioupata Taifa Stars dhidi ya Gambia umewafurahisha wengi, lakini hata hivyo mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita umeacha kumbukumbu ya matukio kadhaa yanayovutia na kustaajabisha pia.

Bendera ya Tanganyika uwanjani:
Miongoni mwa matukio yasiyokuwa ya kawaida yaliyojiri kwenye mchezo huo ni kitendo cha mashabiki wa soka nchini walioketi jukwaa la mashariki walionekana wakishangilia mabao yote mawili ya Taifa Stars huku wakipeperusha Bendera ya Tanganyika.


Hakuna Usimba wala Uyanga:
Tukio la kupendeza na kufurahisha ni kukosekana tofauti za kiitikadi katika kushangilia miongoni mwa mashabiki waliofika uwanjani kinyume na siku za hivi karibuni, ambapo mechi za Stars zimekuwa zikiwagawa mashabiki, baadhi wakishangilia na wengine wakizomea.

Mashabiki Gambia waukimbia Uwanja:
Katika hali ya kushangaza kikundi kidogo cha mashabiki wa timu ya taifa ya Gambia kilichokuwa upande wa Kaskazini wa uwanja kiliondoka uwanjani hapo baada ya beki Erasto Nyoni kufunga penati dakika ya 85 iliyoipa Stars bao la ushindi.

Gambia wamganda mwamuzi:
Ama kweli kipigo kinauma. Hii ilidhihirika baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa ambapo, wachezaji wa Gambia walimvaa mwamuzi kwa jazba kutokana na kile kilichoonekana kupinga penalti ya Taifa Stars.

Kaseja awashukuru mashabiki Yanga:
Tukio jingine lililosisimua uwanjani hapo ni lile lililotokea baada ya pambano kumalizika, ambapo kipa Taifa Stars, Juma Kaseja alipokwenda kwenye jukwaa wanaloketi mashabiki wa Yanga na kuwapigia makofi kama ishara ya kuwashukuru kwa uzalendo waliouonyesha kwa nchi yao na kuweka unazi pembeni na mashabiki hao wa Yanga walijibu kwa kumpigia makofi na kumshangilia.

Kocha Gambia adondosha chozi:

Matukio ya aina yake kwenye pambano hilo yalikamilishwa na kitendo cha kocha wa Gambia Luciano Mancini kumwaga chozi hadharani baada ya pambano hilo na kusababisha viongozi wengine wa benchi la ufundi la timu yake kufanya kazi ya ziada ya kumtuliza.
Wakati huohuo, mchezo huo wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 uliingiza kiasi cha Sh124 Milioni zilizotokana na viingilio vya watazamaji 31,122.
Viingilio kwenye mchezo huo vilikuwa Sh3,000, 5,000, 10,000, 20,000 na 30,000.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kuwa mashabiki 25,901 walikata tiketi za Sh3,000.

Alisema asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni Sh18.9 Milioni ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa Sh6.5 Milioni.
Alisema bonasi kwa Taifa Stars ni Sh15.5, waamuzi Sh13.3, usafi na ulinzi Sh2.3 Milioni, maandalizi ya uwanja Sh400,000,, Wachina- Beijing Construction Sh2 Milioni, umeme Sh300,000 na mafuta ya jenereta Sh200,000.

0 comments:

Post a Comment