Monday, June 18, 2012

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la PEN-TRUST lenye makao yake makuu katika mji wa Minesota nchini Marekani linatarajia kutoa msaada wa umeme wa nishati ya jua katika shule za sekondari za kata kumi mkoani Singida.
Mwenyekiti wa shirika hilo nchini, Athumani Mungwe alisema shule hizo kumi zitakazopokea msaada huo ni kati ya sekondari 156 zilizopo mkoani hapa.

Alizitaja shule zitakazonufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza kuwa ni Ikhanoda, Mwasauya, Mughamu, Itaja na Maghojoa.
Nyingine ni Mikiwu, Madasenga, Makuro, Matumbo na Merya.
Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone licha ya kukiri kupokea misaada mingi kutoka kwenye shirika hilo, hakusita kuwasilisha ombi jingine la vitabu kwa ajili ya shule za msingi zilizopo mkoani hapa.

Hata hivyo, Dk. Kone alifafanua kwamba alishiriki katika kutoa wazo la shirika hilo kuweka nishati ya umeme wa jua katika shule za sekondari kwa kupendekeza kuanzishwa kwa maktaba katika shule za sekondari na kuweka huduma hiyo ya umeme wa sola.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa huyo hakusita kusisitiza umuhimu wa kuwakumbuka watu wenye ulemavu kwa madai kwamba ni kundi ambalo bado linahitaji kukumbukwa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na makundi mengine ya jamii.

0 comments:

Post a Comment