Sunday, June 10, 2012


 Ibrahim Yamola 
CHAMA Cha Madaktari Tanzania (MAT) kimetangaza mgogoro na Serikali na kuipa wiki mbili kuyapatia ufumbuzi matatizo yao la sivyo watafanya mgomo wa nchi nzima.  Wametoa msimamo huo walipokutana jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya ujumbe wao uliokuwa kwenye mazungumzo na Serikali kugoma kusaini makubaliano kwa kile walichoeleza mpaka wapate ruksa ya wanachama.  Jana ilikuwa ni siku ya ujumbe huo kuwasilisha taarifa ya makubaliano ambayo Serikali ilitaka waisaini na hivyo wanachama hao hawakuyaridhia hivyo kuamua kutangaza mgogoro.
 Habari zilizoifikia Mwananchi Jumapili kutoka ndani ya kikao hicho cha ndani zilieleza kuwa madai ambayo 
Serikali imeshindwa kuyatekeleza ni nyongeza ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi, marupurupu, nyongeza ya posho ya wito wa dharura, posho za nyumba na chanjo.
 Mkutano huo ambao uliwashirikisha madaktari pamoja na viongozi wa chama hicho walikubaliana kutangaza mgogoro wa wiki mbili na baada ya hapo wataingia katika mgomo ili kuishinikiza Serikali kuyapatia ufumbuzi madai yao.
 Walidai kuwa kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ilishindwa kuyatatua matatizo yao kwa kigezo kwamba Serikali haina uwezo wa kifedha.
 
 “Hata kama Serikali ingekuwa na fedha isingeweza kuongeza mishahara kama ambavyo tunataka kutokana na madai kwamba itasababisha migogoro na watumishi wengine,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya mkutano huo wa madaktari.
 Madaktari hao walilalamika kwamba ahadi iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwenye mkutano wao ya kuhakikisha madai yao yanashughulikiwa kikamilifu wakati akiwataka warejee kazini baada ya mgomo waliofanya Januari mwaka huu, haikutekelezwa. 
 “Haiwezekani Serikali imeshindwa kutatua madai yetu hata moja na sisi tuendelee kukaa kazini hii ni dharau na kitakachofanyika ni kurudi kama tulivyofanya awali na itakuwa zaidi ya mgomo tulioufanya,” alisikika akilalamika mmoja wa wajumbe kwenye mkutano huo.
 
Walielezea kushangazwa kwa tabia ya Serikali kutotekeleza ahadi zake hadi pale watu wanapochukua hatua mbadala, kama vile kuandamana na kugoma.
 Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema wamekubaliana waendelee kufanya migomo kushinikiza kukubaliwa matatizo yao.
 Walidai kuwa Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa mazoea na wakati mwingine ikiingiza siasa katika masuala ya msingi kitu ambacho ni hatari kwa jamii na taifa kwa ujumla.
 Wanasema serikali imeshindiwa hata kuwapatia chanjo ya kuwakinga na maambukizo ya magonjwa mbalimbali wakiwa kazini.
 
“Serikali kweli imeshindwa hata kutufanyia chanjo na kusema itafanya hivyo kwa awamu huu ni uuaji kwani tunafanya kazi katika mazingira magumu, lakini inashindwa kututhamini,” alilalamika daktari huyo.  Walionya kuwa Serikali isipokuwa sikivu kwa safari hii watafanya mgomo ambao utakuwa mbaya kuliko ule uliofanyika awali na kusababisha taharuki kubwa kwenye hospitali nchini hususan Muhimbili.
 Hata hivyo, baadaye Mjumbe wa MAT, Dk Godbless Charles aliwaambia waandishi wa habari kuwa walichoamua wanachama katika mkutao wasio ni mrejesho wa tathmini ya taarifa ambayo ilitolewa na Serikali baada ya kikao kilichofanyika Machi 31 mwaka huu. 
“Sisi tumewapelekea na wao wakataka irudi mezani na kupitiwa upya madai kabla ya wiki mbili na yawe yamepatiwa ufumbuzi,” alisema Dk Charles.
 
 Akielezea juu ya mazungumzo yao alisema: “Tangu kamati hiyo ilipoundwa na Waziri Mkuu ili kushughulikia madai yetu, tumekutana mara sita na mara zote tulishindwa kufikia mwafaka. “Baada ya kurejesha taarifa ambazo hazikuwa na majibu ndio maana tukaamua kuitisha kikao cha ndani ili wanachama waamue wenyewe wasije kutuona tunawasaliti,” alisema.
 
 Rais wa MAT,  Dk Namala Mkopi alikiri kwamba wanachama wamekubaliana kutangaza mgogoro wa wiki mbili na serikali na baada ya hapo watapanga hatua za kuchukua.”
 Mgomo uliofanyika Januari mwaka huu ulisababisha vifo kwa wananchi kwa kukosa huduma ambapo Waziri Mkuu Pinda aliwasimamisha kazi mara moja Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na 
Mganga Mkuu Dk Deo Mtasiwa.  Madai mengine ya madaktari hao ilikuwa ni kuwang’oa mawaziri jambo ambalo Rais Kikwete alilitekeleza kwa kutowarejesha kwenye Baraza alilolisuka upya kwa kuteua wengine.

0 comments:

Post a Comment